Naona vinasaba vya Nyerere ndani ya Rais Magufuli

29May 2016
J.M. Kibasso
Dar es Salaam
Nipashe Jumapili
Naona vinasaba vya Nyerere ndani ya Rais Magufuli

BABA wa Taifa Mwalimu Julius Nyerere, aliongoza mapambano ya kudai Uhuru kwa ujasiri mkubwa hadi ulipopatikana Desemba 9 , 1961 miaka saba baada kuanzisha Chama cha TANU mwaka 1954.

BABA wa Taifa Mwalimu Julius Nyerere

BABA wa Taifa Mwalimu Julius Nyerere, aliongoza mapambano ya kudai Uhuru kwa ujasiri mkubwa hadi ulipopatikana Desemba 9 , 1961 miaka saba baada kuanzisha Chama cha TANU mwaka 1954.

Baada aya Uhuru kupatikana shabaha ya awamu ya pili ya vita vya ukombozi chini ya Mwalimu Nyerere ilikuwa ni kuyatumia madaraka yaliyopatikana kuyaongoza mapambano dhidi ya madhila ya ukoloni ili kumtoa Mwafrika katika unyonge na uduni wa maendeleo na kumfikisha katika hali ya neema na ustawi.

Katika awamu hiyo ya vita ya ukombozi jitihada zilielekezwa kupambana na maadui umaskini, ujinga na maradhi, shabaha au malengo ya harakati za kudai uhuru yalikuwa ni kutaka kurejesha haki iliyoporwa na wakoloni ya kujitawala wenyewe. Kujitawala wenyewe ni pamoja na haki ya kuunda mfumo wa kisiasa na kijamii na taasisi na asasi nyingine zitakazouwezesha umma kushiriki kama raia huru katika kuamua mambo ya msingi yanayogusa maslahi yao.

Katika kufanikisha azma hizo, Mwalimu Nyerere aliitisha Halmashauri Kuu ya TANU mwaka 1967 iliyokutana Arusha na kutangaza Azimio la Arusha na sera ya taifa ya Ujamaa na Kujitegemea.

Siasa ya Ujamaa ambayo misingi yake ililenga kuondoa unyonyaji wa aina yoyote na njia kuu za uchumi kumilikiwa na Watanzania wote (umma), ilileta kutaifisha mabenki, bima, biashara ya nje na ya ndani, mashamba makubwa, taasisi za huduma kama hospitali na shule.

Utaifishwaji huu uliwezesha kuundwa kwa sekta ya dola ya uchumi ambayo ilichukua nafasi ya mhimili katika uchumi wa taifa. Kwa kuzingatia mazingira hayo, changamoto kwa viongozi ilikuwa ni kubaini namna bora na endelevu ya kulinda uhuru na heshima ya utu taifa letu katika dunia ya kibeberu inayobadilika.Tusisahau kauli mbiu za kipindi hichi ilikuwa ni Uhuru na Umoja pia Uhuru na Kazi.

Kauli mbiu hizi zina maana kwetu sisi leo katika serikali ya Rais John Magufuli kama zilivyokuwa na umuhimu kwa mashujaa wa Uhuru na waasisi wa taifa letu. Ndiyo maana nimesema kuna kila dalili ya vinasaba vya uongozi wa Nyerere ndani ya Rais Magufuli.

Ni kauli mbiu zinazoashiria dhamira ya kisiasa ya kuandaa umma ili ushiriki kikamilifu katika ukombozi wake kwa kuyatumia madaraka tuliyopata kujiletea maendeleo na ustawi. Hii ndiyo dira endelevu ya Rais Magufuli.

Dhamira hii naiona katika serikali hii ya awamu ya tano kama ilivyokuwa kipindi cha mpito, Baba wa Taifa Mwalimu Nyerere mara baada ya kupata Uhuru, leo hii changamoto anazokumbana nazo Rais Magufuli pia haziachani na alizokumbana nazo Mwalimu Nyerere.

Rais Magufuli amedhamiria kubuni sera za kiuchumi na kijamii zenye lengo la kutuondoa katika hali ya unyonge bila kuvunja au kuvuruga msingi wa umoja wetu. Nachelea kusema kwamba kauli mbiu ya Rais inakwenda sawia na maudhui yaliyoainishwa katika Azimio la Arusha iliyotamkwa:-

“Tumeonewa kiasi cha kutosha, tumenyanyaswa kiasi cha kutosha, na tumepuuzwa vikali. Unyonge wetu ndiyo uliotufanya tuonewe tunyonywe na kupuuzwa. Sasa tunataka mapinduzi, mapinduzi ya kuondoa unyonge ili tusionewe tena, tusinyonywe tena na wala tusipuuzwe tena” (Azimio la Arusha ukurasa wa 9).

Dhamira ya serikali ya Rais Magufuli inaashiria kutetea matakwa ya Azimio la Arusha, hatua anazochukua, zinaendana na miiko na maadili ya viongozi alizosimamia Mwalimu Nyerere kwa nguvu zake zote, sasa zimeanza kuonekana katika awamu hii ya tano.

Ninachokusudia kusema ni kwamba nauona vinasaba vya uongozi wa Mwalimu Nyerere katika damu ya Rais Magufuli. Ni dhahiri Rais anapingana na udhalimu na aina zote na unyonyaji ambao kwa sasa umewatenganisha wenye nacho na wasio nacho au mafukara.

Falsafa yake ya kutumbua majipu kwa maana nyingine ya kuwaajibisha v viongozi wazembe, walevi, mafisadi na wanaotuhumiwa ni kiashiria tosha kuamini kwamba Rais Magufuli ana kila dalili ya vinasaba vya utawala wa Mwalimu Nyerere.

Inaelekea amedhamiria kwa dhati kupunguza pengo kati ya walio nacho na wasio nacho. Ni utawala uliojielekeza kwa wanyonge, unaokusudia kuanzisha vita vya ukombozi vya walalahoi yenye shabaha ya kuondoa unyonge, kuonewa, kunyanyaswa na kudhulumiwa. Bila shaka ushindi wa Rais utatokana na kutukuza na kudumisha maadili. Dhana ya maadili inadumishwa kwa nguvu za maoni ya umma kuhusu tabia, mwenendo, mila na desturi za watu katika jamii yenye lengo la kujenga usawa.

Ni dhahili kwamba, uamuzi wake wa kutengua uteuzi wa Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Charles Kitwanga, ni kiashiria tosha kuwa hazitambui tabia za kupendeleo wala kuoneana haya hata kama kunakufahamiana ama urafiki.

Mawasiliano:0713- 399 004, 0767 399 004,jmkibasso@gmail.com.