Fursa ya kurasimisha makazi ichangamkiwe

13Aug 2021
Mhariri
Dar es Salaam
Nipashe
Fursa ya kurasimisha makazi ichangamkiwe

MOJA ya mambo ambayo serikali inakazania na kuyawekea msukumo, ni kuhimiza wananchi kurasimishaji mkazi yao, kwa kuwa hatua hiyo itawanufaisha wanapokuwa wanamiliki ardhi ambayo imepimwa.

Kwa kawaida, ardhi iwe kiwanja au nyumba thamani yake hupanda pale inapokuwa imepimwa na maana ya kupima ardhi ni kuirasimisha, hivyo faida nyingi hupatikana baada ya ardhi kurasimishwa.

Baadhi ya faida ambazo mtu anaweza kuzipata baada ya urasimishaji, ni ardhi hupanda thamani yake, kuwa na sifa ya kukopesheka katika benki na taasisi za fedha kwa urahisi. Ardhi kutumika kama dhamana mahakamani, lakini kubwa ni mmiliki kuwa na uhakika kuwa anaimiliki kihalali na kisheria.

Kadhalika, urasimishaji ni kazi shirikishi inayowezesha wananchi kukubaliana mipaka ya viwanja, kufungua njia na kutoa maeneo ya huduma za jamii kama shule, barabara vituo vidogo vya polisi, makaburi, zahanati na maeneo ya wazi.

Kutokana na umuhimu huo, Benki ya NMB imezindua huduma mpya ya mkopo wenye riba nafuu wa kuwasaidia wananchi wa kipato cha chini kutekeleza takwa la kisheria la kurasimisha makazi yao.

Huduma hiyo iliypewa jina la ‘NMB Plot Loan’ inaendeshwa kwenye Programu ya Kitaifa ya Urasimishaji wa Makazi ikitekelezwa kwa ushirikiano kati ya benki hiyo na Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi.

Benki hiyo itawasaidia wananchi kulipia gharama zote za urasimishaji wa makazi kuanzia upimaji wa viwanja mpaka uandaaji wa hatimiliki, na kwamba mwananchi atalipa kidogo kidogo ndani ya miaka miwili.

Aidha, riba ya mkopo huo inatajwa kuwa ni asilimia 10, na kwamba mwananchi atapatiwa hatimiliki baada ya kukamilisha urejeshaji wa mkopo wake katika benki hiyo.

Sisi tunaona kuwa hiyo ni fursa nzuri kwa kuwa inawawezesha wananchi wa kipato cha chini kumiliki makazi ambayo yanatambulika kisheria, hivyo tunawashauri kuichangamkia, kwa ajili ya faida yao, kwa kuzingatia kuwa kwa sasa ardhi ni mali hasa inapokuwa imepimwa.

Mtu anaweza kutumia adhi yake kukopa fedha benki na kufanyia shughuli za maendeleo au akiamua kuuza kwa bei nzuri, hivyo tunaamini kuwa suala la kurasimisha ardhi lina umuhimu mkubwa na wa kipekee ambao kila mwananchi hanabudi kuuchangamkia.

Ni jambo lililo dhahiri kwamba Watanzania wengi wanaoshindwa kurasimisha makazi yao kwa kukosa fedha za kulipia gharama za urasmishaji, lakini tunaona kuwa kupitia uwezeshaji wa mkopo NMB, utawaondolea hali ya unyonge na kuwapa unafuu wenye nia ya kurasimisha makazi yao.

Tunaipongeza Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi kwa kuendeleza ubunifu katika utekelezaji wa majukumu yake ya kusimamia sekta ya ardhi, hatua yake ya kushirikiana na NMB itekeleza mpango huo inathibitisha umakini na weledi wa viongozi wakuu wa wizara hiyo.

Changamoto iliyobaki sasa ni ya utoaji wa elimu na uhamasishaji wa wananchi kuielewa programu hiyo kisha kuanza taratibu za kukopa fedha kwa ajili ya urasimishaji wa makazi yao.

Tunadhani kwamba mpango huo ni mzuri na unapaswa kuwa endelevu ili kila wakazi wananchi wawe wakirasimisha makazi yao kwa lengo la kunufaika kama tulivyoeleza awali. Kupitia mpango huu, maeneo mengi ya Tanzania yatarasimishwa tofauti na sasa ambapo maeneo mengi hayajarasimishwa na kutambuliwa kisheria.

Hata hivyo, jambo la msingi ambalo wahitaji wa mkopo huo watatakiwa kulizingatia ni kuelewa kwamba fedha watakazopewa sio zawadi, bali ni mkopo kutoka kwa walipakodi wa nchi hii, hivyo watawajibika kuzirejesha baada ya urasimishaji wa makazi yao.