Usajili wachezaji wapya uende sawa na mazoezi

14Aug 2021
Mhariri
Dar es Salaam
Nipashe
Usajili wachezaji wapya uende sawa na mazoezi

TIMU mbalimbali zinazotarajiwa kushiriki Ligi Kuu Tanzania Bara msimu wa 2021/22 zinaendelea na mchakato wa kusajili wachezaji wapya kwa ajili ya kuboresha na kuimarisha vikosi vyao.

Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), lilitangaza dirisha la usajili litafungwa rasmi Agosti 31, mwaka huu, lakini timu zinazoshiriki mashindano ya kimataifa yanayoandaliwa na Shirikisho la Mchezo huo Afrika (CAF), zenyewe zinatakiwa kukamilisha mchakato huo hapo kesho Jumapili.

Huku tayari TFF imeshatangaza msimu mpya utaanza ifikapo Septemba 29, mwaka huu, lakini ukifunguliwa na mchezo wa Ngao ya Jamii utakaochezwa Septemba 25, mwaka huu kwenye Uwanja wa Benjamin Mkapa jijini Dar es Salaam kwa kuwakutanisha watani wa jadi, Simba na Yanga.

Kwa sasa kila timu imekuwa ikiendelea na mchakato wa kusajili wachezaji wapya ambao inaamini watasaidia kuongeza nguvu katika timu zao kwa kuzingantia mapendekezo kutoka kwa makocha wao, lakini ikiwaacha nyota ambao inaamini hawapo kwenye mipango yao.

Tunazikumbusha timu zote kuendelea kusajili kwa kuzingatia mahitaji halisi na kuacha kufuata 'mkumbo' kwa kuangalia wapinzani wao wanachofanya, kwa sababu kwa kufanya hivyo hawatafikia malengo yao na huko mbele wakajiweka kwenye hatari ya kushuka daraja.

Nipashe inazikumbusha timu zote mbali na kusajili, wanatakiwa pia kuwapa wachezaji hao maandalizi sahihi kulingana na ushindani wa ligi na mashindano yote watakayoshiriki.

Baadhi ya timu ambazo hupata matokeo mabaya katika mechi zao za ufunguzi, zimekuwa ya kulalamika kukosa maandalizi bora ikiwamo kucheza mechi za kirafiki na hivyo kuanza msimu mpya wakati wachezaji wao hawajafahamiana vyema au wamekosa kile wanachoita muunganiko.

Wamiliki wa timu wanatakiwa wakumbuke pia kuboresha mabenchi yao ya ufundi na kuacha tabia ya kuajiri kocha mwenye sifa, lakini anayezungukwa na wasaidizi ambao hawana elimu iliyojitosheleza na matokeo yake hushindwa kutoa msaada pale Kocha Mkuu anapoelemewa.

Huu ndio wakati wa makocha kuhakikisha programu zao zinatekelezwa vyema na kuondoa malalamiko baada ya kipenga kuanza kwa sababu kila timu inakuwa imepata muda sahihi wa kujiandaa.

Sio lazima kila timu inayoshiriki Ligi Kuu Tanzania Bara iweke kambi nje ya nchi, timu zinaweza kujipanga kwa kuandaa kambi yake hapa hapa nyumbani, lakini kwa kuhakikisha programu zote zinatekelezwa na hatimaye kufikia malengo waliyojiwekea katika msimu mpya unaokuja.

Kujiandaa vyema ndio kutaifanya timu iweze kupata matokeo chanya katika mechi zake, lakini ikivuna pointi nyingi kwenye mzunguko wa kwanza ambao hutoa taswira ya timu zitakazokuwa kwenye mbio za ubingwa na zile zitakazobakia kupambana kujinasua kutoshuka daraja.

Huu ni wakati mwingine kwa wachezaji kujitambua kwa sababu atakayefanikiwa kuonyesha kiwango kizuri, atajiweka kwenye nafasi nzuri ya kupangwa katika kikosi cha kwanza cha timu yake, lakini pia kuendelea kukitangaza kipaji chake kwa klabu nyingine za ndani na nje ya Tanzania.

Mchezaji atakayejituma na anayetumia vizuri kipindi hiki cha maandalizi ya msimu, atakuwa amejiimarisha na hapo atajitengenezea njia ya kuitwa katika kikosi cha Timu ya Taifa (Taifa Stars), ambacho kocha wake mkuu, Kim Poulsen huifuatilia hiyo kwa karibu ligi hiyo ya juu nchini.

Bingwa wa ligi au mafanikio katika soka hupatikana kwa timu iliyojiandaa vyema na si jambo lingine lolote la nje ya uwanja.