Mtihani anaoupata mwanafunzi kwenye daladala kwenda na kurudi shule

05Oct 2023
Christina Mwakangale
​​​​​​​Dar es Salaam
Nipashe
Mtihani anaoupata mwanafunzi kwenye daladala kwenda na kurudi shule

WANAFUNZI wanaosoma elimu ya kutwa hususan jiji la Dar es Salaam, ni miongoni mwa wanaokumbana na changamoto ya usafiri waathirika wakuu ni waliopo mwaka wa mitihani ya kitaifa; darasa la nne na la saba.

Dar es Salaam ni kati ya majiji 10 yanayokua kwa kasi barani Afrika, likishika nafasi ya pili, ikitanguliwa na jiji la Abidjan nchini Ivory Coast, huku la tatu likiwa Addis Ababa (Ethiopia), kwa mujibu wa utafiti wa Afrika Reloaded, mwaka 2021.

Ukuaji huo umekuwa ni changamoto. Mojawapo ni usafiri wa umma ambao hutegemewa na wakazi wa miji hiyo, ikiwamo wanafunzi ambao wanakwenda na kurudi shuleni siku tano za wiki.

Dar es Salaam, ina wakazi milioni 5.4 kwa mujibu wa Sensa ya Watu na Makazi Mwaka 2022, hali hiyo imesababisha jiji kuwa na msongamno mkubwa watu, magari yanayokadiriwa kuwa milioni moja kwa mujibu wa Kikosi cha Usalama Barabarani nchini.

Hali hiyo imetajwa kusababisha foleni baadhi ya maeneo hususan majira ya asubuhi na jioni, licha ya maboresho ya miundombinu ya barabara yanayoendelea.

Wadau wa elimu ikiwamo wanasaikolojia, walimu, wanaharakati na wataalamu, wanaziona athari zitokanazo miji kukua na kusababisha mazingira duni ya ujifunzaji mwanafunzi, kama vile uhaba wa usafiri wa umma, ukiwa chanzo cha kikwazo cha uelewa na kushusha ufaulu wa masomo ya darasani.

Uchunguzi uliofanywa na Nipashe kwa kipindi cha miezi miwili, umebaini wanafunzi wa jiji hilo, wanaosoma shule za msingi za umma, nyingi zikiwa za kutwa hutumia kati ya saa 15 hadi 16, kuwa nje ya nyumbani, kila siku.

Hesabu hiyo ni muda wa safari ya kwenda na kurudi shule, ambao ni takribani saa nne hadi tano kwa siku, na muda unaosalia mwanafunzi huutumia akiwa mazingira ya shule ambazo ni saa nane kwa siku tano za wiki, kwa mujibu wa Sera ya Elimu ya Msingi Toleo la Tatu la Mwaka 2019.

Ofisa Elimu wa Mkoa Dar es Salaam, Abdul Maulid, akizungumza na Nipashe anasema hadi kufikia mwaka 2021 mkoa wa huo, ulikuwa na shule za msingi 780 ambazo nyingi ni za umma na kutwa.

Kadhalika, taarifa ya Katibu Tawala Msaidizi ambaye pia ni Ofisa Elimu wa Mkoa, kwenye ukurasa wa tovuti ya mkoa huo, anasema ongezekao la watu ni changamoto, kwa kuwa uwiano wa watoto ni mkubwa kuliko mikoa mingine na inasababisha idadi kubwa ya wanafunzi katika mkoa wa Dar es Salaam.

Mwalimu na mtunzi wa vitabu, Richard Mabala, akijibu kuhusu suala hilo, anasema utafiti uliwahi kubainisha baadhi wanafunzi huacha shule kutokana na athari za mwendo mrefu kufuata shule ilipo, akishauri kuitwa mjadala wa kitaifa, kuondoa adha hiyo akiitaja imedumu kwa miaka 30.

MAISHA YAO

Mwanafunzi Amina Shirima (si jina halisi), anaishi jijini Dar es Salaam, wilaya ya Ilala, Kwa Mkolemba, anafuata masomo kila siku shule ya msingi Msasani, iliyopo wilaya ya Kinondoni, umbali wa takribani kilomita 35 kutoka anakoishi.

Amina (12) anasoma darasa la saba, anazungumza na Nipashe, majira ya jioni, iliyokutana naye kwenye usafiri wa daladala ruti ya Gongo la Mboto-Msasani, akirejea nyumbani, anasema kila jioni, anaporudi nyumba inampasa kuzunguka na daladala, ili angalau apate siti ya wanafunzi, iliyotengwa jirani na kiti cha dereva.

Anasema jioni hutumia Sh. 800 kwa safari ya kwenda shule na kurudi nyumbani, kwa kuwa nauli ya safari moja kwa mwanafunzi ni Sh. 200.

“Napandia daladala hapa kituo cha Shule (Msasani), naenda kugeuka nalo Masaki mwisho, nalipa Sh. 200 alafu gari likigeuka kurudi Gongo la Mboto nalipia tena Sh. 200 jumla 400. Pia nikishuka kituo cha Mombasa, napanda tena daladala kuelekea Kwa Mkolemba nalipa Sh. 200 au nikipanda bajaji nalipa Sh. 500. Kwa siku napewa Sh. 2,000 inayobaki nanunua mihogo shuleni,” anasema Amina.

Amina, anasema huamka saa 11 alfajiri na kufika shuleni saa moja asubuhi na akirudi kutoka shuleni hufika nyumbani saa tatu au saa nne usiku.

“Nachoka…naamka asubuhi sana, narudi usiku. Mama amesema siwezi kuhama mwaka wa masomo. Zamani tulikuwa tunakaa huku (Msasani) ila baba amejenga huku (Kwa Mkolemba-Gongo la Mboto), na tumehamia mwaka jana,” anasema.

WADAU NA WALEZI

Mkurugenzi Mtendaji wa Shirika la Wanawake Katika Jitihada za Kimaendeleo (WAJIKI), Janeth Mawinza, anasema miongoni mwa sababu zilizolisukuma shirika hilo kuanzisha kampeni ya 'Safari Salama, Bila Rushwa ya Ngono kwa Wanafunzi na Wasichana Inawezekana'

“Tulibaini wanafunzi wanaosafiri kwa saa nyingi kwenda shuleni na kurudi nyumbani, huathiriwa na ukatili huku jamii na abiria kwenye usafiri wa umma, daladala, kutojihusisha moja kwa moja na changamoto hizo. Watoto wanaosoma mbali na wanapoishi wanakumbwa na ukatili.” anasema Janeth.

Mwalimu Richard Mabala, anasema tatizo la mwanafunzi kusoma umbali mrefu kutoka anakaoishi limetokana na kutoheshimiwa mipaka ya kiutawala kama vile kata, ambayo ikizingatiwa wanafunzi watasoma kwenye kata zao.

“Lakini uhaba wa walimu kwenye shule ni tatizo, mzazi anaona hawezi kumsomesha mwanae ambako kuna walimu wachache, au vifaa duni vya kufundishia hata miundombinu. Tatizo hili limedumu kwa miaka karibu 30 sijui kwa nini hatutafuti suluhisho, kutoelewana baina ya wanafunzi, wenye daladala na serikali,” anasema.

“Kila shule iwe na daladala lakini hili uwezekano ni mdogo. Hali hii imesababisha wanafunzi baadhi kubakwa, kufanyiwa ukatili, kutongozwa. Mipaka ya kata iheshimiwe, ukisema shule ya kata iwe hivyo. Mkutano uitishwe kuondokana na hili,” anabainisha Mwalimu Mabala.

Mwalimu wa shule ya msingi mstaafu, Paulina Julius, anasema ili mwanafunzi apate uelewa, kunahitajika vitu kadhaa ikiwamo mwalimu bora, miundombinu, mazingira rafiki na mwanafunzi mwenyewe.

“Mazingira wezeshi, kupumzika baada ya masomo yote ni mazingira yanalyoleta matokeo chanya ya mwanafunzi. Shule zote zina ushindani wa matokeo hivyo nyingi agizo ni wanafunzi wa mwaka wa masomo kuanza vipindi saa 12 asubuhi. Madarasa ya Jumamosi nayo yamerudi.

“Anayeathirika zaidi ni mtoto wa kike ambaye ana majukumu mengine ya kijinsia, ambaye akifika nyumbani anatakiwa aoshe vyombo, apike tofauti na mvulana,” anasema Paulina.

MSAFIRISHAJI

Kondakta wa daladala inayofanya safari kati ya Gongo la Mboto na Masaki, Dar es Salaam, Rashid Hamza, anaiambia Nipashe kwamba, kwa siku kati ya abiria ambao huwasafirisha huwapo wanafunzi wenye umri tofauti.

“Kwa uzoefu wa kazi yangu huwa napenda kuwapakia abiria ambao ni wanafunzi wadogo yaani siwaachi kituoni. Wale wakubwa wa sekondari naona angalau wanauelewa. Najiuliza hivi mzazi ana amani gani kumsomesha mwanae shule mbali na anapoishi.

“Kwa siku ninawavusha barabara watoto watatu au wanne. Kwa sababu ukimshusha upande huu wa kituo anahitaji kuvuka upande wa pili anakoishi, sasa mtoto mdogo wa miaka tisa au 10 anakabilinaa vipi na magari ya jiji,” anasema kondakta huyo.

Amesema wapo wanafunzi ambao wakipata nafasi ya kujiegesha kidogo, hulala mwanzo hadi mwisho wa safari, na kuwa katika hatari ya kupitilizwa kituo.

MZAZI

Martha Mwakalukwa, ni mzazi, anaishi Karakata, jirani na ulipo Uwanja wa Ndege wa Mwalimu Nyerere (JNIA), jijini Dar es Salaam, anasema hapendi mwanaye asome mbali na wanakoishi, ila mazingira ya maisha yamesababisha.

“Mimi nimeishi Msasani muda mrefu, mume wangu alikuwa anakaa kwenye nyumba za watu ambao walimweka kama mlinzi, hivyo watoto tuliowapata tuliwaandikisha shule ya msingi Msasani.

“Baada ya miaka 10 tumejaliwa nyumba ambayo tumejenga Karakata, mwanangu wa mwisho yupo darasa la nne siwezi kimhamisha hadi mwaka wa mtihani wa darasa la nne uishe,” anasema Martha.

WALINZI WA JAMII

John Ambrose, mwasaikolojia, anasema asilimia 30 ya watoto kufeli kwenye mitihani yao ya darasani huchangiwa na kukosa muda ya kupumzisha ubongo, kwa kuwa hulala kwa muda mfupi wa kulala.

Anasema jamii inahitaji kuelimishwa kuhusu kulinda afya ya akili kwa mtoto kwani ni eneo muhimu, akisema wengi hawapumziki, na kuna athari hasi ubongo kutopumzishwa.

Busungu Mathias, mwanasosholojia, anasema changamoto wanazopata watoto wa shule katika maeneo ya majiji au miji mikubwa kama Dar es Salaam, Mwanza na Arusha, zinatokana na sababu nyingi.

“Kwanza ni changamoto ya umasikini wa kipato, kwani wazazi hawana uwezo wa kipesa kiasi cha kumudu gharama za usafiri binafsi kwa watoto wao, ili waweze kufika shule kwa wakati, lakini pia bila usumbufu.

“Pili, mpangilio mbovu katika kuwachagulia watoto shule za kwenda kusoma mara baada ya kuhitimu elimu ya msingi na kuchaguliwa sekondari, ni ajabu sana mwanafunzi awe amemaliza darasa la saba Gongo la Mboto, kisha apangiwe kidato cha kwanza Sinza au Makumbusho,” anasema Busungu.

Anabainisha kikwazo cha tatu kuwa, ni ongezeko la foleni za magari barabarani jambo linalosababisha kutumia muda mwingi kusafiri, na kwamba kukosa usafiri mzuri usio na bughuza njiani kwa watoto, ni tatizo.

Jambo lingine, ni ongezeko au idadi kubwa ya watu katika miji mikubwa jambo linalosababisha uhaba wa vyombo vya usafiri wa umma, anasema.

“Majiji na miji mikubwa haitofautiani na watoto wa vijijini kutembea umbali mrefu zaidi ya kilomita sita, kutoka nyumbani hadi shuleni kwa mguu."

ATHARI

Mtalaamu huyo wa jamii anasema, madhara ya watoto kusafiri umbali mrefu kwenda shuleni ni pamoja na anakosa muda wa kutosha wa kusoma na kujisomea kwa kuwa muda mwingi anautumia kugombania usafiri au kutembea umbali mrefu.

“Kwa utafiti usio rasmi (kati ya saa 24 takribani saa sita, hutumika kutafuta namna ya kufika shuleni, saa tisa hutumiwa shuleni na saa tisa kwa ajili ya kupumzika na shughuli za nyumbani,” anasema Busungu akiongeza:

Busungu anasema mwanafunzi huyo hufikiri kuhusu kutafuta usafiri na kuwaza muda mwingi namna ya kupata usafiri kurudi nyumbani huku viwango vya ufaulu kwa ngazi ya shule na miji, vikishuka.

“Watoto wa sasa hukosa muda wa kutosha kucheza, kukaa na wazazi au walezi wao kama moja ya njia ya kuboresha mahusiano (bond)."

Mwanasosholojia huyo anashauri, serikali kuangalia upya utaratibu wa upangaji wa shule, kuondokana na dhana kwamba shule bora ipo mbali kuliko jirani na anapoishi.

Daktari wa Binadamu, Shadrack Mwaibambe anasema: “Mtoto hana ratiba ya kucheza, kukaa na ndugu zake, wazazi wake, anarudi nyumbani amechoka…saa 10 alfajiri ameamshwa. inaathati kiafya.”

SERA ELIMU INASEMAJE?

Sera ya Elimu ya Msingi Toleo la Tatu la Mwaka 2019, linaelekeza mwanafunzi akae darasani kwa siku tano za wiki, ikiwa na jumla ya muda usiozidi saa 30.

Kwamba, wanafunzi watasoma vipindi 38 kwa wiki, ambayo ni sawa na jumla dakika 1,520 ambayo ni sawa na saa 25 na dakika 33; hiyo inaangukia wastani wa saa tano kwa kila siku ya masomo.

Uwiano unaoonyesha wastani wa saa sita uliotajwa kwenye sera, unajumuisha muda wa ziada wa mengineyo kama mapumziko.