Wanahabari wa leo wanavyotishiwa na maslahi duni, kukosa usalama

12Oct 2023
Na Mwandishi Wetu
DAR ES SALAAM
Nipashe
Wanahabari wa leo wanavyotishiwa na maslahi duni, kukosa usalama

USALAMA wa waandishi wa habari ni muhimu katika kutekeleza majukumu ya kupasha umma habari kwa kuhakikisha kuwa kuna uwajibikaji katika kila linalofanyika ili wananchi wanufaike na rasilimali zao, haki itamalaki na demokrasia kushamiri ndani ya taifa.

Kwa wanahabari usalama huanzia kwenye uhuru na ubora wa kipato, hali kisaikolojia, kidijitali, sehemu ya kazi kuwa na vifaa vya kisasa,haki za kisheria kama likizo, stahiki mbalimbali kama posho na kwenye mifuko ya hifadhi ya jamii, matibabu na kulindwa akitekeleza majukumu yake kwenye jamii kama kwenye mikutano ya hadhara.

Pia, haki ya kupata taarifa kama ilivyoainishwa kwenye Sheria ya Haki ya Taarifa 2016, ambayo inawataka maofisa wa serikali kutoa taarifa kwa mujibu wa sheria, ili kusiwe na kikwazo chochote kwa mwandishi wa habari kutekeleza majukumu yake.

Sheria ya Huduma ya Habari mwaka 2016, imeweka kipengele cha kuwabana waajiri kuhakikisha wanahabari wanakuwa na bima za afya, ingawa utekelezaji wake umekuwa wa kusuasua.

Mwaka jana, Shirika la Umoja wa Mataifa la  Elimu, Sayansi na Utamaduni (UNESCO), linachapisha ripoti inayoonyesha ongezeko la asilimia 50 la mauaji ya wanahabari mwaka 2022, ikimaanisha kuwa mwandishi mmoja anauawa kila baada ya siku nne.

Aidha, ripoti hiyo inabainisha kuwa hakuna yeyote aliyekamatwa wala kufikishwa mahakamani katika asilimia 86 ya kesi zilizofunguliwa kwenye mataifa mbalimbali duniani, huku Mexico ikitajwa kuwa kinara kwa mauaji ya wanahabari sawa na Haiti, huku sababu kubwa ikiwa ni kutokana na uandishi wa taarifa za uhalifu, mizozo, rushwa na mazingira.

Ripoti ya 21 ya Waandishi Wasio na Mipaka (RSF) ya mwaka 2023, inayoangazia siasa, jamii na tekonolojia katika mataifa 180 imebainisha kuwa hali ni mbaya katika mataifa  31, ni ngumu kwenye nchi 42,  ni tatizo ndani ya nyingine  55 na ya kuridhisha katika nchi 52.

“Kwa maneno mengine mazingira ya uandishi wa habari ni mabaya katika nchi saba kati ya 10, ya kuridhisha kwenye mataifa matatu pekee kati ya 10,”inasema ripoti hiyo.Kielelezo cha Uhuru wa Vyombo vya Habari Duniani kinaonyesha hali tete, kukiwa na kupanda na kushuka kwa kiwango kikubwa na mabadiliko ambayo hayajawahi kushuhudiwa, kama vile Brazili kwa nafasi ya 18 na kuanguka kwa Senegali kwa nafasi ya 31.”

“Kukosekana kwa utulivu huku ni matokeo ya kuongezeka kwa uchokozi kwa upande wa mamlaka katika nchi nyingi na kuongezeka kwa chuki dhidi ya wanahabari kwenye mitandao ya kijamii na katika ulimwengu wa kimwili.Kuyumba huko ni matokeo ya ukuaji wa tasnia ya maudhui ya kughushi ambayo huzalishwa na kusambaza taarifa potofu na kutoa zana za kuzitengeneza,”anasema Katibu Mkuu wa RSF, Christophe Deloire

Kwa mujibu wa ripoti hiyo, Tanzania imeshika nafasi ya 143 ikichukua alama 44.02 ikilinganishwa na nafasi ya 123 mwaka 2022 ikiwa na pointi 48.28, katika moja ya mambo muhimu ambayo ripoti hiyo imeangazia  kwa taifa hili ni maslahi duni hali inayowafanya washindwe kuwa huru katika kutekeleza majukumu yao.

“Waandishi wanalipwa malipo duni huku kazi yao ikiwa ni ya hatari. Serikali inawajibu mkubwa kwenye uchumi wa vyombo vya habari, vyombo vya binafsi vinapata matangazo yake kati ya asilimia 40 hadi 80 kutoka serikalini, na Februari mwaka 2022 serikali iliahidi kutoa matangazo kwa vyombo vyote kwa ushindani,”inasema sehemu ya ripoti hiyo.

Kuhusu usalama RSF inasema mwaka 2022 vyombo na waandishi wa habari waliacha kukosoa utawala kwa kuhofia kufungiwa, kushikiliwa na kutekwa huku serikali ikieleza kwamba hakuna jambo kuhusu Azory Ngwanda aliyetoweka katika mazingira tatanishi mwaka 2017.

Ofisa Programu anayeshughulikia utafiti, mafunzo na machapisho wa Umoja wa Klabu za Waandishi wa Habari Tanzania (UTPC), Victor Maleko, anasema kuna mabadiliko makubwa kwa madhila wanayopitia waandishi wa habari kutokana na ushirikiano uliopo baina ya wadau wa habari na serikali.

Anasema mwaka jana yaliripotiwa madhila 26 lakini kwa mwaka huu yamerekodiwa tisa pekee, na kwamba mengi ni mvutano baina ya mamlaka na wanahabari kukamatwa na vitisho.

“Madhila wanayokutana nayo zaidi ni kutishiwa maisha na kukamatwa na polisi, mfano mwaka jana wengi walikamatwa na kutishiwa wakiambia usiandike habari hii nitakuondoa kwenye hili eneo au nitakukamata. Mambo yanayofanywa na taasisi za serikali kama wakuu wa wilaya au makatibu tawala,  lakini kutumia mazungumzo kumesaidia,”anasema Maleko.

Aidha, kuna nyakati ambazo waandishi hukosea na kwenda kinyume na sheria na taratibu na wanapoambiwa huwa wabishi kwamba wako kwenye utekelezaji wa majukumu yao, anaeleza na kuongeza: “Baadhi ya maeneo tumeona wenyewe wanakuwa chanzo cha migogoro, anaambiwa usifike hapa anafika kwasababu tu ni mwandishi, kuna baadhi wanakosa weledi au kutojua, kuna wengine wanaandika mambo yanayoleta taharuki kwenye nchi au eneo jambo ambalo siyo sawa.”

Aidha, anashauri kila mmoja, waandishi na serikali wafanyekazi kwa kuzingatia maadili ili kuondoa mvutano na kwamba kila upande ukisimama eneo lake na kuzingatia misingi haitafika kwenye hatua ya kupishana, kwa mujibu wa Maleko, na kuona umuhimu wa kuzijua sheria na taratibu zilizopo kwa kuwa hakuna taaluma iliyo juu ya sheria.

Kuhusu malipo na usalama wa wanabahari, anasema ili mwandishi atekeleze majukumu yake vizuri ni muhimu akalipwaipasavyo  ikiwa ni pamoja na kuwa na bima ya afya ili afanyekazi kwa kujiamini.

Mwenyekiti wa Chama cha Wafanyakazi wa Vyombo vya Habari (JOWUTA), Mussa Juma, anasema usalama wa waandishi ni mdogo kutokana na kwamba wengi hawana kipato cha uhakika huku mikoani zaidi ya asilimia 95 hawana ajira wala mikataba.

“Serikali isimamie sheria ili wawe na maslahi bora na usalama iwe ni sehemu ya masuala ya msingi ya sheria za wanahabari nchini. JOWUTA tunafanya mafunzo ya ulinzi na usalama kazini, pia tunakusanya taarifa za waajiriwa na wasio na ajara, ili tuishawishi serikali kulipa madeni ya vyombo vya habari ili viwalipe wafanyakazi,”anasema.