timu hiyo.
Kwenye mechi hiyo ya Ligi Kuu iliyochezwa Desemba 24, mwaka jana ambayo Simba ilishinda mabao 4-1, shabiki huyo alikuwa na furaha iliyopitiliza iliyomfanya kuruka na kuingia eneo lisiloruhusiwa kwenda kwa wachezaji wa Simba waliokuwa wakishangilia, lakini furaha yake ikageuka kuwa majonzi baada ya kukutana na kipigo kikali cha mbwa mwizi,
'akikatwa mitama' na mmoja wa walinda usalama uwanjani hapo, kitu ambacho kilileta malalamiko makubwa kutoka kwa wadau wa soka nchini Tanzania na hata nje ya mipaka.
Kwa hakika tukiwa wadau wa michezo, tulilaani vikali kitendo hicho na tukilitaka Shirikisho la Soka nchini (TFF), kutoa elimu kwa watu wa usalama kutotoa vipigo kwa mashabiki wanaoshindwa kuzuia hisia zao na kuingia uwanjani, na badala yake kuwatoa kwa usalama kwa kuwa si maadui, lakini tulikemea vikali tabia hiyo ya mashabiki kuingia uwanjani.
Hata hivyo, juzi tena kwenye Uwanja wa Benjamin Mkapa, katika mechi ya Simba dhidi ya Azam FC, lilitokea tena tukio kama hilo, baada ya shabiki mmoja kuvamia uwanjani, safari hii siyo kushangilia bao, yeye alikwenda kuonyesha 'mahaba' yake makubwa kwa kumkumbatia kipa namba moja wa timu ya Simba na Taifa la Tanzania, Taifa Stars, Aishi Manula.
Inawezekana kabisa kuwa wahusika walisoma maoni yetu, kwani wanausalama wa uwanja huo waliingia na kumchukua kijana huyo kistaarabu na uungwana wa hali ya juu na kisha kumtoa nje bila mvutano wala kipigo cha aina yoyote.
Nipashe tunatoa kongole kwa uungwana uliotumiwa na wanausalama wa uwanja huo kwa kitendo walichokifanya ambacho hakionyeshi tu kuwa ni cha kistaarabu, lakini kinaziambia hata nchi zingine za nje ya nchi kuwa Tanzania ni moja kati ya nchi ambazo zinathamini utu wa mtu.
Kumpiga mtu, mateke na kumswaga kama ng'ombe kama walivyofanya wanausalama wa Uwanja wa Ali Hassan Mwinyi mkoani Tabora, kunadhalilisha utu wa mtu na kujenga hofu kwa wapenda soka kuhudhuria uwanjani hasa wale wenye mihemko mikubwa na timu zao.
Lakini kitendo kama kile kinamdhalilisha mtendwa mbele ya familia yake ambayo hata kama haikuwapo pale pengine ilikuwa ikishuhudia kupitia televisheni ama kwa kuhadithiwa baada ya tukio lile.
Si kwamba tunaunga mkono vitendo vya mashabiki kuvamia uwanja, la hasha. Tunavikemea kwa nguvu zote na kuvipinga vikali huku tukitaka mashabiki wenye mihemko kujitahidi kujizuia, lakini pindi inapotokea tukio kama hilo, basi busara itumike kama ambavyo wamefanya wanausalama katika mechi kati ya Simba na Azam juzi Uwanja wa Benjamin Mkapa.
Ni kwa sababu wataufanya mchezo wa soka si tu uonekane wa kiungwana, lakini kuwafanya mashabiki waliopo uwanjani wajione wako salama na amani zaidi, na kusababisha watu wengine zaidi kuupenda na kuzidi kumiminika viwanjani, hasa wanawake na watoto ambao wanaandaliwa kuwa mashabiki wakubwa wa kesho.
Tunaamini wanaoshindwa kujizuia na kuingia uwanjani kuonyesha hisia zao, si maadui na wengi wao hawana nia ovu ya kwenda kuwadhuru wachezaji, hivyo TFF izidi kutoa darasa kwa walinda usalama, ili kuzidi kuufanya mchezo wa soka kuwa burudani na rafiki kwa kila mmoja anayehudhuria uwanjani.










