Wazazi msimuache nyuma Mtoto wa kike masomo sayansi

03Aug 2022
Mhariri
DAR ES SALAAM
Nipashe
Wazazi msimuache nyuma Mtoto wa kike masomo sayansi

IPO dhana kwenye jamii kuwa mtoto wa kike au mwanamke sio wa kusoma au kufanyakazi ngumu badala yake zinapaswa kufanywa na mtoto wa kiume jambo linalorudisha nyuma au kuua ndoto zao.

Kwa muda mrefu Tanzania imeweka mikakati ya kuongeza na kushawishi watoto kupenda masomo ya sayansi ikiwamo kutoa zawadi, ufadhili wa masomo na mikopo ya elimu ya juu kwa asilimia 100.

Kuwavunja moyo watoto wa kike kuchukua masomo hayo kumesababisha fani za taaluma hiyo kuchukuliwa na watoto wa kiume.

Ukiangalia marubani wengi wa ndege, marubani wa meli, wahandisi na fani zenye taaluma ya masomo ya sayansi wanawake ni wachache sana ikilinganishwa na wanaume.

Hata inapotokea mtoto wa kike kuwa rubani wa meli au chombo ambacho kimezoeleka kuendeshwa na mwanaume inaonekana kuwa jambo lisilo la kawaida.

Unapotembelea vyuo vikuu utabaini kukosekana kwa wanawake wengi wanaosoma masomo ya sayansi, hali ambayo ilisukuma serikali na wadau kuweka nguvu ili kuwapa motisha.

Pia, wanawake wanaohitimu vyuo vikuu katika fani za sayansi wameajiriwa kwa haraka, lengo ni kutoa motisha zaidi na tayari tunaona mafanikio ya ongezeko la madaktari kwenye jamii.

Hivi karibuni Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia ilitangaza kuanza kutoa ufadhili kwa wanafunzi waliofaulu masomo ya sayansi ikiwa wataendelea na masomo hayo ngazi ya chuo kikuu, ambao watasoma bure kwa vyuo vya ndani na unaangaliwa uwezekano wa kuwapeleka nje ya nchi.

Wakati jitihada hizo za wadau zikiendelea bado kwenye jamii yetu kuna mtazamo hasi dhidi ya watoto wa kike kusoma masomo ya sayansi, hali hiyo huanzia ndani ya familia kwa kuwaaminisha ni magumu.

Lakini mazingira ya shule nayo huwakatisha tamaa kwa kuwa hakuna vifaa vya maabara vya kujifunzia kwa vitendo hali inayoongeza ugumu kwao kwa kuwa masomo hayo hueleweka kwa vitendo zaidi.

Julai 31, mwaka huu wadau wa elimu na sayansi nchini walipoadhimisha Siku ya Mwanamke wa Kiafrika pamoja na mambo mengine walisema kuwa malezi yanachangia pia kurudisha nyuma ndoto kusoma sayansi.

Tunatoa angalizo kwa wazazi kuacha kulea watoto wao wa kike kizamani bali waendane na kasi ya sayansi na teknolojia ambayo inahitaji wataalam zaidi katika sekta ya sayansi bila kubagua jinsia kwa sababu wanaume peke yao hawatoshi.

Tunawasihi wazazi na walezi wawape watoto wao wa kike muda wa kutosha wa kuendeleza vipaji vyao vya kisayansi badala ya kuwabana wafanye kazi ndogo za nyumbani kama vile kuosha vyombo, kufagia na kudeki wakiamini kuwa huo ndiyo msingi pekee wa maisha.

Pia, tunawakumbusha kuchunguza vipaji vya watoto wao wa kike katika sayansi kupitia shughuli mbalimbali kama vile kuchora, kupaka rangi, kutengeneza vitu mbalimbali katika michezo yao na kuviendeleza.

Watoto wanaathiriwa zaidi na maneno yanayotoka kwa watu wao wa karibu, hasa wazazi na walezi kwa kuwa wanawaamini zaidi, kwasababu hiyo wazazi watumie mwanya huo kuwajenga na kuwatia moyo watoto wa kike katika masomo hayo.

Aidha, tunawasihi wadau wa sayansi nchini kuendelea kufanya uchunguzi na kuibua sababu mbalimbali zinazosababisha mwanamke kuachwa nyuma katika sayansi ili zipatiwe ufumbuzi.

Tunawakumbusha pia kuendelea kutoa elimu kwa jamii kuhusu umuhimu wa kuwa na usawa wa kijinsia katika sayansi ili wanawake wasiachwe nyuma.