Nyongeza ya siku 7 sensa ikalete chachu kuhesabiwa

31Aug 2022
Mhariri
Nipashe
Nyongeza ya siku 7 sensa ikalete chachu kuhesabiwa

SENSA ya Watu na Makazi ni mchakato wa kitaifa unaofanyika kila baada ya miaka 10 na ya mwisho kufanyika nchini ilikuwa mwaka 2012.

Sensa ya mwaka huu iliyoanza Agosti 23, ni ya sita kufanyika nchini baada ya Muungano wa Tanganyika na Zanzibar mwaka 1964. Sensa nyingine zilifanyika mwaka 1967, 1978, 1988, 2002 na 2012.

Juzi, Kamisaa wa Sensa Kitaifa, Anne Makinda, alitangaza kuongezwa siku saba katika mchakato wa kukamilisha Sensa ya Watu na Makazi na kueleza mchakato huo utakamilika Septemba 5.

Sababu kuu ya kuongezwa kwa siku hizo ni kuwafikia Watanzania wote na kufanyika kwa sensa ya majengo ambayo imeanza jana.

Pia, hadi kufikia juzi saa 2:00 asubuhi idadi ya Watanzania waliohesabiwa walifikia asilimia 93.45, huku waliosalia wakiwa ni asilimia 6.5.

Tunatoa pongezi kwa serikali kwa kuwezesha kuifikia idadi hiyo ya Watanzania ni imani yetu kwa siku hizo zilizoongezwa kila Mtanzania anakwenda kuhesabiwa.

Pia, tunapongeza hatua hiyo ya kuongeza muda wa kukamilisha mchakato huo kwa sababu idadi kubwa ya Watanzania ilikuwa na kilio cha kutofikiwa na makarani wa Sensa ya Watu na Makazi.

Tunaamini kwamba kuongezwa kwa siku hizo kutakamilisha mchakato huo muhimu kwa mustakabali wa taifa na maendeleo kwa wananchi wote.

Hivyo, kuongezwa kwa siku hizo kuwaamshe makarani ambao kwa namna moja ama nyingine walikuwa na kasi ndogo ya kuchukua takwimu za wananchi.

Sasa makarani wanapaswa kuchangamka, kuhakikisha wanapita mtaa kwa mtaa, nyumba kwa nyumba kuchukua takwimu muhimu zinazohitajika.

Katika siku hizo saba elimu zaidi itolewe kwa Watanzania ambao walikuwa wamegoma kuhesabiwa, busara na hekima zitumike kuwaelimisha umuhimu wa kupata takwimu za wananchi.

 

Ni imani yetu kwamba kuongezwa kwa siku hizo pia kutawaamsha baadhi ya Watanzania ambao wakati wa kuanza kwa mchakato huo Agosti 23, mwaka huu, walikuwa na majukumu mengine waliyokuwa wakiyafanya, kusababisha kutohesabiwa.

Kila Mtanzania ambaye hakupata fursa ya kuhesabiwa wakati mchakato huo umeanza ni wakati muafaka kwa sasa kwa wao kuhesabiwa kwa manufaa ya taifa.

Sote tunafahamu kwamba umuhimu wa Sensa ya Watu na Makazi ni pamoja na kuisadia serikali kupata taarifa za msingi zitakazosaidia mchakato wa utekelezaji wa Dira ya Maendeleo ya mwaka 2025, mageuzi ya masuala ya afya na jamii, pamoja na ufuatiliaji wa ajenda za maendeleo za kimataifa.

Faida nyingine ni taarifa za watu husaidia katika mamlaka za wilaya katika utekelezaji wa mipango ya maendeleo ambayo huakisi matakwa ya watu katika ngazi husika na kusaidia kwenye uwiano wa mgawanyo wa rasilimali.

Faida nyingine ni takwimu zitakazokusanywa zitaiwezesha serikali kujua ongezeko la idadi ya watu, kwa mgawanyo na viashiria vingine, ambavyo ni muhimu kwa usimamizi wa mazingira.

Mwisho, tunatoa rai kwa Watanzania wenye tabia ya kutoa taarifa za uongo kwa makarani kuacha mara moja kwani takwimu sahihi zinahitajika kwa ajili ya ugawaji wa majimbo ya uchaguzi kwa ufanisi, kurekebisha mipaka ya kiutawala katika serikali za mitaa.