Wajasiriamali wataja vikwazo vinavyokwamisha biashara

11Mar 2016
Christina Mwakangale
Dar
Nipashe
Wajasiriamali wataja vikwazo vinavyokwamisha biashara

KATIKA kundi la Watanzania milioni 22 waliopo katika sekta isiyo rasmi, wanawake wakiwa miongoni mwao hawajaachwa nyuma katika shughuli mbalimbali za kiuchumi.

Mke wa Rais wa Zanzibar, Mama Mwanamwema Shein, akitembelea mabanda ya maonesho ya wanawake wajasiriamali. PICHA NA MTANDAO

Wanawake wajasiriamali ni tegemeo kubwa kwa familia nyingi nchini kutokana na mchango mkubwa wanaoutoa katika kuhudumia familia hasa chakula na matibabu.

Takwimu za uchumi duniani zinaonyesha sekta ya ujasiriamali inaendelea kukua duniani na kutoa mchango mkubwa na kuongeza ajira.

Takwimu za Shirika la Kazi Duniani (ILO), za mwaka 2010 zinasema asilimia 80 ya Watanzania wapo katika sekta hiyo.
Hapa nchini karibu nusu ya wajasiriamali wote yaani asilimia 43 ni wanawake.

Wanawake hawa ni wale waliojikita katika kujipatia kipato kupitia kilimo, ujasiriamali pamoja na kufanya biashara ndogondogo kama vile upishi maarufu mama lishe, ushonaji, ususi, ufugaji, uvuvi, usindikaji na nyinginezo.

Biashara hizo zinawapatia kipato kina mama hawa na kuimarisha hali ya kiuchumi kwa familia zao, pamoja na kuupiga kikumbo umaskini.
Maonyesho ya bidhaa za wajasiriamali wa kati, wadogo na wafanyabiashara wa ndani yaliyoanza Februari 24 hadi 27 mwaka huu, jijini Dar es Salaam yalilenga kuwakutanisha wazalishaji wa viwandani, wafanyabiashara, taasisi za serikali na sekta binafsi, kutambua mchango wao katika viwango kibiashara ndani na nje ya nchi.

Maonyesho ya mwaka huu yaliyokuwa na kaulimbiu 'Mchango wa Viwango katika kumwendeleza Mwanamke', yalilenga kutambua ubora na viwango wa bidhaa zinazoandaliwa, kuzalishwa, kutengenezwa na kusindikwa na wanawake.

Pia, maonyesho hayo ilikuwa ni fursa pekee kwa kampuni zilizoshiriki kutangaza bidhaa zao na kukuza soko kupitia utambulisho wa 'Made in Tanzania'.

CHANGAMOTO
Sylvia Dotto, mmoja wa washiriki katika maonyesho ambaye ni mjasiriamali mdogo mkazi wa jijini Mwanza, anayeandaa na kufungasha katika mifuko ya kisasa dagaa wa Ziwa Victoria, anaeleza changamoto zinazomkabili katika biashara hiyo.

Anasema pamoja na maonyesho hayo kumpa fursa ya kujitangaza zaidi, upatikanaji wa mkopo kutoka taasisi za kifedha, ili kukuza biashara ni changamoto kubwa inayokwamisha wajasiriamali wengi.

Anasema pia kuwa mfumo wa upatikanaji wa leseni, vibali ulio katika ofisi tofauti katika taasisi na mamlaka za serikali, unachangia baadhi ya wajasiriamali kutotimiza vigezo na kanuni za kibiashara kutokana na usumbufu wanaopata wakati wa kufuatilia kutimiza matakwa hayo ya kisheria.

“Kwa mfano ofisi ya kupatia leseni TRA ama TBS, TFDA na benki kwenda kulipia, zipo maeneo tofauti na mbali, lakini huduma hizi zingepatikana katika eneo moja, ingeondoa usumbufu,” anasema Dotto.

Pia anasema ukosefu wa mkopo unasababisha kushindwa kununua vifaa vya kisasa vya kusindikia bidhaa, kisha kuwafanya kutumia usindikaji wa kawaida ambao unakumbana na ushindani sokoni.

Anasema vikwazo hivyo vikiondolewa, biashara za wajasiriamali nchini zitamudu ushindani sokoni na kukuza kipato chao na pato la Taifa.

SERIKALI IFANYE NINI?
Mkurugenzi Mtendaji wa Taasisi ya Sekta Binafsi Tanzania (TPSF), Godfrey Simbeye, anasema serikali iweke sera ya kulinda viwanda, wazalishaji, wajasiriamali wa kati na wadogo pamoja na wakulima wa ndani.

"Serikali ije na Sera ya kulinda wajasiriamali, wakulima, wenye viwanda kwani wanapata ushindani mkubwa kutokana na bidhaa zinazoingia nchini, zisizo na viwango, ubora, huku zikiuzwa kwa bei ya chini," anaeleza Simbeye.

Simbeye anasema baada ya soko la ndani kulindwa, kuwe na uhamasishaji kwa Watanzania kununua na kutumia bidhaa zinazozalishwa nchini na mkazo uwekwe kwa wazalishaji kuzingatia ubora.

“Uhamasishaji wa kununua bidhaa bora nchini ni mchakato endelevu wa kukuza viwanda vyetu, kutengeneza ajira, kuongeza kipato na kuleta amaendeleo,” anasema.

WAJIBU WA WAJASIRIAMALI

Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Viwango Tanzania (TBS), Joseph Masikitiko, aliwataka wazalishaji, wajasiriamali wa kati na wakubwa kupeleka bidhaa zao katika shirika hilo, ili bidhaa zao ziweze kukaguliwa na kuthibitishwa ubora wake na kisha kupatiwa nembo ya ubora.

Anasema ili kufungua milango ya kibiashara katika soko la ndani na nje ya nchi, viwango vya ubora wa bidhaa kwa mtumiaji ni muhimu.

Masikitiko anaeleza kwamba, wajasiriamali wachache nchini ndio waliozisajili bidhaa zao na kuwafanya ambao hawajazitambulisha bidhaa zao katika mfumo huo, kutokuwa na uhakika wa soko.

"Wajasiamali ni wengi nchini, lakini bado hawajazileta bidhaa zao TBS ili tuweze kuthitisha viwango, ubora na kupanua wigo wa soko lao la ndani na nje ya nchi," anasema Masikitiko.

Pamoja na ushauri wa TBS, Katibu Mkuu wa Wizara ya Viwanda, Biashara na Uwekezaji, Prof. Adolf Mkenda, anasema kuwa serikali itaendelea kuboresha mazingira ya ujasiriamali nchini ili kuwasaidia kukuza vipato vyao na uchumi wa taifa.

Prof. Mkenda anayasema hayo wakati akifunga maonyesho hayo jijini Dar es Salaam, baada ya kutembelea vibanda vya wajasiriamali na wazalishaji bidhaa yaliyoandaliwa na TBS na TPSF.

Anasema serikali ya awamu ya tano imedhamiria kukuza viwanda nchini ili kufikia uchumi wa kati, hivyo uzalishaji wa bidhaa bora zilizo na viwango unahitajika.

"Miundombinu wezeshi ni muhimu, TBS iimarishe kazi zake kwa kutumia weledi, ufanisi na kutoa maamuzi bila woga katika kuhakikisha bidhaa hafifu haziingii nchini na kuua soko la ndani," anasema Prof. Mkenda.

TUZO KWA WAJASIRIAMALI
Ili kukuza soko na matumizi ya bidhaa za ndani, tuzo za huduma na bidhaa 50 bora zinazozalishwa nchini zitapata fursa ya kupatiwa tuzo.

Mchakato huo umeanza sasa na inaelezwa kuwa hadi Juni mwaka huu, bidhaa zitachaguliwa na kupata fursa ya kushiriki tuzo za ubora za Jumuiya ya Maendeleo ya Nchi za Kusini mwa Afrika (SADC).

Tuzo hizo zitatolewa katika mkutano wa Baraza Kuu la Shirika la Viwango Afrika (ARSO), utakaofanyika Juni mwaka huu, jijini Arusha.

Mkutano huo utajumuisha nchi 37 za Afrika na kampuni za bidhaa zitakazoshiriki katika mashindano ya ubora ya mabara, nchini Misri baadaye mwaka huu.