Jihadhari usiwe kati ya 158,000 wanaokufa kila mwaka na dawa feki

02Aug 2023
Na Mwandishi Wetu
DAR ES SALAAM
Nipashe
Jihadhari usiwe kati ya 158,000 wanaokufa kila mwaka na dawa feki
  • *Fahamu namna ya kutambua, kukwepa

BAADA ya kazi za kutwa unahisi kuwa una maumivu ya kichwa. Unachokifanya ni kununua dawa za kutuliza maumivu kutoka kwa muuzaji wa duka lililoko mtaani. Kisha unameza mbili.

 

 

 

Lakini unajuaje iwapo vidonge hivyo ni halisi au ni bandia? Muuzaji siyo mtaalamu na kama ni duka halisi la dawa lililothibitishwa na mamlaka za uhakiki?

Hofu ya dawa feki ni tatizo kubwa Afrika na matokeo yake iwapo mtu atameza dawa zisizo na ufanisi ni kusababisha vifo.

 

Ni hatari kuwa kati ya vifo 64,000 na 158,000 vinavyohusishwa na ugonjwa wa malaria kila mwaka katika eneo la Kusini mwa Jangwa la Sahara na Tanzania ikiwepo, ni matokeo ya kutumia dawa feki.

Wagonjwa wanapewa dawa ambazo hazitafanya kazi mwilini au hazijatengenezwa kikamilifu kutibu ugonjwa husika ni hatari. Mambo hayaishii hapo zaidi ya watoto 250,000 duniani kote hufa kutokana na dawa feki kila mwaka.

 

Kwa mwaka uliopita pekee zaidi ya watoto 300 walikufa baada ya kutumia dawa feki za kikohozi au za kutuliza maumivu.

 

Lakini, hebu fikiria unanunua dawa hakuna kifungashio kinachoonyesha maelezo ya dawa na viwango au vipimo vya kutumia. Je, itakuwaje ikiwa umejaribu kutibu kichwa chako kwa kutumia dawa feki au bandia? Kama ripoti zinavyoeleza hakuna kupona matokea yake ni kifo.

Neno "bandia" humaanisha dawa ambazo zimeghushiwa kimakusudi na kwa ulaghai. Pia huitwa dawa zilizo chini ya kiwango au zilizoghushiwa, ni dawa ambazo ziko chini ya vipimo na viwango vya ubora ambavyo vimeidhinishwa na mamlaka za udhibiti wa dawa kitaifa na kimataifa.

Usizichanganye na dawa za asili  hizo ni za bei nafuu, lakini zimethibitishwa kisayansi kuwa ni salama na zenye ufanisi na zina hati miliki.

 

Dawa feki au bandia zinazojulikana zaidi huwa ni dawa maarufu zaidi zikiwamo za kutuliza maumivu, za kutibu maambukizi mfano ‘antibiotic’ zipo za malaria, za kupunguza makali ya virusi vya UKIMWI VVU ambazo ni ARVs, kuna nyingine zinazoelezwa kuwa huongeza nguvu za kiume maarufu kama Viagra, kadhalika kuna za  kupunguza uzito.

 

Dawa bandia, feki au za kughushi ni tatizo kubwa katika nchi nyingi za Afrika. Utafiti umeonyesha kuwa mataifa mengi yanayoendelea yana kiwango kikubwa cha dawa zisizo na viwango wala ubora

Kwa mfano, hadi asilimia 88.4 ya dawa za malaria katika baadhi ya masoko ya Afrika zimeripotiwa kuwa ni bandia.

 

KUKABILIANA NAZO

Juhudi za kukabiliana nazo ni pamoja na kuimarisha ufuatiliaji wa serikali kuhusu dawa bandia. Kwa mfano, katika nchi nyingi za Kiafrika wafamasia wanapewa mafunzo ya kujenga uelewa wa dawa hizo na uwezekano wa kupenyezwa kwa dawa hizo katika mnyororo wa usambazaji.

 Hii itawafanya wajiandae vyema kugundua dawa feki na kubadilishana taarifa na wagonjwa wao.

Hata hivyo, kuelimisha watumiaji wa mwisho wa dawa hawa ni wagonjwa,  ni nguzo muhimu zaidi ya matumizi ya dawa salama.

Wagonjwa lazima wajue jinsi ya kukagua dawa kwa macho kwa kuangalia tarehe ya mwisho wa matumizi na alama zingine za utambulisho. Kuweza kutofautisha kati ya dawa bora na zile bandia kunaweza kuleta tofauti kati ya uhai na kifo. Zipo hatua tatu za kuchukua ili kubaini dawa bandia.

DUKA RASMI

Kumbuka kununua dawa katika maduka yaliyosajiliwa, iwe maduka ya rejareja yaliyo na leseni na kwenye zahanati.

 

Hawa wanapaswa kubandika leseni zao kwenye kuta zao na unaweza kusoma kujiridhisha.Wafamasia na wasaidizi wao wamefunzwa jinsi ya kushughulikia dawa. Wanawajibika kisheria na kimaadili kwa dawa zilizo chini ya udhibiti wao. Hii inamaanisha kuwa watapata bidhaa kupitia njia rasmi za dawa ambazo kuna uwezekano mdogo wa feki kupenyezwa.

 

EPUKA MTANDAOUsinunue dawa kutoka kwa maduka ya mitandaoni. Katika nchi nyingi za Kiafrika, hakuna maduka ya dawa halali mtandaoni, mengi yanaelezwa ni feki.

 

KAGUA KWANZAIkague na kuihakiki dawa yako, hakikisha kukagua na kusoma kifungashio cha dawa.

Inapaswa kuwekewa lebo ya jina la bidhaa, maelezo ya mtengenezaji kama vile jina lao na anuwani ya mahali na tarehe ya mwisho wa matumizi.

 

Inapowezekana, angalia nambari ya kundi hii ni 'serial number' au msimbomilia au namba mistari ‘barcode’   ambayo inaweza kutumika kufuatilia ni lini na wapi bidhaa ilitengenezwa.

 

Ikiwa ni dawa ulizowahi kutumia hapo awali, jaribu kuilinganisha na vifungashio vyote viwili,

 

Piga picha yake ikiwa unaitumia mara kwa mara kwa kulinganisha katika siku zijazo na hakikisha dawa imefungwa vizuri na iko sawa,

fungua kifurushi na uhakikishe.

 

Vidonge kwenye pakti, kwa mfano ni lazima kuhakikisha kwamba hakuna aliyejaribu kuvifungua na pia vidonge hivyo chunguza na  hakikisha kwamba vinafanana bila kubadilika rangi, visiwe na madoadoa au ngozi yake isionekane yenye rangi tofauti, pia visiwe vimepasuka au kuwa na ukungu.

 

Baadhi ya mabaki ya poda katika vidonge yanakubalika, lakini haipaswi kuwa mabaki ama poda nyingi zaidi.

 Hii inaweza kumaanisha kuwa vidonge havijabanwa vizuri, lakini pia haipaswi kuwa na harufu. Vidonge vinapaswa kung'aa na siyo kukutwa vimepasuka, kunata au kukunjamana.

 

UKIBAINI FEKI

Ikibaini kuwa dawa yako ni feki, haina ubora au ni bandia, unapaswa kuripoti mara moja kwenye taasisi za udhibiti wa dawa au mdhibiti wa kitaifa wa dawa. Kila nchi barani Afrika ina mamlaka ya kitaifa ya kudhibiti dawa kama mamlaka huru au ndani ya wizara ya afya.

Ni vizuri pia kama umeitumia kusema athari ulizozipata hospitalini kwa wataalamu wa afya,

BBC