Wimbo huo unaonekana kuelezea jinsi Simba ilivyokuwa inaongoza Ligi Kuu kwa wiki nzima kutoka mikononi mwa Yanga, lakini kwa ushindi huo ikarejea tena kileleni kwa pointi 46 na kuiacha Simba na pointi zake 45.
Mabao ya Donald Ngoma na Amissi Tambwe ambao wote ni wachezaji wa kigeni, si tu yaliifanya Yanga kuongoza ligi, lakini pia kuendeleza rekodi yake nzuri dhidi ya Simba kwenye mechi za Ligi Kuu tangu ilivyoanzishwa mwaka 1965 ikiitwa Ligi ya Taifa na aliyekuwa kocha wa Taifa Stars, Milan Celebic.
Mechi ya Jumamosi iliyopita ilikuwa ni ya 81 tangu timu hizo kwenye Ligi Kuu bila kujumlisha mechi za Ligi ya Muungano kirafiki, Mtani Jembe, Kombe la Kagame na hata Tusker.
Katika ya mechi hizo Yanga imeifunga Simba mara 31, wakati Simba imeshinda mara 23. Timu hizo zimetoka sare mara 27.
Jumla ya magoli 168 yamefungwa tangu kuanza kwa Ligi Kuu mwaka 1965, Yanga ikiongoza kuifunga Simba magoli mengi zaidi.
Timu hiyo imeishindilia Simba magoli 91, huku Simba ikitumbukiza nyavuni kwa Yanga magoli 77.
Karne ya 21
Faraja pekee yaliyokuwa nayo wanachama na mashabiki wa Simba ni kwamba timu yao inaongoza kwa kuifunga Yanga tangu kuingia kwa karne ya 21.
Kwa mujibu wa rekodi zetu tangu kuingia mwaka 2000, Simba imeifunga Yanga mara 11, zikiwa zimetoka sare mara 15, huku Yanga ikishinda mechi nane kwenye mechi za Ligi Kuu tu.
Watani hao wamekutana mara 34 kwenye mechi za Ligi Kuu Bara.
Katika mechi hizo zote, magoli 65 yamefungwa, Simba ikiwa imefunga magoli 35 dhidi ya 32 ya Yanga.
Msimu mmoja yashinda mara mbili
Yanga imeweza kuifunga Simba mara mbili kwa msimu mmoja kwa mara ya kwanza tangu mwaka 1991.
Ikumbukwe kuwa kabla ya Ligi Kuu kubadilishwa na kuanza kuchezwa kwa mfumo wa msimu kama England, ilikuwa ikichezwa mwanzoni mwa mwaka hadi mwisho, hivyo timu zilikuwa zikikutana mwaka mmoja mara mbili, tofauti na sasa zinapokutana msimu mmoja, lakini miaka tofauti.
Mfano mechi ya kwanza Simba iliyofungwa mabao 2-0 msimu huu ilichezwa Septemba 26 mwaka jana.
Hii ni tofauti na mwaka 1991 Yanga ilipoifunga Simba mara mbili kwa msimu mmoja, lakini pia ilikuwa mwaka huohuo.
Ilikuwa ni Mei 18, Yanga ilishinda bao 1-0 lililofungwa na Said Sued 'Scud' dakika ya saba na mechi ya marudiano mzunguko wa pili ikashinda tena bao 1-0, mechi iliyochezwa Agosti 31, mfungaji akiwa ni yuleyule Scud.
Yanga kiboko kwa wafungaji
Katika mechi zote 81 zilizopita na kuzaa mabao hayo 168, winga machari wa Yanga Omar Hussein ‘Keegan’ wa Yanga ndiye anayeongoza kwa kufunga magoli mengi katika historia ya timu hizo, akiwa amezifumania nyavu mara sita akifuatiwa na straika Abeid Mziba pia wa Yanga aliyefunga magoli matano kwenye mechi zinazoihusisha timu hizo.
Mastraika wengine wa Yanga Idd Moshi na Jerry Tegete wa Yanga pia wao wamepachika mabao manne kila mmoja.
Hata hivyo, Simba nayo imeingiza wachezaji waliofunga magoli manne kwenye mechi za watani ambao ni marehemu Edward Chumila na Musa Hassan 'Mgosi'.
Rekodi zinasema kuwa tangu kuingia karne ya 21, yaani kuanzia mwaka 2000 wachezaji wanaoongoza kwa kufunga magoli mengi kwenye mechi za watani ni Mgosi na Tegete ambao kila mmoja amefunga magoli manne, idadi ambayo haijafikiwa na mchezaji yoyote ile karne hii.
Wachezaji waliopachika mabao matatu kwenye mechi za watani wa jadi kwa upande wa Yanga ni Kitwana Manara, Maulid Dilunga, Said Mwamba na Mohammed Hussein 'Mmachinga' Na kwa upande wa Simba ni Abdallah Kibadeni na Emmanuel Okwi.
Orodha hiyo inaonyesha waliofunga mabao mawili kwa upande wa Yanga ni Salehe Zimbwe, Juma Mkambi, Rashid Hanzuruni, Said Sued 'Scud', Makumbi Juma 'Homa ya Jiji’, Issa Athumani, Idelfonce Amlima, Sekolojo Chambua, Ben Mwalala na Sunday Manara.
Kwa upande wa Simba ni Jumanne Hassan ‘Masimenti’, John Makelele 'Zig Zag’, Malota Soma ‘Ball Jugler’, Nicodemus Njohole, Dua Said, Steven Mapunda 'Garincha', Madaraka Selemani, Ulimboka Mwakingwe, na Athumani Machupa.
Machungu ya Nyamagana 1974
Moja ya tukio litakalobaki kumbukumbu kwa muda mrefu kwa wanachama na mashabiki wa Simba ni mwamuzi Jonisiya Rukyaa kumtoa mapema beki Abdi Banda wa Simba dakika ya 20 na kuwafanya kucheza pungufu kwa muda mrefu, huku ikilazimika kubadilisha mbinu ilizokuwa nazo awali.
Tukio hili limeonekana kulalamikiwa sana na mashabiki wa Simba, ambao awali waliamini kuwa timu yao itaibuka kidedea.
Walidai kuwa rafu ya Banda ilikuwa nyepesi mno na mwamuzi hakupaswa kutoa kadi nyekundu, hasa ikizingatia mechi kubwa kama ya watani wa jadi.
Wakati Yanga wakitoka na nderemo na vifijo, Simba walitoka uwanjani wakilia na mwamuzi Rukyaa.
Hii inakumbusha miaka 42 iliyopita kwenye mechi ya Ligi Kuu (Ligi daraja la Kwanza Tanzania Bara wakati huo) iliyochezwa kwenye Uwanja wa Nyamagana mjini Mwanza.
Ni mechi ambayo haitosahaulika kirahisi na kizazi cha soka kilichokuwa hai wakati huo.
Katika mechi hiyo iliyochezwa Agosti 10, Yanga iliifunga Simba mabao 2-1 kwenye pambano kali, tata na lililokuwa na matukio ya kukumbukwa.
Simba ilielekea kuwa bingwa na kushinda mechi hiyo kwa bao 1-0 lililofungwa na Adam Sabu dakika ya 16.
Dakika ya 87 marehemu Gibson Sembuli aliisawazishia Yanga bao.
Dakika saba za nyongeza, Sunday Manara (baba yake mzazi Haji Manara msemaji wa Simba) akaiandikia Yanga bao la pili na kutwaa ubingwa.
Simba ilimlalamikia sana mwamuzi marehemu Manyoto Ndimbo kwa madai alikuwa amezidisha muda. Mchezaji Saad Ali wa Simba alianguka na kuzirai na mpaka sasa zipo simulizi kuwa eti sehemu ile aliyoangukiwa hapaoti tena majani hadi leo hii na wengine wakidai kumeota kichuguu.










