Hili la viwanja 20/20 litolewe elimu

02Sep 2022
Mhariri
DAR ES SALAAM
Nipashe
Hili la viwanja 20/20 litolewe elimu

SERIKALI kupitia Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, imeeleza kutovitambua viwanja vyenye vipimo vya 20/20 na kutaka wote waliopimiwa warudishiwe fedha zao.

Sababu iliyotolewa ni kuwa ukubwa huo haukubaliki kwa sababu hakuna viwanja vyenye upana na urefu wa namna hiyo kisheria.

Pia imeagiza kampuni binafsi za upangaji, upimaji na mengine yanayojihusisha na masuala ya ardhi na kuuza vipande vya ardhi kwa ukumbwa huo, kusitisha.

Serikali imechukua hatua hiyo kwa mujibu wa Sheria ya Mipango Miji Na. 8 ya mwaka 2007, sura 355, kifungu Na. 77 (1) (b), (i), kanuni ya viwango vya upimaji maeneo, zilizotangazwa kwenye Gazeti la Serikali namba 91 na 93, inayoainisha ukubwa wa maeneo kwa matumizi mbalimbali.

Ufafanuzi ni kwamba viwanja hivyo vinatakiwa kuwa na mapana na marefu yenye uwiano wa moja kwa mbili mpaka moja na mbili na nusu.

 

Mfano uliotolewa ni kiwanja chenye ukubwa wa mita za mraba 400 kinapaswa kuwa katika uwiano wa upana wa mita 16 na urefu 25.

Kutokana na ufafanuzi huo Waziri mwenye dhamana ya ardhi ameagiza bodi zote za kitaalamu kuanzia ya Usajili Wataalamu wa Mipango Miji, Baraza la Wapima Ardhi Tanzania na Bodi ya Usajili ya Wathamini, kufanya uchunguzi wa kampuni zote zinazofanya kazi kinyume na sheria ili hatua kali zichukuliwe haraka.

Kwetu sisi tunasema jambo hili ni jema, lakini swali linakuja kwa wale ambao tayari wameshapimiwa viwanja hivyo kwa makosa na kuweka makazi yao ya kudumu, wanasaidiwa vipi.

Sheria ipo na watu wanaopaswa kuisimamia ili isivunjwe ndiyo wanaopitisha viwanja hivyo mpaka kufikia hatua ya mtu kupewa hati.

Wanaokwenda kupima viwanja hivyo ni watu wenye taaluma ya masuala ya ardhi na wanaelewa ukubwa unaotakiwa kwa viwanja hivyo, lakini wameendelea kuchukua fedha za watu wakijua ni kosa kisheria.

Waliopimiwa na kupata hati za viwanja hivyo pia wamekuwa kwenye orodha ya wanaolipia viwanja vyao kwa mujibu wa sheria inavyotaka na kujiona ni wamiliki halali.

Leo anapoambiwa kuwa viwanja hivyo havitambuliki ni kumweka kwenye njia panda.

Hata hivyo, serikali imewataka wananchi kuwa makini na watu wanaowauzia ardhi kwa aina hiyo kabla ya kununua kwa kupata taarifa au mwongozo kutoka ofisi ya ardhi ziliko halmashauri au ardhi mkoa ili kupata ushauri.

Tunavyofahamu wananchi wanaponunua ardhi ni lazima waanzie kwenye ngazi ya serikali ya mtaa kujiridhisha kuwa eneo analouziwa halina tatizo na kisha kwenda ardhi ambako hupata taratibu za kupimiwa mpaka kupata hati.

Kilichoishtua wizara ni kuibuka kwa uuzaji holela wa viwanja ambavyo havizingatii matakwa ya sheria ya mipango miji na baadhi ya kampuni na wakala wa ardhi kugawa na kuuza viwanja ambavyo havijapangwa wala kupimwa maarufu 20/20.

Wananchi wameshauriwa kupata viwanja ambavyo wanaweza kuzalisha shughuli za kiuchumi.

Wizara imesema imekuwa ikipokea maombi kutoka kwa wananchi wakitaka kupimiwa maeneo yao, ambayo wanadai wameshauziwa, lakini eneo halijapangwa wala kupimwa.

Ilibainisha kuwa kampuni zimekuwa zikinunua maeneo na kukata viwanja vidogo vidogo vyenye ukubwa wa mita za mraba 300 bila kuzingatia sheria na mahitaji ya huduma za jamii kisha kuwauzia wananchi.

Viwanja hivyo vinaelezwa kuwa havina huduma za jamii, barabara na wakati huo huo wameuza na kuleta migogoro.

Waziri ameibainisha kuwa kampuni hizo wameshazitambua na kinachoangaliwa ni namna ya kuzichukulia hatua.