Kabla ya mechi tatu za jana, Mtibwa Sugar ikiikaribisha Tanzania Prisons, Mbeya City ikiwa mwenyeji wa Mbeya Kwanza FC na Namungo FC ikiwa nyumbani kuialika Kagera Sugar, hakuna timu yoyote ilishinda zaidi ya mabao mawili kwenye mechi hizo za awali, jambo ambalo linaonyesha itakuwa ni ligi ngumu zaidi msimu huu.
Lakini hadi sasa ni timu ya Polisi Tanzania pekee iliyoongoza kwa kushinda mechi zote mbili kwa mabao mawili, ikianza kwa kuichapa KMC FC mabao 2-0 kisha ikapata ushindi wa 2-1 dhidi ya Azam FC. Timu nyingine ni Namungo ambayo iliifunga Geita Gold mabao 2-0 na zingine zote zikipata ushindi wa bao moja, suluhu ama sare 1-1.
Ugumu na ushindani huo mkubwa ndio tunaoutaka katika ligi yetu kwani utaongeza mvuto, hivyo kuvutia wawekezaji wengi na hatimaye kuinua vipato vya wachezaji na klabu kwa ujumla, hivyo hauna budi kulindwa na kusimamiwa kwa makini zaidi kutoka kwa wote wenye dhamana na soka letu hususan Shirikisho la Soka Mpira wa Miguu nchini (TFF) kwa kushirikiana na Bodi yake ya Ligi, TPLB.
Hata hivyo, tayari kumeibuka wanasiasa mbalimbali ambao wamekuwa wakiahidi na kutoa motisha kwa baadhi ya klabu za mikoa yao ama wanayoiongoza au walipozaliwa, wakiweka donge nono mezani kama zikishinda kwa baadhi ya timu.
Kwa hakika si jambo baya, lakini kwa namna ahadi hizo zinavyotolewa, kama zikiachwa kuendelea hivyo kuna uwezekano mkubwa tukashuhudia ligi mbaya zaidi ya ukiukwaji wa kanuni kwa kupanga matokeo.
Mechi ya Biashara United dhidi ya Simba katika Uwanja wa Karume mjini Musoma, Mkuu wa Mkoa wa Mara, Ally Hapi aliahidi timu hiyo ikishinda dhidi ya mabingwa hao watetezi atatoa motisha wa Sh. milioni 15 na endapo itatoka sare ataipa milioni 10, ahadi ambayo aliitekeleza kwa kutoka suluhu katika mchezo huo.
Lakini pia wakati Dodoma Jiji FC ikiikaribisha Simba, Mbunge wa Dodoma Mjini, Anthony Mavunde, aliahidi kuipa donge kama hilo kama itaibuka na ushindi, lakini ikalikosa baada ya 'Wekundu wa Msimbazi' hao kushinda bao 1-0. Nipashe tunaamini ni ahadi nzuri kwa kuongeza motisha kwa wachezaji, lakini kwa nini iwe zinapocheza na Simba pekee, badala ya kutolewa kwa angalau kila inaposhinda mchezo wake wa nyumbani na ikiwezekana hata ugenini?
Tunasema hivyo, hasa kwa kutambua si suala la kufichika kwamba Simba na Yanga zimeigawa nchi katika makundi mawili, hivyo viongozi wa timu hizo upande mmoja unaweza kwa nia ovu kabisa wakatumia mwanya huo wa mashabiki ama wanachama wao viongozi wakisiasa kwa mgongo kwamba ni timu zao, kupenyeza fedha za kupanga matokeo kwa madai ni motisha kutoka kwa viongozi wa mikoa yao.
Hilo ni moja lakini, waamuzi nao hawana budi kufuata kanuni na sheria 17 za soka hususan usalama wa kulinda afya za wachezaji uwanjani kwani kwa namna tulivyoshuhudia rafu mbaya zilizoonyeshwa na timu hizo baada ya kuahidiwa motisha huo, ni wazi kuna dalili msimu huu baadhi wakapata majeraha mabaya yanayoweza kuwasababishia kushindwa kucheza soka kabisa.
Katika hilo tulishuhudia mechi mechi hizo mbili wachezaji watano wa Simba wakishindwa kuendelea na mechi kutokana na kuchezewa rafu mbaya, hivyo ni wakati pia kwa TFF na TPLB kutupia waamuzi jicho mapema ili kuhakikisha wanalinda afya za wachezaji kwa kuchezesha kwa haki.
Kama tunataka tuwe na ligi bora zitakazowavutia mashabiki na wawekezaji pia, ni lazima waamuzi wanapaswa kuacha woga na kutoa kadi iwe ya njano ama nyekundu hata kama ni mwanzo wa mchezo, pale inapostahili kufanya hivyo.










