Ni kipindi ambacho wananchi ambao ni wapigakura hukusanyika katika mikutano ya hadara kusikiliza sera za kila mmoja.
Kupitia sera na ahadi hizo ndipo wanbanchi hupata furasa ya kufanya uamuzi ni mgombea yupi anafaa kuwaongoza.
Mbunge wa Busega (CCM), Dk. Raphael Chegeni anasema ili mwanasiasa aendelee kuungwa mkono na wananchi ni lazima atimize wajibu wake ipasavyo
Anaeleza kuwa siri ambayo itamfanya Mbunge kurudi bungeni bila vikwazo vyovyote ni kuhakikisha anawatumikia wananchi hususani kuhakikisha anatatua kero muhimu.
Dk. Chegeni anasema wananchi kwa sasa uelewa wa wananchi kuhusu masuala ya siasa ni mkubwa na kwamba kama Mbunge atafanya tofauati na alivyoahidi atapata wakati mgumu katika uchaguzi utakaofuata.
''Kipimo cha kurudi bungeni kipo kwa wananchi unajua wabunge wengi wanajisahau hasa wakishapata madaraka,” anasema Dk. Chegeni
Dk. Chegeni anasema uchaguzi ni uchaguzi hivyo ushindani ni sehemu ya changamoto.
Anasema kumshinda mtu kwenye kiti alichokikalia kwa miaka mitano siyo jambo rahisi, lakini siku hizi wapiga kura wana uelewa mkubwa.
“Kwa hilo hakuna longo longo, ukipewa nafasi ukawafanyia kazi daima watakuchagua, lakini usipofanya nao hawatakuchagua hata ukisema utumie hela hapo ndiyo unazidi kujimaliza, kwani wananchi wana uelewa mkubwa ikilinganishwa na zamani,” anasema Dk. Chegeni
Jimbo la Busega ni miongoni mwa majimbo yaliyokuwa na utata hatua ambayo ilikifanya Chama Cha Mapinduzi (CCM) , kuagiza kura za maoni ndani ya chama hicho zirudiwe.
Dk. Chegeni anakiri kwamba kupitia uchaguzi wa mwaka jana amejifunza kuwa ili uwe mwanasiasa imara unahitaji kufahamu wajibu wako na ujue haki zako za kisiasa ndani ya chama.
Anasema Chegeni ambaye alikuwa Mbunge mwaka 2005 kabla ya kudondoshwa mwaka 2010 na Dk. Titus Kamani anasema alivyoshindwa 2010 kwake ilikuwa changamoto.
''Uchaguzi ni uchaguzi na matokeo ni sehemu ya siasa hivyo nilikubali matokeo na nikajipanga kwa uchaguzi mwingine'', anasema
Akizungumzia Bunge la mwaka 2005 na hili la sasa Dk. Chegeni anasema, kila Bunge linakuwa na utofauti.
Anasema asilimia 32 ya wabunge wa mwaka 2005 ndiyo waliorudi huku asilimia 68 wakibwagwa na wakiwamo wale ambao hawakutaka kugombea kutokana na kuangalia upepo wa kisiasa.
Kuhusu madi ya baadhi ya wadau kwamba nidhamu ya Bunge imeshuka, Dk. Chegeni anasema, inatokana na wabunge wengi kutojua nafasi zao pamoja na majukumu yao.
“Lakini nina imani kadri muda utakapokwenda wengi watajua na kuelewa kuwa nafasi ya ubunge ni dhamana kubwa ya wananchi kwao,” anasema
Dk. Chegeni ambaye pia ni Mwenyekiti wa Jumuiya ya Mabunge ya Madola, anasema changamoto zilizopo jimboni kwake ni pamoja na ukosefu wa maji safi na salama, miundo mbinu ya barabara na matatizo ya wavuvi.
Anasema kuwa wavuvi hawana vitendea kazi sahihi kwa ajili ya shughuli zao na hivyo kujikuta wakifanyakazi katika mazingira magumu.
Dk. Chegeni anasema chanagmoto nyingine ni ukosefu wa shule za sekondari na vyuo vya mafunzo stadi za maisha.
“Tumejipanga kuzitatua kwa kuweka mikakati kwa kushirikiana na wilaya na tayari nimeanzisha programu ya kutafuta ufumbuzi wa masuala hayo.
''Tutashirikisha serikali na wadau wote ndani na nje ya nchi katika kufanikisha hili,” anasema
Mwaka jana jimbo hilo liligombewa na wana CCM wengi akiwamo aliyekuwa Waziri wa Maendeleo ya Mifugo na Uvuvi, katika serikali ya awamu ya nne, Dk. Titus Kamani.










