Kiini 'jipu' mishahara hewa lazima kipatikane

10Apr 2016
Mhariri
Nipashe Jumapili
Kiini 'jipu' mishahara hewa lazima kipatikane

Kwa mujibu wa Waziri wa Utumishi, Angela Kairuki, watumishi hewa wameshaisababishia serikali ya Rais wa tano, John Magufuli hasara Sh. bilioni 7.6 kati ya Januari na Machi tu.

Na wakati kampeni ya kuwabaini watumishi hewa hao ndani ya serikali ikichukua sura mpya bada ya kuanza kwa uchunguzi wa kuwabaini wanufaika halisi na kuwachukulia hatua za kisheria, imebainika kuwa ufisadi huo unaweza kuwa umeshaligharimu taifa takribani Sh. bilioni 150 katika kipindi cha miaka mitano iliyopita.

Machi 15 kwaka huu, wakati akiwaapisha wakuu wapya wa mikoa, Rais Magufuli alitoa siku 15 kwa kila mmoja wao kuhakikisha kuwa anafichua watumishi hewa katika mkoa wake.

Agizo hili, ambalo ni la kwanza la aina yake katika uongozi wa kisiasa nchini, hasa ikizingatiwa kuwa wakuu wa mikoa ndiyo viongozi wakuu wa serikali katika maeneo yao, lina kila ishara kuwa Rais wa tano Magufuli amepania kuondoa kabisa mishahara hewa katika orodha ya mianya ya upotevu wa fedha za umma, Nipashe tunaona.

Lakini kwetu Nipashe, tunaona pia kwamba, kwa vile tatizo la mishahara hewa limekuwa likijitokeza kwa angalau awamu tatu zilizopita za uongozi wa juu wa serikali, dawa halisi ya kumaliza ufisadi huo si tu kuondoa watumishi hewa kwenye orodha bali kuondoa watumishi ambao huchomekea majina hewa kwenye orodha ya malipo.

Na habari za faraja, kwetu Nipashe, ni kwamba zipo fununu kuwa serikali imeanza uchunguzi kuwabaini watumishi wote waliokuwa wakijilipa mishahara hiyo ili hatimaye wachukuliwe hatua.

Na fununu hizi zinakuja muda mfupi baada ya Rais Magufuli, akiwa katika mapumziko ya 'mwisho' wa mwaka wilayani Chato, mkoani Geita, kusema kwamba amegundua mfanyakazi wa Mamlaka ya Mapato (TRA) ambaye alikuwa akijilipa mishahara 17 ya watumishi hewa.

Tunashukuru, Nipashe, kwamba tatizo la mishahara hewa 17 ya TRA, limepatiwa ufumbuzi wa kudumu baada ya Rais kuahidi pia kuwa mtumishi huyo atafikishwa mahakamani ili sheria ichukue mkondo wake.

Na mtindo huu wa kufikisha wanufaika halisi wa malipo hayo, tunaona Nipashe, ndiyo pekee ambao utamaliza kabisa tatizo la mishahara hewa kwa sababu unashughulika na mzizi wa ufisadi wenyewe na si wizi wa mishahara pekee kama ilivyokuwa chini ya awamu za marais wastaafu Ali Hassan Mwinyi, Benjamin Mkapa na aliyepita, Jakaya Kikwete.

Tunaisukuma basi, Nipashe, Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (Tamisemi), kuongeza kasi ya uchunguzi wake kuwabaini maofisa utumishi waliokuwa wakitafuna fedha hizo ili wakamatwe.

Na tunasukuma pia basi, Nipashe, Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (Tamisemi), George Simbachawene, kuhakikisha kuwa watumishi ambao watabainika kuhusika kujilipa mishahara ya watumishi hewa wanachukuliwa hatua kali ili iwe fundisho kwa wahasibu wengine wenye ndoto kama hizo.