Waelimishaji wa masuala ya kujamiiana wapambana kuvunja miiko

09Feb 2016
Nipashe
Waelimishaji wa masuala ya kujamiiana wapambana kuvunja miiko

MWANDISHI wa habari wa Liberia, Mae Azango, anasema alitumia mwaka mzima akiishi "kama panya, akipita mti mmoja hadi mwingine" akiwa na binti yake ili kuepukana na wanadini wenye msimamo mkali waliotishia kumuua kutokana na kutangaza masuala ya tohara kwa wanawake nchini mwake mwaka jana.

Yeye ni mwandishi mwandamizi katika gazeti la nchini humo la FrontPage Africa, Azango aliiambia IPS kuwa pamoja na kwamba serikali ya Liberia ilitia saini mkataba mwaka 2012 unaoahidi wananchi wake haki ya habari, inaendelea kushikilia takwimu za haki ya kujamiiana na uzazi kwa waandishi wa habari.

"Kwa kila habari ninayoandika, nahatarisha maisha yangu," anasema, akiongeza kuwa anategemea kwa kiasi kikubwa taarifa "za vyanzo vya siri" kutoka serikalini kukusanya taarifa, kwani ni habari chache mno zinasambazwa kwa umma.

Matatizo yake yanaungwa mkono na wanawake wengi na wataalam wa afya waliokusanyika katika mji mkuu wa Malaysia, Kuala Lumpur kwa ajili ya jukwaa la tatu la kila mwaka la Women Deliver hivi karibuni.

Wakitoka pande zote za dunia, washiriki wa mkutano huo hawana shida na kubainisha malengo: na wameweza kuvunja miiko inayozunguka elimu ya kujamiiana na kujenga mazingira salama ya utetezi, wasomi wa masuala ya afya na waelimishaji kusambaza elimu ya ngono salama na uzazi wa mpango.

Nchini Morocco, nchi yenye jumla ya wakazi milioni 32, shule zimepiga marufuku utoaji elimu ya kujamiiana kwa vijana kwa sababu wabunge wana imani kuwa ni "dhana ya kishetani, iliyobuniwa kukuza uasherati," mtetezi wa afya ya kujamiiana na ya uzazi, Amina Lemrini, aliiambia IPS.

Anasema mafanikio ya kuboresha huduma za afya ya uzazi nchini mwake yamekuja polepole mno kutokana na miiko iliyoanzishwa na viongozi wa kidini.

Huku serikali ikishindwa kuwakosoa viongozi wa dini, kazi ya kusambaza huduma muhimu za afya inaangukia kwa kiasi kikubwa kwa mashirika ya kijamii, ambayo jitihada zao zinatishiwa.

Lemrini anasema hatambui mwanaharakati hata mmoja wa haki za uzazi ambaye hajatishiwa maisha. Hata hivyo serikali haiwapatii ulinzi wowote ule.

Matatizo yao yametambuliwa na wataalam wakongwe katika nyanja ya afya ya uzazi, ikiwa ni pamoja na mkurugenzi mtendaji wa Shirika la Idadi ya Watu la Umoja wa Mataifa (UNFPA), aliyeiambia IPS kuwa imani kali za kidini ni "jambo linalotia wasiwasi" linapokuja suala la kuendeleza afya ya kujamiiana.

Hata hivyo, bado anawataka wanaharakati kuendelea kufanya kazi zao, akiongeza kuwa, "Imani kali zinaendelea katika jamii na dini zote – jambo la msingi ni jinsi gani tunaweza kuwasilisha ujumbe."

Ana imani kuwa kama watu wengi zaidi wanatambua haki na chaguo lao, hawatasita kukataa sheria za kishamba na kile kinachojulikana kama "miiko ya kitamaduni."

"Mtu wa kawaida mtaani hataki hali ambapo kifo kinaita kila wakati kutokana na sababu kwamba hakiwezi kuzuiliwa," alisisitiza.

Hata kwa kuangalia kwa haraka takwimu za kimataifa inatosha kutoa msimamo wenye nguvu wa kuwasiliana vizuri: kwa mujibu wa UNFPA, karibu wanawake 800 wanakufa kila siku kutokana na matatizo yanayohusiana na mimba; kwa mwaka, idadi hiyo inafikia 350,000, ambapo kati ya vifo hivyo, asilimia 99 vinatokea katika nchi zinazoendelea.

Utoaji wa mimba usiokuwa wa kitaalam na kutelekezwa kwa watoto wa kike wadogo wanaojifungua kumesababisha wastani wa vifo milioni 134 duniani kote.

Ikikusanya takwimu duniani kote, UNFPA inakadiria kuwa "mamilioni ya watoto wa kike" wanafanya ngono isiyokuwa salama na wanakosa taarifa za uzazi wa mpango.

Osotimehin hivi karibuni aliandika kuwa "mahitaji yasiyofikiwa ya uzazi wa mpango ni miongoni mwa asilimia 33 ya watoto wa kike kati ya miaka 15 na 19 nchini Ethiopia, asilimia 38 nchini Bolivia, asilimia 42 nchini Nepal, asilimia 52 nchini Haiti na asilimia 62 nchini Ghana."

Nyaradzayi Gumbonzvanda, mkuu wa Chama cha Vijana wa Kikristo Wanawake (YWCA), aliiambia IPS kuwa kuwekeza katika mawasiliano ya afya ya kujamiiana na uzazi ni suala la kuchagua.

"Tunahitaji mazingira mazuri kwa wale wanaojadili suala hili," alisema. "Tunahitaji kulinda vyombo vya habari – hili siyo chaguo.
Serikali lazima iongeze kiwango cha ushirikiano na kutoa msaada wa kisheria pale ambapo haupo."
Gumbonzvanda anadhani kuwa, uandishi wa habari wa kiraia unapaswa kuchukua nafasi kuondokana na hatari inayotokana na misimamo mikali, siyo kwa kutoa sauti tu kwa wale ambao mara nyingi hawasikiki, pia kuwapatia uwezo wananchi wa kawaida kuchukua hatua.

Hakuna mahali ambapo nguvu ya uandishi wa habari wa jamii imeonekana zaidi kuliko kipindi cha mapinduzi nchini Misri mwaka 2011, ambapo blogu, tweeter, na Facebook vilichukua nafasi ya vituo vya televisheni, magazeti na vituo vya redio katika kuwafikia watu.

Leo hii Wamisri wanakabiliana na sera za kihafidhina za utawala wa chama cha Muslim Brotherhood, ambapo mitandao ya uandishi wa habari wa kijamii imegeuza suala la afya ya uzazi na kujamiiana mada ambayo imetelekezwa na Uislam.

Ahmed Awadalla, ofisa jinsia na afya ya kujamiiana kwa Afrika katika Shirika la Wakimbizi la Mashariki ya Kati (AMERA), aliiambia IPS kuwa kila mmoja anajadili suala la hatari ya kuwekwa kizuizini, kukamatwa na kuwekwa jela.

Matokeo yake idadi ya wenye blogu inaongezeka kila siku, kwani wananchi na watetezi wanakimbilia katika nafasi ya mtandao kutafuta usalama wao katika kusambaza taarifa.

"Ninapoandika katika blogu kuhusu haki za kujamiiana za wanawake navunja sheria mbili," Awadalla alisema. "Kwanza, kwa kuzungumza kuhusu suala ambalo limezuiliwa na pili kuzunguma kama mwanaume, ambaye hatakiwi kuchukua nafasi ya mwanamke."

Pamoja na kukabiliana na ukandamizaji mbaya, hakuna ambacho kitamrejesha nyuma kutoa utetezi wake.

Lakini wakati wananchi wanabuni mawazo mapya ili kukabiliana na vitisho vikali vya kutoa elimu ya kujamiiana, wataalam wanasema serikali lazima isiachwe kwa kushindwa kutoa huduma hizi za msingi.