Wagombea CUF Zanzibar wanapolazimishwa kunywa maji ya mtoni

17Feb 2016
Rahma Suleiman
Zanzibar
Nipashe
Wagombea CUF Zanzibar wanapolazimishwa kunywa maji ya mtoni

CHAMA cha wananchi (CUF) kimepaza sauti na kutakawagombea wake wafutwe kwenye kumbukumbu za Tume ya Uchaguzi (Zec), ikiwamo kuondoa picha za wagombea wao kwenye karatasi za kupigia kura.

Naibu Katibu Mkuu wa Chama cha Wananchi (CUF) upande wa Zanzibar, Nassor Ahmed Mazrui.

Hata hivyo, Zec imesema inaendelea na utaratibu wake kama kawaida na kwamba uchaguzi wa marudio utafanyika mwezi Machi 20, na kwamba hakiwezi kufanya mabadiliko yoyote ikiwamo kuondoa picha za wagombea.

Kitendo hicho kinalalamikiwa na Naibu Katibu Mkuu wa CUF, Zasnzibar, Nassor Ahmed Mazrui kwa madai kwamba hiyo siyo demokrasia ya kweli katika nchi ambayo inatawaliwa kwa utawala wa sheria.

Mazrui anasema wao kama chama hawatatambua uchaguzi wa marudio wa Zanzibar uliopangwa kufanyika mwezi machi 20 mwaka huu namatokeo yake yatakayotangazwa na Tume ya Uchaguzi ya Zanzibar (ZEC).

Anasema ni kitendo cha aibu na dheheha ZEC kung'ang'ania kuweka picha za wagombea wa CUF katika karatasi za kupigia kura licha ya kutangaza kujitoa.

CUF kinasema uchaguzi huo wa marudio ni haramu hivyo hata matokeo yake yatakuwa hivyo hivyo.
Hadi sasa wagombea 54 wa CUF wa Udiwan, Uwakilishi na Urais kila mmoja ameshapeleka barua ZEC kujiondoa katika uchaguzi wa marudio lakini pia chama kimeshapeleka barua kuhusu wagombea wake kujitoa katika uchaguzi huo.

Kinachotaka kufanywa na ZEC kinafanana na kile kilichofanywa na NEC, mwaka jana kwenye Uchaguzi Mkuu katika jimbo la Segerea jijini Dar es Salaam, baada ya tume hiyo kurudisha jina na picha ya mgombea wa ubunge kupitia (Chadema) licha ya kuandika barua ya kujitoa.

HATIMA YA SERIKALI YA UMOJA WA KITAIFA (SUK)
Akizungumzia hatima ya SUK , Mazrui anasema Wazanzibari ndiyo wenye maamuzi ya kutaka kuendelea au kutoendelea kwa serikali hiyo.

Mazrui anasema ili kuleta usawa wa kidemokrasia ni lazima serikali ya CCM ikubali kukabidhi nchi kwa upinzani kama wataonekana wameshinda uchaguzi badala ya kuzua visingizio vingi ili kupata sababu ya kufuta uchaguzi kama kilivyofanya kwa sasa.

Anasema katika uchaguzi wa Zanzibar wenye mamauzi ni Wazanzibar wenyewe na haitakiwi chombo fulani kikatengeneza nguvu ya kuzima ndoto zao.

Mwanasiasa huyo anasema anawashangaa viongozi wa kitaifa wa CCM ambao hawataki kuona Zanzibar inaongozwa na upinzani na kwamba hatua hiyo ni mbaya kwa taifa.

Ushauri wake kwa wananchi wa Zanzibar ni kuwataka wakae kimya na waendelee na shughuli zao kwa kuwa hawataki suala la uchaguzi linaharibu maisha yao.

MAZOMBI NI NANI ZANZIBAR
Kuhusu kikundi cha watu wanaopiga watu kijulikanchoa kama Mazombi, Mazrui anasema hao ni Askari wa Jeshi la Polisi ndiyo wanaofanya kazi hiyo na wala siyo raia wa kawaida.

“Nilihudhuria kikao cha Polisi kilichotukutanisha viongozi wa vyama vya siasa, Kamishna wa Polisi na Maafisa wa Jeshi na nilipata nafasi ya kuwauliza swali na nikajibiwa kuwa hao Mazombi ni askari maalum," anasema
Anasema anashangazwa kuona serikali na jeshi la polisi sasa wanakana kutotambua Mazombi ambao wanapiga watu bila ya hatia yoyote.

“Mazombi tunawaona wanaongozwa na gari za vikosi vya serikali tena wakiwa na silaha wala huwaoni Mazombi wakitembea na gari yangu Mazombi wanatembea na gari za serikali,” alisema.

AMSHANGAA RAIS MAGUFULI.
Anasema anamshangaa rais John Magufuli kwa kutangaza kujitoa sakata la Zanzibar na kushindwa kutotatua mgogoro huo.

Kauli ya Rais Magufuli wiki iliyopita ya kutoingilia masuala ya ZEC na ile aliyoitoa wakati akifunguwa Bunge la 11 la kwamba atashughulikia mgogoro wa kisiasa Zanzibar.

“Kauli zake zimekuwa zikipishana kama ardhi na mbingu na wala sisi hatukutaka aingilie kati mgogoro wa Zanzibar, bali alitamka mwenyewe kuwa atalishughulikia suala la Zanzibar ndiyo maana na sisi tukataka kauli yake aitekeleze kwa vitendo,” alisema.

Anaongeza kuwa Magufuli ameonesha wazi kuwa yeye ni mtawala wa Zanzibar na Zanzibar ni koloni la Tanganyika na Muungano wa Tanganyika na Zanzibar unakandamizwa kidemokrasia.

Mwanasiasa huyo anamshangaa Magufuli kumtuma Waziri wa Mambo ya nje wa Tanzania, Balozi Augustino Mahiga kwenda Burundi kushughulikia matatizo ya nchi hiyo lakini upande wa Zanzibar anasema hilo hawezi kuliingilia.

“Burundi imekuhusu nini wewe Magufuli, na kuiacha Zanzibar ambayo ni sehemu ya nchi yako," anasema
MWISHO