Bila utawala bora, hakuna klabu bora

01Aug 2022
Mhariri
DAR ES SALAAM
Nipashe
Bila utawala bora, hakuna klabu bora

DHANA ya utawala bora inahubiriwa dunia nzima. Nia ya injili hii ya utawala bora ni kuhakikisha kila kitu kinakwenda kwa mujibu wa taratibu. Na taratibu zikifuatwa maana yake ni kuwa kila kitu kitafanywa kwa uwazi.

Mpira wa miguu ni sehemu ya dunia hii tunayoishi. Ni mchezo ambao unahusisha wadau wengi, kutokana na ukweli kuwa mpira wa miguu ndiyo unaoongoza kwa kuwa na washabiki wengi kuliko mchezo mwingine wowote.

Klabu za mpira wa miguu kama ilivyo vyama vya mpira wa miguu ni taasisi ambazo zinaongozwa kwa mujibu wa katiba ambazo zimeziunda ikiwamo kanuni za uendeshaji zinazotokana na katiba hizo na miongozo ya vyama vya mpira wa miguu vilivyo juu yao.

Ni katika utaratibu huo ndiyo maana umekuwapo mgawanyo wa majukumu. Klabu zina viongozi wa kuchaguliwa kwa mujibu wa katiba zilizoasisi taasisi hizo. Viongozi ndiyo wanaowajibika kwa mkutano mkuu wa wanachama.

Kwa mamlaka hayo ambayo uongozi umepewa na mkutano mkuu, una majukumu mbalimbali ya kutekeleza. Baadhi ya makujumu hayo ni kuajiri sekretarieti pamoja na mabenchi ya ufundi. Kocha mkuu kwa kawaida ndiye kiongozi wa Benchi la Ufundi.

Kwa mantiki hiyo sekretarieti inatarajiwa kuundwa na wataalamu kulingana na nafasi za kazi walizoomba kwa kuzingatia sifa zao.

Utaratibu huo huo ndiyo unaotumika vilevile kwa kuajiri Benchi la Ufundi kwa kuzingatia matakwa ya kocha ambaye ndiye anayeongoza benchi hilo likihusisha wataalamu wa nyanja nyingine za mpira wa miguu.

Hali ni mbaya, kwani sasa imekuwa kawaida kwa mwenyekiti au makamu mwenyekiti kufanya kazi za ofisa habari. Au mjumbe au mwanachama kufanya kazi za kocha (kusajili wachezaji).

 Imefika mahali huwezi kujua nani ni katibu mkuu (mtendaji) katika klabu, na nani ni mwenyekiti au makamu mwenyekiti katika klabu au chama cha mpira wa miguu katika ngazi tofauti.

Nini kifanyike kama sekretarieti ina upungufu, udhaifu au ni mbovu? Kama ilivyo kwa mwajiri yeyote, kama mfanyakazi anashindwa kutekeleza majukumu yake kulingana na maelekezo aliyopewa anachukuliwa hatua za kinidhamu.

Katika utaratibu huo huo wa utawala bora, shughuli za mpira wa miguu hazitakiwi kuingiliwa na mamlaka nyingine nje ya uzio huo. Mfano, Shirikisho la Kimataifa la Mpira wa Miguu (FIFA) halitaki serikali kuingilia vyama vya mpira wa miguu.

Ingawa dhana hii imekuwa ikipotoshwa na baadhi ya viongozi dhaifu, ukweli ni kuwa FIFA inaamini katika utawala bora. Ni katika dhana ya utawala bora kila mwenye wajibu wake atatekeleza, kila mwenye haki yake ataipata.

Lakini hiyo itawezekana tu iwapo waliopewa majukumu/dhamana kulingana na katiba na miongozo mingine watatekeleza.

Kwa upande wa uchaguzi hiki ndicho kipindi chake ambapo kwa dhana ya utawala bora zimeundwa Kamati za Uchaguzi. Kamati hizi zinafanya kazi kwa mujibu wa Katiba ambazo ndizo msingi wa kuundwa kwao pamoja na kanuni za uchaguzi.

Katiba inaeleza sifa za uongozi (kwa maana ya watu wanaostahili kugombea, ingawa haki ya kuchagua inabaki kwa mpigakura). Kanuni kwa upande wake zinaelezea taratibu za uchaguzi (mchakato mzima) hadi viongozi wanapochaguliwa.

Au timu inashiriki katika mashindano X. Lakini kabla hujaingia katika mashindano ni lazima usome na ujue kanuni za mashindano husika, vinginevyo utakuwa msumbufu na kusababisha usumbufu kwa wadau wengine bila sababu za msingi.

Hayo yote ni matatizo ya kutozingatia utawala bora. Ni vizuri kuzingatia kanuni vinginevyo mtu anaweza kuonekana kituko mbele ya jamii/umma bila sababu za msingi. Huwezi kuwa na klabu bora huzingatii utawala bora.