Viongozi vyama vya siasa wahamasishe chanjo corona

12Aug 2021
Mhariri
Dar es Salaam
Nipashe
Viongozi vyama vya siasa wahamasishe chanjo corona

IMERIPOTIWA kuwa 126 wamepatiwa chanjo corona wilayani Njombe Mkoa wa Njombe kuanzia Agosti 5, mwaka huu, tangu uzinduzi wa chanjo ufanywe na Rais Samia Suluhu Hassan, mwishoni mwa mwezi uliopita.

Idadi hiyo ya watu waliochanjwa, ni kwa mujibu wa Mganga Mkuu wa Halmashauri ya Wilaya ya Ludewa, Dk. Stanley Mlay na kwamba ili kuongeza kasi ya uchanjaji, halmashauri hiyo imeamua kuongeza vituo vyingine vinne kutoka vitatu vilivyokuwapo awali.

Anasema mwitikio ni wa wastani, tangu waanze kutoa chanjo, na kutoa wito kwa walengwa wa chanjo hiyo kujitokeza kwa wingi ili kuchanjwa kwa kuwa ni salama.

Kwamba huduma hiyo ni salama, kwa sababu serikali ipo inazisimamia, na kushauri watu kujitokeza kwa wingi ingawa suala la chanjo ni hiari, lakini ni muhimu kwa ajili ya kupunguza matatizo ambayo yanaweza yakatokea.

Wakati huduma ya chanjo ikiendelea kutolewa katika maeneo mbalimbali nchini, tunadhani kwamba kuna haja kwa wadau wote kushiriki kwenye kazi ya kuhamasisha wananchi kujitokeza kwa wingi kuliko ilivyo sasa.

Tunataja wadau kwa maana ya viongozi wa vyama vya siasa, kwamba wao pia wanaweza kushiriki katika uhamasishaji ili Watanzania wengi zaidi waendelee kujitokeza kuliko ilivyo sasa.

Mfano mzuri ni hiyo idadi ya watu wa wilaya ya Njombe, ambayo kimsingi ni ndogo hasa ikizingatiwa kwamba wilaya inaundwa na vijiji vingi, hivyo kujitokeza watu 126 tunadhani ni idadi ndogo.

Sisi tunashauri wanasiasa kama wadau washiriki katika uhamasishaji, kwa sababu, kwanza wana majukwaa ya kukutana na wanachama wao ikiwamo vikao vya ndani na hata mikutano mingine, ambayo wanaweza kuitumia pia kwa kazi hiyo.

Viongozi wa vyama vya siasa, ni miongoni mwa Watanzania ambao wamepata chanjo na wakakiri kuwa haina matatizo, hivyo kwa kauli zao hizo, tunadhani ni vyema wakazitumia pia kushawishi wanachama wakachanjwe.

Kwa kutumia ushawishi wao wa kisiasa, tunaamini idadi ya watu kujitokeza kuchanjwa inaweza kuongezeka, ingawa kuchanjwa ni hiari, lakini wakati mwingine watu hawajitokezi kutokana na ukosefu wa elimu sahihi kuhusu chanjo.

Pamoja na kwamba viongozi hao wanaweza kuwa na majukumu mengi, lakini tunaona kuwa si vibaya ndani ya majukumu hayo wakaongeza lingine la kuwaelekeza wanachama na umma kwa ujumla kupata chanjo ili nao wawe salama.

Kwa kuwa wao wameshachanjwa, tunaona kwamba, wana nafasi nzuri ya kuwahakikishia usalama wa chanjo hiyo wanachama wao ambao bado wanasita kuchanjwa kutokana na sababu mbalimbali.

Tunadhani kwamba kusuasua kwa wananchi kujitokeza kuchanjwa katika maeneo kadhaa ya nchi yetu, kunaweza kuchangiwa na mambo mawili, uhiari na kutokana na elimu waliopewa awali.

Hivyo, sisi kwa mtazamo wetu ni kwamba, wadau hasa viongozi wa vyama vya siasa kwa kutumia majukwaa yao, wana nafasi nzuri ya kuwaeleza wale ambao wanasita kujitokeza kwa sababu ya elimu ya awali waliopata kuhusu chanjo pengine kutowafikia wengi.

Tumetoa msisitizo kwa wanasiasa tikiamini kwamba nyuma yao kuna watu wengi ambao ni wafuasi wao, ambao ni rahisi kuwasikiliza na kuwaamini.

Kwa upande mwingine, kuna viongozi wa dini ambao nao wana wafuasi wengi nyuma yao. Hata hivyo, jambo la kufurahisha wamekuwa mstari wa mbele wa kuwahamasisha na kuwashawishi waumini wa dini zao kupata chanjo hiyo tangu siku iliyozinduliwa na Rais Samia.