Kubwa wanalolilalamikia ni gharama wanayoingia kutafuta usafiri wa kuwafikisha kwenye maeneo yao wanayoishi hasa wanapoingia jijini Dar es Salaam usiku mwingi.
Malalamiko kutoka kwa baadhi ya wasafiri ni kitendo cha baadhi ya kampuni za usafirishaji kuamua kuwarahisishia gharama ya usafiri abiria wao kuanzia safari kwenye ofisi za mabasi yao hadi kwenye kituo kikuu cha Mbezi.
Hata hivyo, imedaiwa kuwa kampuni hizo zimepigwa marufuku kuchukua abiria kwenye vituo vya ofisi zao na badala yake abiria wawakute kwenye kituo kikuu kilichopangwa ambacho ni Mbezi.
Maswali yanayoibuka kwa baadhi ya wadau ni kuwa kwanini basi liondoke likiwa tupu hadi Mbezi ilihali kuna abiria wanaoishi maeneo ya karibu na ofisi zao ambao wangeweza kuwasaidia kwa kuwarahishia usafiri.
Vivyo hivyo, malalamiko yamekuja kwa abiria wanaotoka mikoani kulazimika kushukia kituo cha Mbezi na kutafuta usafiri mwingine wa kuwafikisha majumbani kwao.
Kilio kinachotolewa na wananchi wengi ni muda wa baadhi ya mabasi yanayoingia kutoka mikoani kuwa ni usiku mwingi na gharama wanazoingia kupata usafiri wa kuwafikisha makwao kuwa zaidi ya mara mbili ya nauli waliyolipia tiketi. Yaani unaweza ukatoka Morogoro hadi Dar es Salaam kwa gharama ya tiketi ya Sh. 9,000, lakini usafiri wa kukutoa Mbezi hadi unapoelekea ukaambiwa ni Sh. 20,000.
Kwa kweli gharama hizo ni kubwa na kwa watu ambao hawana uwezo wa kulipa inawabidi walale stendi ili kukikucha watafute daladala.
Fikiria abiria mwenye watoto na mizigo ni usumbufu gani anaoupata? Na wengine hata kupoteza baadhi ya mizigo yao.
Ingawa kumetolewa ufafanuzi wa kuwa kuna madereva wa bodaboda, bajaji na taxi wanaoegesha kwenye kituo hicho kwa kufanya biashara ya kutegemea abiria wanaoshuka kwenye mabasi hayo, lakini ukiangalia ni abiria wachache wanaobaki kwenye mabasi yanayokwenda kupaki kwenye ofisi zake, huku wengi wakiteremkia kituo hicho.
Ni kweli wafanyabiashara wanatafuta riziki zao kupitia abiria hao, lakini watu wasilazimishwe kufuata taratibu ambazo zinawagharimu na wengine kulazimika kutofanya safari hata za kusalimia ndugu zao mikoani kwa kukwepa gharama hizo.
Kwa mfano mtu ametoka mkoani na anashukia Kimara, inamlazimu kushukia Mbezi, wakati basi alilopanda kumtoa mkoani linapita kituo hicho hicho anachoshukia. Hii haijakaa sawa.
Tunashukuru Waziri wa TAMISEMI, Innocent Bashungwa kwa kuliona hilo na kumuagiza Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Amos Makalla kukutana na wadau na wamiliki wa mabasi ili kuweka utaratibu mzuri na shirikishi wa utoaji huduma kwa wananchi kwenye kituo hicho kikuu cha mabasi cha Magufuli.
Waziri amesema amekuwa akifuatilia kwa ukaribu malalamiko yanayotolewa na wananchi kuhusu huduma katika stendi hiyo.
Amemtaka Mkuu wa mkoa kushirikiana na Mamlaka ya Udhibiti Usafiri Ardhini (LATRA), pamoja na wadau wengine ili kukubaliana na kuweka utaratibu utakao rahisisha utoaji huduma bora bila kuleta adha kwa wananchi wala kuathiri malengo ya serikali kujenga stendi hiyo.
Ni matumaini yetu kuwa mazungumzo yatakwenda vizuri na kupata muafaka wa kumaliza adha hii.