Hongera Magufuli kubainisha mjenga nchi ni mwananchi

21Feb 2016
J.M. Kibasso
Nipashe Jumapili
Hongera Magufuli kubainisha mjenga nchi ni mwananchi

Rais John Pombe Magufuli alikutana na Wazee wa Mkoa wa Dar es Salaam katika ukumbi wa Diamond Jubilee Jumamosi iliyopita, ikiwa ni kuitikia wito wao wa kutaka kumpongeza baada ya kumaliza siku 100 akiwa katika Ikulu ya Magogoni.

Rais wa Jamhuri ya Muungano ya Tanzania Dk. John Pombe Magufuli akisalimiana na Mwenyekiti wa Wazee wa mkoa wa Dar es salaam mzee Hemed Mkali.

Awali ya yote napenda nichukue fursa hii kumpongeza kwa dhati mwenyekiti wa Wazee, Hemed Mkali kwa kutambua Mchango wa Rais Magufuli katika siku 100.

Kama alivyotangulia kusema Rais Magufuli kwamba, “Ninyi wote wazee, mzee (Hemed) Mkali na wazee wengine mkiongozwa na Baba wa Taifa, mliihangaikia hii nchi tukapata Uhuru miaka zaidi ya 50 iliyopita; Uhuru tumeishaupata, sasa hivi kinachotakiwa ni maendeleo ya huo Uhuru mliokuwa mkiutafuta.

Kauli hii ya Rais Magufuli kuhusu kipindi cha Ukombozi inanikumbusha maneno ya Baba wa Taifa, Mwalimu Julius Nyerere kuwa vyama vya ASP na TANU wakati huo, vitaendelea kuwa vyama vya ukombozi wa wanyonge hata baada ya kupatikana Uhuru.

Nirejee katika hotuba ya Rais Magufuli. Kimsingi niseme tu kwamba hotuba ile ilijaa unyenyekevu, utu na heshima mbele ya wazee. Mara zote alitanguliza utu na hivyo kuifanya mapokeo yake kupenya kwenye mioyo ya wazee waliokuwa wakimsikiliza.

Kwa mfano kuna wakati Rais Magufuli aliweka Urais wake pembeni na kuwaangukia wazee wa Dar es Salaam mithili ya mtoto mdogo.

"Saa nyingine unapozungumza na wazee lazima uwe mwangalifu kwasababu unaweza ukakosea na ukatandikwa viboko hapo hapo, lakini kama yapo wazee wangu niliyowakwaza mnisamehe, lakini nimezungumza haya yote kwa sababu ya uchungu wa Tanzania yangu,” Alisema Magufuli.

Maneno hayo yanaweza yakachukuliwa kama ni ya utani, lakini kwa vijana wa zamani waliobahatika kufundwa na wazee wao katika mila, miiko na tamaduni za makuzi, watakubaliana na mimi kwamba maneno hayo ya Rais magufuli yalijaa utii na heshima ya hali ya juu kutoka sakafu ya moyoni mwake.

Kikubwa alichokigusia Rais Magufuli na nina imani ndiyo ukweli lakini inauma, na mara nyingi binadamu hapendi kuambiwa ukweli, ni pale alipowageukia watanzania na kuwataka badala ya kupima utendaji wa serikali yake tu katika siku 100 hizo, nao pia wafanye tathimini ya walichoifanyia nchi katika siku hizo.

Kila mmoja wetu, kila mahali alipo, ana wajibu na yeye wa kujipima kwamba katika siku hizi 100 za awamu ya tano ameifanyia nini Tanzania.

Hii ni changamoto kwa jamii kwasababu mjenga nchi ni mwananchi mwenyewe. Bila shaka shabaha ya Rais Magufuli ilikuwa ni kufuta fikra ya walio wengi wanaodhani kuwa ujenzi wa nchi uko mikononi mwa serikali pekee.

Bila kumung’unya maneno, hotuba ile ilijaa busara na hekima. Ni hotuba elekezi kwa watendaji wa serikali lakini pia kwa jamii ya watanzania.

Hatuwezi kubaki kuwa jamii inayolalama tu, matatizo mengine yanayotukabili yapo ndani ya uwezo wetu.

Rais alirudia tena kauli yake aliyoitoa siku za nyuma alipozungunza na wafanyabiashara akisema, wawekezaji wazalendo wa kitanzania, huu ni wakati wao kwani nchi hii haiwezi kujengwa na watu kutoka nje. Kwamba rasilimali tumepewa na Mungu lazima tuziendeleze sisi wenyewe.

Nitumie fursa hii kutoa ushauri kwa serikali ya Rais Magufuli kwamba iongee na taasisi za fedha zinazotoa mkopo ili wafikirie watanzania wa hali ya chini, kwani masharti ni magumu mno.

Mfano mtu mwenye leseni ya makazi hatambuliki kwenye taasisi hizi ambazo huhitaji hati kutoka Wizara ya Ardhi.

Sambamba na hilo nimalizie kwa kumwomba Rais Magufuli kwamba serikali ianze kuona utaratibu wa kuwaajiri moja kwa moja wanafunzi wanaotoka vyuoni. Kwa mfano, wanafunzi wanaomaliza Chuo cha Uhasibu katika kiwango cha ama digrii au diploma wachukuliwe moja kwa moja kwenye Halmashauri zetu badala ya kusubiri uzoefu.
Hongera Rais Magufuli kwa hotuba yako nzuri kwa wazee wa Dar es Salaam.

Mob: 0713 -299 044 / 0767 399 004
Email: jmkibasso@gmail.com