Ajali hizi zinaweza kuepukika hatua zikichukuliwa

05Jan 2022
Mhariri
Dar es Salaam
Nipashe
Ajali hizi zinaweza kuepukika hatua zikichukuliwa

JUZI watu 14 wa Kijiji cha Lindumbe Wilaya ya Newala mkoani Mtwara walifariki na wengine 22 kujeruhiwa, baadhi yao vibaya kutokana na ajali ya gari aina ya Scania linalobeba maji ya kutengeneza barabara, kuwagonga wakati wakicheza ngoma ya unyago.

Tukio hilo lilitokea juzi majira ya saa 2:00 hadi 2:30 usiku wakati wananchi hao walikuwa wakivuka barabara, huku wakicheza ngoma na kugongwa na gari hilo ambalo lilikuwa kwenye mwendokasi, bila kuwa na taa wala honi kuwatahadharisha wapiti njia.

Ni msiba mzito kwa familia na taifa kwa ujumla kwa kuwa sasa ndugu ambao walikuwa kwenye tukio la furaha limegeuka msiba mkuu kijijini hapo.

Nipashe inatoa pole kwa familia na marafiki walioondokewa na wapendwa wao, tunawaombea uvumilivu wakati huu mgumu.

Ajali hii inaonyesha kiasi gani dereva alikuwa mzembe kwa kuwa alipaswa kuhakikisha gari yake ina taa na breki zinafanyakazi.

Kutokana na uzembe huo maisha ya watu 14 yameteketea wakiwamo watu wazima, vijana na watoto huku wengi wakiwa wanategemewa na familia zao.

Kwa waliojeruhiwa wameingia kwenye hatua mpya ya maisha kwa kuwa kuna ambao hawatarudi kwenye afya zao kama awali, watakuwa wamepata ulemavu wakati huo kutakuwa na gharama kubwa ya matibabu na huenda wengine watachukua muda mrefu kupona.

Yote hii ni kugharimu maisha ya mtu mmoja mmoja kiasi cha kuathiri uchumi wa mtu na taifa kwa ujumla, kwa kuwa mtu aliyekuwa anategemewa sasa naye kageuka kuwa tegemezi au kaacha wapendwa wake ambao sasa hawana mtu wa kuwahudumia.

Kama watu hawa walikuwa wanafanya shughuli za uzalishaji na kulipa kodi hawataweza kufanya hivyo, maana yake idadi ya walipa kodi inapungua na mapato pia, na sasa tumeongeza wategemezi jambo ambalo ni hasara kwa taifa.

Ajali kama hizi hujitokeza kutokana na uzembe kwa kuwa kama dereva angepiga honi au gari ingekuwa na taa watembea kwa miguu wangeona na wangeepuka, hivyo ni muhimu kila anayeendesha chombo cha moto kuhakikisha taa na vifaa vingine muhimu vinafanyakazi ili kuwajali watumiaji wengine wa barabara.

Mwaka 2021 ulimalizika vyema bila matukio makubwa ya ajali tofauti na miaka mingine ajali za mabasi huwa ni nyingi, kutokana na kazi nzuri iliyofanywa na Jeshi la Polisi nchini, Kitengo cha Usalama Barabarani ya kuelimisha wananchi juu ya mwendokasi, alama na ukaguzi wa vyombo vya usafiri kila mara kumesaidia kupunguza.

Sasa ni wakati wa kufuatilia magari ya ujenzi na yanayovuta magari mengine yanapopata ajali ambayo kwa ujumla mengi yana hali mbaya, kiasi cha kuwa chanzo cha ajali.

Mathalani, Dar es Salaam magari hayo aina ya Rand rover huegeshwa kila kwenye makutano ya barabara ambako mara nyingi kuna ajali nyingi, ukiyaangalia baadhi ni mabovu na wakati mwingine hayana taa.

Lakini ipo haja ya Jeshi la Polisi kufanya ukaguzi wa kushtukiza kwenye njia nyingi Dar es Salaam, kwa kuwa wanaoendesha wengi sio madereva bali wanajifunza. Ni muhimu kufanya ukaguzi na kuhakikisha vyombo vyote vya moto viko salama, hasa nyakati za usiku kwa kuwa tayari kuna watu wamepoteza maisha kwa uzembe wa wachache.