Zanzibar idhibiti utoaji leseni kupunguza ajali

29May 2016
Mwinyi Sadallah
Zanzibar
Nipashe Jumapili
Zanzibar idhibiti utoaji leseni kupunguza ajali

HAKI ya kuishi ni jambo moja muhimu sana katika maisha ya binadamu, ndiyo maana imepewa uzito mkubwa katika katiba ya Zanzibar ya mwaka 1984.

Hakuna mtu asiyependa kuishi na ndiyo maana hukimbilia hospitali afya zinapotetereka kwa maradhi.

Hata hivyo, ajali za barabarani Zanzibar zimeanza kuvunja haki ya kikatiba ya kuishi kutokana na kuwepo kwa ongezeko kubwa katika visiwa vya Unguja na Pemba kwa mwaka.

Ripoti ya Haki za Binadamu Zanzibar ya mwaka 2015 imesema watu 150 walipoteza maisha na 791 walijeruhiwa katika ajali 26,832 zilizotokea Visiwani humo kipindi hicho.

Ripoti hiyo iliyoandaliwa na Kituo cha Huduma za Sheria Zanzibar (ZLSC), imesema zipo sababu mbali mbali za kuongezeka kwa jail ikiwemo uchakavu wa barabara, barabara hizo kutosafishwa mchanga na uzembe wa madereva wenyewe.

Uchakavu wa barabara umekuwa ukisababisha waendesha vyombo vya usafiri kukwepa mashimo na kuingia sehemu zinazotumiwa na watembea kwa miguu, na hivyo wakati mwengine kusababisha ajali na watu kupoteza maisha.

Kama watu wanalipwa mishahara kwa kazi ya kutunza barabara, kwa nini wanashindwa kusafisha michanga au kufukia kwa kifusi mashimo kabla ya hali kuwa mbaya na kusababisha ajali?

Utamaduni wa kufukia mashimo mapema yanapojitokeza kabla ya kuleta madhara ndiyo njia pekee ya kupunguza ajali pamoja na kuweka utaratibu mzuri wa matumizi ya barabara ikiwemo kuondoa tatizo la mifugo kuzagaa barabrani.

Na kama mamlaka zimeshindwa kusafisha barabara kwa nini kazi hiyo wasipewe kampuni binafsi badala ya barabra nyingi za rami kuendelea kukabiliwa na tatizo la mchanga na wakati mwengine kufikia nyasi kuota juu yake?

Pamoja na sababu mbali mbali zilizoelezwa kuwa chimbuko la ajali bado kuna umuhimu mkubwa wa kutoa mafunzo ya udereva katika vyuo vinavyotambulika badala ya watu kufundishana mitaani bila ya kuzingatia sheria za usalama barabarani.

Imekuwa kawaida maeneo mengi ya wazi Zanzibar kuwaona watu wakifundishana kuendesha magari badala ya kutumia vyuo maalum, wakiwemo watoto chini ya umri wa miaka 17.

Mapenzi ya wazazi pia yamevuka mipaka baada ya watoto wa chini ya umri wa miaka 18 kununuliwa vyombo vya usafiri, zikiwemo pikipiki na kuvitumia.

Wakati umefika kwa serikali kuweka mfumo mzuri wa upatikanaji wa leseni pamoja na kuondoa tatizo la rushwa na kusababisha watoto chini ya umri kupatiwa leseni na wengi wao kukumbana na ajali za barabarani.

Lazima ajali za barabarani zitaendelea kuongezeka kama watoto wadogo wanachiwa kuendesha pamoja na kuwepo kwa askari wa kusimamia usalama barabarani na wakati mwengine kupita mbele ya macho yao bila ya kuchukuliwa hatua.

Bila ya sheria kusimamia kwa nguvu zote ajali za barabarani zitaendelea kupoteza maisha ya watu na kuongeza idadi ya watu wenye ulemavu.

Udhibiti huo utakuwa kazi bure, hata hivyo, kama serikali haitaweka vituo maalum vya daladala ili kuzuia gari za abiria kusimama bila ya mpangilio na wakati mwengine kusimama katika maeneo hatarishi na kusababisha ajali.

Pia ni lazima ongezeko la idadi ya magari Zanzibar liendane na usimamiaji bora wa sheria za usalama wa barabarani kwa madhumuni ya kupunguza ajali na vifo.