Watu wengi wanatamani kufanya shughuli hiyo, lakini wanashindwa kutokana na sababu mbalimbali.
Baadhi ya sababu hizo ni ugumu wa upatikanaji vifaranga vya samaki, ukosefu wa elimu ya ufugaji, soko na utunzaji wa mabwawa yake.
Abdallah Salum Issa na Ahmed Salum Issa, ni wafugaji samaki wa kijiji cha Pujini kisiwani Pemba. Ni miongoni mwa wafugaji wanaokabiliana na baadhi ya changamoto za ufugaji.
ELIMU YA CHINA
Abdallah anasema wameanza biashara hiyo tangu mwaka 2000 wakiwa hawana ujuzi wowote. Mwaka 2011 Serikali ya Mapinduzi Zanzibar (SMZ), iliwapeleka nchini China kusomea ufugaji wa samaki.
Wanandugu hao wanakiri kila mmoja kwa wakati wake kwamba, elimu ya China imewapa mbinu za kisasa za ufugaji samaki na kuwahamisha kutoka mtindo wa zamani.
Abdallah anasimulia kuwa baada ya kurudi kutoka China, hakuwa mchoyo. Alitumia fursa hiyo kuwafunza wenzake njia bora za kufuga samaki na sasa wameshirikiana na wafuga samaki wengine kuanzisha ushirika wao wa ufugaji uitwao ‘Siri Fish Farm.’
Anasema ushirka huo una mabwawa ya samaki zaidi ya 10 yenye uwezo wa kufuga samaki 10,000 wa aina mbalimbali. Anataja baadhi yao kwa majina; Kamba, ‘Milk Fish’ na Mangroof, wote ni wanaokuwa baharini.
Anasema mabwawa ya samaki wanayaunganisha na bahari ya Pujini, ila wameweka uzio kuzuia samaki wanaowafuga wasiliwe na wengine baharini.
“Naishukuru Wizara ya Uvuvi, pamoja na serikali kuu imekuwa ikitusaidia sana katika shughuli hii ya ufugaji samaki, kwa kunipa ushirikiano mzuri wa kuendeleza ufugaji huu,” anasema Abdallah.
MATARAJIO MAKUBWA
Anasema alipoanza biashara hiyo, hakutarajia kuwa na tija ya kiwango alichofikia na sasa anapata faida, kwani huvuna samaki tani mbili hadi tatu anaowauza na kumpatia pato la Sh. milioni nane.
Mfugaji huyo anasema ana uwezo wa kuzalisha zaidi ya tani 100 kila baada ya miezi sita, iwapo atakuwa na vifaranga vya samaki wa uhakika na wa kutosha, lakini kwa bahati mbaya kuna upungufu.
“Soko la samaki ni zuri sana, maana samaki wengi huwa wanahitajika, lakini kutokana na uhaba wa upatikanaji wa vifaranga, tunashindwa kulifikia soko hilo,” anasema.
Abdalllah anasema biashara hiyo ya samaki kwa sasa ni mkombozi wa maisha yake yenye watoto wanane, kwa kumpatia huduma zote muhimu.
WANUNUA MASHINE
Anasema ushirika wao wa samaki, hivi sasa umenunua mashine ya uzalishaji wa chakula cha samaki na sasa watakuwa na uwezo wa kuzalisha chakula cha samaki.
“Licha ya mashine hiyo ambayo itatuwezesha kuzalisha chakula cha samaki, pia chakula kingine tutawauzia wafugaji wengine wa samaki, hivyo mapato yatazidi kuongezeka.” anasema.
Kwa mujibu wa Abdallah, Ushirika huo wa ufugaji umegeuka sehemu ya kujifunza kwa watu mbalimbali wanaotaka kupata elimu kuhusu samaki.
Anataja matarajio ya baadaye, ni ushirika huo kuwa na mpango wa kumiliki kiwanda cha kusindika samaki.
Pia anasema hivi sasa wana lengo la kufuga aina zingine za samaki kama Changu, Kolekole na Pono na ombi lake kwa serikali, ni iwasaidie kuwapatia vifaranga vya samaki, ili kuboresha biashara yao na wanufaika wengine.
UFUGAJI WA MAONYESHO
Mfugaji wa samaki Kijiji cha Jozani mkoa wa Kusini Unguja - Mohammed Salum Haji, anasema ufugaji wake wa samaki ni kwa ajili ya maonyesho kwa watalii na sio kuuza kama anavyofanya Abdallah na wengine.
Anasema watalii wanaofika huangalia samaki na kupewa maelezo ya kila wanachotaka kujua, kwa malipo ya Dola 10 au sawa na Sh. 21,850 na kipato chake cha miezi sita ni Sh. milioni moja na nusu.
“Biashara hii sio ya peke yangu. Ni ushirika ambao fedha tunayoipata huwa tunagawana kila baada ya miezi sita na fedha zingine, tunaimarisha mradi wetu,” anasema.
Kama walivyo watangulizi wake, anataja changamoto kubwa mbele yake ni upatikanaji vifaranga katika kutimiza azma ya kupanua uzalishaji samaki.
Haji ambaye naye ni mnufaika aliyekwenda kusoma China, anasema kuwa elimu hiyo imemsaidia kuimarisha shughuli hiyo ya ufugaji samaki na kugeuka kivutio kikubwa kwa watalii.
Ushauri wake ni kwamba, vijana wasio na ajira wanaweza kutafuta njia mbadala za kujiajiri kupitia ufugaji.
MIKAKATI YA SMZ
Wizara ya Kilimo, Maliasili, Uvuvi na Mifugo ya SMZ tayari imeingia mkataba na wadau wa maendeleo, kutekeleza mradi wa miaka mitatu wenye thamani ya Dola milioni 3.2. (Sh.bilioni saba), ikilenga kusaidia ufugaji samaki, hasa katika uzalishaji wa vifaranga.
Wadau wanaofadhili mradi huo ni asasi ya Korea International Cooperation Agency (KOICA) na utatekelezwa na Shirika la Umoja wa Mataifa la Chakula na Kilimo (FAO),kwa ajili ya kuboresha ufugaji samaki na upatikanaji wa chakula bora
“Kuanzishwa kwa mradi huu hapa Zanzibar, kutasaidia kuzalisha samaki wadogo (vifaranga), ili kusaidia maisha ya kundi kubwa la wakazi wa vijijini, hasa wanawake na vijana wasiokuwa na ajira,” anasema Waziri wa Kilimo, Maliasili,Uvuvi na Mifugo, Hamad Rashid Mohammed,
Anasema SMZ imejipanga kubadilisha mfumo wa kilimo na uvuvi, ili kuingia katika mfumo wa kisasa na bora zaidi.
Hamad anaeleza dhamira ya wizara yake katika kuwawezesha wafuga samaki kupata vifaranga bora vya samaki.
“Mradi huu ni wa uzalishaji wa vifaranga vya samaki ambao ni mradi wa muda wa miaka mitatu. Sasa tunataka kuingia katika uvuvi wa kufuga, badala ya kuvua, kwa sababu maji ya karibu baharini huwezi kupata samaki, kutokana na wavuvi kutumia mabomu nadawa mbalimbali na kuua vizalia vya samaki”.
Hamad anasema hali hiyo imewafanya samaki wahamie katikati kwenye kina kirefu ambako hawasumbuliwi.
Anasema mradi huo utasaidia kuandaa soko la samaki ndani na nje ya nchi, ili bidhaa nyingi za bahari ziweze kuzalishwa na wananchi wafuge na kupata samaki wengi, ili pato la taifa liongezeke.
Zanzibar ina vikundi 144 vya ufugaji samaki na hadi sasa wananchi wakazi wengi wa Pemba wamehamasika zaidi ikilinganishwa na Unguja.










