Huo ni mwitikio wa swali lililoulizwa katika mafunzo ya siku mbili ya kutetea haki za watu wenye ulemavu na hasa wanawake na wasichana, dhidi ya madhara ya rushwa ya ngono.
Katika kundi hilo la washiriki, baadhi ni watu wenye ulemavu na wengine ni wasio na ulemavu.
Mafunzo hayo yalifanyika kuanzia Mei 21 hadi 22 mwaka huu kijijini Masaki, wilayani hapa na yaliandaliwa na Taasisi ya Waandishi wa Habari za Watu Wenye Ulemavu (TAWAHATA) kwa kushrikiana na asasi ya Women Fund Tanzania.
Washiriki kutoka kata za Msimbu, Kibuta, Kazimzumbwi na Masaki, wote hakuna aliyekiri kukabiliwa na dai la rushwa ya ngono kutoka kwa wanaume, ingawaje wapo waliokiri kukabiliwa na matukio ya ubakaji, hata kuwa na kesi katika vyombo vya sheria.
Mafunzo hayo yaliandaliwa na Taasisi ya Waandishi wa Habari za Watu wenye Ulemavu (TAWAHATA) kwa kuishirikiana na asasi ya Women Fund Tanzania.
Wawezeshaji katika mafunzo hayo, walibaini ugumu wa washiriki kuwa wawazi kuhusu yale waliokumbana nayo, ingawaje ilikuwa vigumu kutambua sababu za kufanya hivyo.
Mwezeshaji katika mafumzo hayo, Enock Kijo, anasema kuwa wanawake wanaokabiliwa na rushwa ya ngono, ni wasiokuwa na uwezo na hasa walemavu,
Kijo anasema kuna baadhi ya wanaume wanaotumia mamlaka na uwezo wao katika kutoa huduma mbalimbali, kuwanasa wanawake kimapenzi.
Kijo anataja baadhi ya maeneo mitego hiyo ya kulazimisha mapenzi dhidi ya wanawake ni kazini, shuleni, vyuoni na kwenye vyombo vya sheria.
Mwezeshaji Enock anawakumbusha watu hao wanaotumia vibaya mamlaka yao, kwamba wanakinzana na misingi bora ya watu kuishi.
Kijo anaorodhesha misingi hiyo kuwa ni Utu, Uhuru, Usawa, Maendeleo, Haki, Umoja, Utaifa na Uzalendo na Amani na Maadili.
“Kila mmoja akizingatia misingi hii, bila ya shaka kesi kama hizi za rushwa na makosa mengine yanayolingana na haya, hayatafanyika kwa kila mtu atalazimika kuzingatia misingi,” anasema.
Ofisa Uchunguzi wa Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU), Walter Jacob, akichangia hoja, anasema kuna mazingira ya usiri ambao wengi hawauweki hadharani, lakini kuna ukweli juu ya kuwapo rushwa hiyo.
Jacob anataja adhabu ya makosa ya rushwa ya ngono, kwamba ni kali kutokana na hatari na madhara yake katika jamii.
Anasema kosa la rushwa ngono kulingana na Sheria za Rushwa ya mwaka 2007, adhabu yake ni kifungo cha miaka mitatu au faini ya Sh. milioni tano au vyote kwa pamoja.
Ofisa huyo anataja waathirika wengi kuwa ni wanawake, wanafunzi na watumishi wa ngazi za chini katika sehemu za kazi.
Walter anataja madhara husika kwamba ni pamoja na ukiukwaji wa haki za binadamu, mimba zisizotarajiwa, kuzorotesha utendaji kazini, maambukizi ya magonjwa ya zinaa na kwa ujumla inarudisha nyuma maendeleo ya nchi.
Ushauri wake ni kwamba endapo kutakuwapo ujasiri wa kukataa dai la rushwa hiyo ya ngono, kuna manufaa mengi yanayopatikana.
Miongoni mwa faida anazotaja ni kuleta heshima, kujenga ujasiri, kazi ajira zisizo na upendeleo na kuepuka magonjwa ya zinaa.
“Nawaomba washiriki kuacha kuficha siri, kwani mficha siri, kifo kitamfichua, kumbukeni madhara yake hayo,” anasema.
Washiriki walionekana kusifu mafunzo yaliyowapa mwanga na ujasiri wa kutoa taarifa endapo watakumbwa na mikasa ya aina hiyo.
Mshiriki, Mwazani Ibrahim (25), anaomba mafunzo hayo yafanyike mara kwa mara, ili kupanua wigo wa hamasa kwa wengi.
“Mafunzo nimeyaelewa vizuri, lakini ni vyema yakaendelea kufanyika kwa wengine. Kwa mimi sasa sidanganyiki, nitatoa taarifa nikikumbwa,” anasema kwa ujasiri.
Mwingine ni Halima Ali (40), anasema: “Naiomba serikali iongeze adhabu kusaidia kukomesha makosa, kwani sisi watu wenye ulemavu, ndiyo tunakuwa wahanga (waathrika) wakubwa kutokana na unyonge wetu.”










