Mkurugenzi wa Taasisi ya Elimu ya Watu Wazima (TEWW), Dk. Michael Ng’umbi, alisema wasichana watanufaika na masomo hayo kupitia Mpango wa Elimu Sekondari kwa njia mbadala chini ya mradi wa kuimarisha ubora wa elimu ya sekondari (SEQUIP- AEP).
Tayari serikali inatoa mafunzo kwa wadau wenye jukumu la kusimamia mradi huo katika uboreshaji wa miundombinu ya madarasa, kujifunzia na kufundishia kwenye mikoa 26 Tanzania Bara.
Alisema wasichana hao ni kati ya 12,000 watakaonufaika na mradi huo wa miaka mitano 2021-2026 wenye lengo la kuimarisha elimu ya sekondari nchini na TEWW imepewa jukumu hilo.
Hadi sasa tunaelezwa wasichana 1,500 kati ya 3,000 wamejiandikisha, ikiwa ni ufadhili wa Dola za Marekani milioni 500, na tunatarajia kuona thamani ya fedha ili hata zikiisha mradi uwe endelevu.
Hii ni habari njema kwa kuwa wasichana hawa ambao ndoto zao zilikaribia kuzimika kutokana na ujauzito au sababu nyingine zilizowafanya wasihudhurie darasani kwa mujibu wa sheria, na sasa kwa mpango huo tunadhihirisha kuwa elimu sio ya mfumo rasmi pekee bali hata njia mbadala inawezesha waliovuka umri wa kwenda shule kupata elimu.
Hii inakuja wakati ambako wasichana wengine waliopata mimba wanaruhusiwa kuendelea na masomo katika mfumo rasmi ndani ya miaka miwili tangu kuacha shule, maana yake fursa ya elimu kwa kundi hili ni kubwa kazi kwao sasa kuitumia.
Kupitia mpango huu sasa wataendelea na masomo na tutakuwa na madaktari, mawaziri, wakurugenzi, wakuu wa taasisi mbalimbali, walimu na kada nyinginezo zenye kuhitaji wataalamu.
Tunaipongeza serikali kwa kukamilisha mpango huu hasa kuhakikisha miundombinu muhimu ipo, walimu pamoja na vitabu vya kiada na ziada vitakavyowawezesha wasichana hawa kusoma kama wengine na kufikia malengo yao.
Tunaamini kama mfumo huu usingekuwapo wasichana hao wangeshindwa kufikia ndoto zao, lakini sasa wanakwenda kuendelea na masomo vinginevyo wangeishia kulea familia.
Hii ni fursa adimu inayopaswa kutumiwa kikamilifu na wasichana hao na haitarajiwi kuwapo kizuizi chochote kutoka kwa familia au kwasababu wana watoto basi waonekane jukumu lao ni kulea.
Kwa kuruhusu wasichana hawa kusoma sasa tunaendelea kuongeza idadi ya wanawake walisoma na kujitambua, lakini kwenye nafasi za maamuzi tutapata wanawake wengi ambao wamepitia changamoto na kujifunza umuhimu wa elimu.
Tunaamini kuwapo kwa mpango huu haitakuwa sababu ya wasichana wanaopata mimba kuongezeka, kwa kuwa wana uhakika wa kuendelea na masomo hata baada ya kujifungua bali iwe ni namna ya kujifunza kujirekebisha kwa kuwa elimu katika mfumo rasmi ni nzuri na inamfanya mwanafunzi kusoma kwa kuwa hana majukumu mengine.
Ikiwa vituo hivyo vitatumiwa vyema itakuwa ni sehemu ya kupika wataalamu ambao watalisaidia taifa, na watatumika kutoa elimu kwa wasichana kutoa mifano yao wenyewe ya maisha yao, ili wengine wasipite njia waliyopita wao.
Haitarajiwi kuona vituo hivyo vinageuka kuwa magofu bali kisima cha elimu nzuri, ili baadaye itakapofanyika tathmini tuone manufaa ya kuwa na mpango huu unaruhusu waliokosa elimu kwenye mfumo rasmi kuipata kama ambavyo kulikuwa na Mpango wa Elimu kwa Waliokosa (MEMKWA), ambayo ilikuwa na vituo kwenye wilaya na mikoa nchini.










