Aidha, Tanzania imeridhia mkataba wa Umoja wa Mataifa wa Haki za Mtoto na Mikataba ya Shirika la Kazi (ILO) kuhusu ulinzi na hifadhi za watoto wenye umri wa chini wa kuajiriwa kwa ajira zinazoruhusiwa na mbaya zinazokatazwa.
Tunatoa angalizo hili, tukirejea maagizo ya Polisi Mkoa wa Mbeya kuwasaka na kuwafikisha mbele ya sheria wazazi na walezi watakaowatumia watoto wao kinyume cha sheria kwenye maonyesho ya Nanenane mkoani humo.
Ni taarifa iliyochapishwa na gazeti hili jana.Tunaungana na polisi kwenye hilo, licha ya kuwapo sheria hizo, watoto wanakabiliwa na aina mbaya zaidi za ajira ikiwamo kutumikishwa nyumbani (house girls na boys) kwenye kila aina ya unyanyasaji na ukatili mkubwa.
Tunasikia kilio cha wanaotumikishwa kingono na hata kuuzwa ughaibuni, wakati mwingine hutokana na biashara haramu ya binadamu wanakwenda kufanyakazi kwenye madanguro.
Watoto pia wanatumiwa kwenye ajira katika kilimo, wanalima mashambani kwa ujira kiduchu au bila malipo, aidha hufanya shughuli za kumwagilia mazao kwa kushika sumu na vihatarishi kwa ajili ya kuua wadudu na zote ni shughuli ngumu zinazotishia ustawi wao.
Watoto wanafanyishwa kazi za kulazimishwa na hutumia vihatarishi haswa katika shughuli za migodini kutumia kemikali mfano zebaki kuchenjulia dhahabu.Aidha, katika zama hizi watoto wengi hudhulumiwa kingono kutokana na biashara haramu ya binadamu inayofanyika ndani na nje ya nchi, hivyo husababisha wavulana na wasichana kuathirika kisaikolojia kwa kutumikishwa katika biashara za kingono hususan maeneo yenye mzunguko mkubwa wa biashara.
Watoto si kwamba wananyanyaswa nje ya familia zao pekee, hata ndani ya nyumba kuna baadhi ya wazazi na walezi wanawatumia kuuza bidhaa mbalimbali ili kuleta kipato kwa familia.
Mara nyingi wazazi wanaambiwa kuwa kuwatumikisha watoto maeneo kama hayo husababisha kunajisiwa na kufanyiwa unyanyasaji wa kingono.
Jeshi la Polisi mkoani Mbeya limekumbusha wajibu wa wazazi katika malezi ya watoto kutowahusisha kwenye uuzaji wa bidhaa katika maonyesho ya Nanenane, hivyo nasi si budi kuukumbusha umma kuwa ni vibaya watoto kutumiwa kwenye sherehe au maonyesho na shughuli zote zinazozidi umri wao.
Tunakumbusha kuwa si vyema kuwatumia katika shughuli mbalimbali za kijamii kwenye matangazo ya biashara kuanzia runinga, mabango mitaani na hata tamthilia. Tunaona kuwa wanaofanya hivyo wananufaika zaidi kuliko watoto kwa vile ni wadogo na hawaelewi kitu wala hawawezi kuingia mikataba.
Tunaona kuwa kwenye muziki watoto wanatumiwa kucheza wakigeuzwa kuwa wahusika kwenye nyimbo au tungo, lakini pia tunawaona wakitumiwa kutoa buruduni kwenye sherehe ambazo hualikwa kuimba au kucheza na kutunzwa fedha kwa kisingizio kuwa ni wahitaji wanahitaji msaada.
Hata hivyo haifahamiki iwapo fedha hizo wanazochangiwa watazipata zote au watagawana na aliyewaleta au mshereheshaji (MC).
Tunasisitiza kuwa ni muhimu na lazima kuwalinda watoto kama katiba, sheria na ILO zinavyoelekeza.Kwa kuwa hawa ndiyo Watanzania wa kesho, hivyo tuwajibike maana taifa lisilolinda watoto wake ni sawa na taifa lililojimaliza na lisilojijali.