Wafugaji hapa ndipo ilipo nyama bora, ukuaji kasi mifugo na gharama

02Aug 2023
Beatrice Philemon
DAR ES SALAAM
Nipashe
Wafugaji hapa ndipo ilipo nyama bora, ukuaji kasi mifugo na gharama
  • nafuu

UNAPOZUNGUMZIA malisho ya mifugo aina ya ‘Cenchrus ciliaris’ (jina la kitaalamu), unachoweza kusema ni hiki. Ndilo suluhisho la mfugaji kuachana na kusota kutafuta majani na kutumia gharama kubwa kulisha wanyama.

 

Watu wengi wamekuwa wakitegemea kuwalisha wanyama wao pumba, mashudu ya alizeti na pamba au uduvi na soya kwa kuku, bata na jamii ya ndege ili kuwaongezea protini.

Lakini ujio wa Cenchrus ilirahisisha hasa kwa wafuga  ng’ombe, farasi, kondoo na  mbuzi gharama zimepungua kwa sababu malisho hayo yanatumia gharama kiduchu na kuongeza uzalishaji wa maziwa na nyama  kwa muda mfupi.

Ni aina ya majani  au malisho ya mifugo ambayo  yametafitiwa kisayansi na kubainika kuwa ni bora na yana virutubisho vingi muhimu  kwa  ng’ombe, mbuzi, kondoo, punda na  farasi.

Ofisa Mtafiti Mifugo kutoka Taasisi ya Utafiti wa Mifugo Nchini (TALIRI), Jovith Kajuna, anasema  hayo jijini Dar es Salaam, anapozungumza na Nipashe, hivi karibuni.

Anasema  kuwa  majani hayo  yanaota na kustawi katika maeneo mengi yenye mvua nyingi, au ya wastani na nyanda kame hapa.

Jovith anazungumzia  umuhimu wa malisho haya kwa mifugo akisema  yana virutubisho vingi muhimu vinavyoongeza uzalishaji maziwa kwenye ng’ombe na mbuzi, kondoo na ukuaji wa haraka na bora wa mifugo pamoja na kuboresha ladha na ubora wa  nyama.

“ Si hayo tu, pia kwa mfanyabiashara na mfugaji, malisho haya yana faida nyingi yanapokuwa yameyastawishwa  katika shamba  kwa sababu yana uwezo wa kuendelea kutoa mazao ya mbegu na nyasi kwa ajili ya kutengeneza malisho ya ‘hei’.”

Mtafiti huyo anaeleza kuwa hei au silages ni aina ya malisho makavu yaliyohifadhiwa ambayo yanaweza kukaa kwa muda wa miaka 10-15 kabla ya kupanda upya shambani.

“Ukifanya ulinganifu wa gharama za uzalishaji wa  malisho aina ya Cenchrus ciliaris na mkulima aliyepanda mahindi shambani au mpunga , utagundua kuwa mkulima aliyepanda mahindi analazimika kila mwaka kuandaa shamba upya, kununua mbegu na kupanda, kupalilia ambavyo  vyote vinamwingiza kwenye gharama zinazojirudia tofauti na aliyepanda malisho aina hii,” anasema Jovith.

Mbali na hilo, malisho haya yanampa mkulima au mfugaji fursa ya kupata faida itokanayo na mbegu ambazo zinauzwa kwa  sasa Shilingi 20,000 kwa kilo katika  taasisi za serikali kama TALIRI na kati ya shilingi 50,000 hadi shilingi 80,000 kwenye maeneo ya watu binafsi.

Lakini pia baada ya kuvuna  mbegu unaweza kuvuna nyasi, ukazikausha na kufunga marobota ya  hei ambazo zinauzwa kati ya Shilingi 3,000 hadi shilingi 5,000 kwenye taasisi za umma au zaidi kwa wauzaji binafsi.

Mtafiti huyo anasema malisho yaliyohifadhiwa hutumika kumsaidia mfugaji kulisha mifugo yake hususani wakati wa kiangazi, au kipindi cha ukame ambapo kuna upungufu  mkubwa wa malisho au majani.

Anasifia uzalishaji wa  malisho aina ya Cenchrus ciliaris kuwa umekuwa ni fursa kubwa  kibiashara ndani na nje ya nchi, kwa sababu huhitajika  na wafugaji wengi  kwa kuwa wengi wamehamasika kufuga kibiashara tofauti na ilivyokuwa hapa zamani.

Aidha,  idadi ya ng’ombe wa wanaofungwa ndani wakiwemo wa maziwa na wa kunenepesha kwa ajili ya nyama nayo imeongezeka.

Kwa upande wa hei ambayo ni majani makavu,  pia masoko ya nje yameongezeka  kwa kasi na kwamba Tanzania haina uwezo mkubwa wa kuzalisha ikilinganishwa na mahitaji ya soko katika mataifa ya  Comoro, Shelisheli na Congo.

Mbali na hilo, Jovith anasema zipo fursa za kununua marobota ya hei katika eneo moja kwenda sehemu nyingine yenye uhitaji kulingana na wafugaji.

“Tunaomba Watanzania watumie fursa hii ya kupanda malisho haya,  wakitaka mafunzo jinsi ya kuyatunza, kuyahudumia, wataalamu kutoka TALIRI wapo tayari kutoa huduma ya kupanda ” anasema mtafiti huyo.

Anasema malisho haya yanawahakikishia kuondoa tatizo la majani kwa mifugo yao na ndiye  mkombozi kiuchumi kwa vile wanaweza kuuza nje na kupata fedha za kigeni.

“Mifugo yao inakuwa na uhakika wa malisho, nyama na maziwa bora na mengi. Ziada wanauza nje , yote hayo yakikuza uchumi na maendeleo ya sekta ya mifugo na kilimo.” Anaongeza,

Ili kusaidia wananchi kujua faida za malisho haya, hivi karibuni TALIRI ilishiriki katika maonyesho ya Sabasaba jijini Dar es Salaam na wataalamu wa taasisi hiyo waliwaelimisha na kuwafunza wananchi kuhusu  uwekezaji huo wenye tija kwenye kilimo cha Cenchrus ciliaris.

UZALISHAJI

Jovith anasema mkulima au mfugaji ambaye yupo tayari kujikita kupanda malisho haya kwa ajili ya biashara na mifugo anatakiwa kufahamu kuwa , hekari moja inatoa kati ya marobota 200 hadi 300 ya malisho hayo lakini pia kutegemea na aina ya udongo.

Halikadhalika anaongeza kuwa maeneo yaliyowekwa mbolea uzalishaji unaweza kufikia marobota 450 kwa hekari moja.