Mchezaji hata kama ana kipaji cha pekee na aina yake, bado atahitaji kuwa na nidhamu. Nidhamu ndiyo inayolinda kipaji chake.
Tumeshuhudia nchi zilizoendelea kisoka zikisisitiza suala la nidhamu ya mchezaji. Mchezaji yeyote wa kulipwa, kama kuna kitu angependa kuwa nacho ni nidhamu ndani ya nje ya uwanja.
Lakini kwa soka letu ambalo kila kukicha tumekuwa tukilalamika kurudia nyuma, suala la nidhamu ni tatizo kubwa.
Wachezaji wetu wameshindwa kubeba dhamana ya kulinda vipaji vyao, nidhamu yao haiendani na kile ambacho wanastahili kufanya.
Kinachoendelea ndani ya klabu ya Simba kwa sasa kuangaika na nidhamu ya wachezaji, ni mfano wa matatizo yanayolikumba soka letu.
Kwa wiki kadhaa sasa, klabu hiyo kubwa nchini imekuwa ikilia na nidhamu mbaya za baadhi ya wachezaji wake.
Pamoja na onyo na adhabu kutolewa, lakini inaonekana kama ndiyo kwanza tatizo linazidi kuongezeka.
Unapokuwa na wachezaji wanaoweza kumjibu kocha wao jinsi wanavyotaka, unapaswa kujiuliza kama kweli kuna sababu ya kuendelea kuwa na aina hiyo ya wachezaji.
Katika zama hizi, inashangaza kumuona mchezaji akitunishiana misuli na kocha wake kwa mambo ambayo hayana msingi.
Ingawa suala la Hassan Isihaka limezungumzwa sana, lakini bado ndani ya klabu ya Simba kuna utamaduni wa baadhi ya wachezaji kujiona wao ndiyo kila kitu.
Wachezaji wa aina hii wanajidanganya kutokana na ukubwa wa majina yao na kujiona ndiyo kila kitu kwenye klabu.
Klabu kubwa kama Simba inahitaji kuwa alama ya nidhamu, lakini inasikitisha pale inapokuwa taswira ya kutunza wachezaji wenye nidhamu.
Siyo dhamira yetu kukosoa nidhamu ya wachezaji wa Simba, lakini tunadhani ni jukumu letu kuhakikisha soka letu linasonga mbele.
Haya yanayotokea klabu ya Simba, tusingependa kuona yanakuwa mfano mbaya kwa wachezaji wa timu nyingine.
Tumeona wachezaji wakubwa duniani wanaocheza klabu maarufu, japo kuzitaja chache; Manchester United, Real Madrid, Barcelona, Juventus, Bayern Munich.
Wachezaji wa timu hizi pamoja na ukubwa wa majina yao, bado hawajioni kuwa juu ya makocha wao au klabu zao.
Wameendelea kuheshimu nidhamu ndani na nje ya uwanja na ni kwa sababu wanajua, wao ni kioo cha jamii.
Haina maana kwamba wachezaji hawapaswi kuhoji wanapoona mambo yanakwenda vibaya, lakini heshima ndiyo jambo muhimu.
Kama kweli wachezaji wetu wana ndoto ya kufika mbali katika soka, basi hawana budi kuanzia sasa kuhakikisha wanaishi katika misingi na miongozo ya nidhamu.
Nidhamu haifundishwi, bali hutokana na utashi na uamuzi wa mtu kuamua namna atakavyo mbele ya jamii inayomzunguka. Tungependa kuona wachezaji wetu wakiwa na ndoto zinazotimia kwenda kucheza soka Ulaya na kwingineko, lakini tu kwa kuweka nidhamu mbele.










