Mechi hiyo itakayopigwa kwenye Uwanja wa Taifa, tayari imeshavuta hisia, hamu na matamanio kutoka kwa mashabiki.
Mabingwa hao watetezi wa Ligi Kuu ya Tanzania Bara ,Yanga inateremka uwanjani leo wakiwa katika nafasi ya pili kwenye msimamo wa ligi hiyo.
Tunaamini, safari ya Yanga kusaka kufuzu kucheza kwa hatua ya makundi ya michuano hiyo mikubwa, pekee na aina yake siyo rahisi.
Siyo rahisi kwa sababu, timu zote zinazocheza michuano hiyo hujiandaa vizuri siyo tu kwa kusaka kuingia hatua ya makundi, bali kutwaa taji kabisa.
Ingawa timu za Tanzania hazina rekodi nzuri ya kujivunia zinapocheza na timu za uarabuni hasa zile kutoka Misri, lakini bado tuna imani Yanga wanaweza kuweka rekodi.
Safari hii Yanga imeonekana kuwa tofauti na maandalizi ya mechi zake mbili za kimataifa zilizopita dhidi ya Cercle de Joachim ya Mauritius na APR ya Rwanda kwa kuongeza programu za mazoezi kwa ajili ya kuhakikisha wanapata matokeo mazuri hapa nyumbani kabla ya mechi ya marudiano mjini Alexandria, Misri.
Kuna msemo unasema; ‘huwezi kumnenepesha mbuzi siku ya mnada’, lakini sisi kama wanamichezo tuna dhamana ya kuwakumbusha Yanga mambo muhimu katika siku yao ya mwisho kabla ya kuwakabili Wamisri.
Hatuna lengo la kuwatisha wawakilishi wetu, lakini lazima kuwapa tahadhari kuwa wanacheza na moja ya timu bora za soka Afrika.
Al Alhy ndiyo timu yenye mafanikio makubwa katika michuano hiyo na ndiyo mabingwa wa kihistoria kutokana na kutwaa taji mara nyingi.
Lakini pia, timu nyingi kutoka Uarabuni zina mbinu nyingi ndani na nje ya uwanja, hivyo wawakilishi wetu Yanga lazima wajipange vizuri. Wachezaji wa Yanga waingie uwanjani wakiwa na kiu ya ushindi mkubwa nyumbani ili iwe rahisi kwenye mechi ya marudiano.
Wajione wamebeba dhamana ya kuwafuta machozi mashabiki kwa kuwafunga Waarabu hao wenye rekodi nzuri dhidi ya timu za Tanzania.
Kwetu, tunaamini kuwa timu iliyoandaliwa vizuri na wachezaji kupewa mahitaji yote ya kimsingi, ndiyo inayokuwa jirani na mafanikio kuliko kinyume chake.
Kauli ya Kocha wa Yanga, Hans van der Pluijim kwamba wachezaji wake wameiva kwa ajili ya mchezo huo, yanatupa imani kuwa leo Yanga wataibuka na ushindi mnene. Ushindi wa Yanga dhidi ya Al Ahly pia utategemea kwa kiasi kikubwa na ujio a mashabiki uwanjani.
Timu inayocheza mechi kwenye uwanja wa nyumbani mbele ya mashabiki wengi, huwa na nafasi ya kufanya vizuri zaidi kuliko ugenini. Hivyo basi, mashabiki wa soka wanapaswa kujitokeza kwa wingi uwanjani kuishangilia timu yao itakapokuwa ikipeperusha bendera ya nchi.
Kama alivyosema msemaji wa timu hiyo, Jerry Muro ya kuwataka mashabiki kuweka pembeni tofauti zao za ushabiki kwenye ligi ya nyumbani na kuelekeza nguvu kushangilia Yanga, ndivyo tunavyowashauri mashabiki kufanya hivyo leo.
Haitakuwa na maana timu ya nyumbani iliyobeba bendera ya nchi ikicheza kwenye uwanja wa nyumbani, halafu inatokea kuna baadhi ya mashabiki wanaishangilia timu ngeni.
Ni nafasi yetu kuonyesha uzalengo kwenye mechi hiyo ili Yanga icheze kwa kujiamini na kupata ushindi.










