Chalinze yajielekeza kuboresha elimu

09Feb 2016
Pwani
Nipashe
Chalinze yajielekeza kuboresha elimu

UAMUZI wa Serikali kutoa elimu bure kuanzia elimu ya msingi hadi kidato cha nne,kuanzia mwaka huu wa masomo wa 2016 ni wa kuungwa mkono nakila anayetaka kuona kila mtoto mwenye umri wa kwenda shule anapata elimu.

Wanafunzi wakiwa darasani

Azma hii ya serikali ni kutaka kuona utekeleza wa Sera ya Elimu na Mafunzo ya mwaka 2014 yenye lengo la kuhakikisha kwamba, watoto wote wa Tanzania wanapata elimu bila kikwazo ikiwamo ada au malipo mengineyo.

Katika kutekeleza maamuzi hayo, imehakikishwa kuwa ada zote zilizokuwa zikilipwa kwa ajili ya elimu ya msingi na sekondari zimefutwa.Pia, waraka wa Elimu namba 8 wa mwaka 2011 kuhusu michango shuleni nao pia umefutwa.

Mpango huo na sera hiyo ya serikali ni ya kupongezwa sana. Hata hivyo, baadhi ya wadau mbalimbali wa elimu wilayani Bagamoyo, mkoani Pwani wameonyesha wasiwasi wao katika utekelezwaji wa sera hiyo na kusema kwamba ni mapema mno kuweka matumaini makubwa ikilinganishwa na idadi ya walimu katika shule pia changamoto walizo nazo walimu na shule .

“Sera ya elimu bure kwa wote ni nzuri na tunaipongeza sana serikali. Lakini wasiwasi wetu ni kuhusu upungufu mkubwa wa walimu katika baadhi ya shule zetu.

Hili ni tatizo sugu mfano shule ya msingi Kisambi kuna mwalimu mmoja tu anayefundisha zaidi ya watoto 120 kwa siku kuanzia darasa la kwanza hadi la saba,” alisema Mratibu wa asasi ya kijamii ya elimu ya NAPASO iliyoko mjini Chalinze mkoani Pwani, Grace Scorey.

Kwa mujibu wa utafiti uliofanywa na asasi ya kijamii ya NAPASO katika mradi wake wa uwajibikaji jamii katika kata 15 za wilaya ya Bagamoyo, ni shule sita tu ziko juu kwa wastani wa kitaifa na kwamba zilizobakia hazina walimu wa kutosha kulingana na idadi ya wanafunzi.

“Walimu wanakataa kwenda vijijini kutokana na mazingira mabovu katika shule. Hakuna nyumba za kuishi na huduma nyingine za kijamii. Ni vema serikali ikaangalia kwa jicho la karibu sana matatizo ya walimu ili waweze kufundisha katika mazingira mazuri,”anasema Scorey.

Grace Scorey anasema katika utafiti huo, walibaini changamoto nyingi za elimu katika kata hizo,kuwa ni upungufu wa vyumba vya madarasa, upungufu wa walimu, ukosefu wa vyoo, umbali wa shule, ukosefu wa nyumba za walimu, uhaba wa vitabu shule na kuwa hali hiyo huchangia utoro shuleni kwa baadhi ya wanafunzi.

“Ndio sababu hata sisi NAPASO tunaungana na walimu kwamba elimu bure kwa wote ili ifanikiwe ni vema serikali ikaangalia namna ya kuboresha miundombinu shuleni na maslahi ya walimu,” anasema Mratibu huyo.

Mwalimu mkuu wa shule ya msingi Muungano kata ya Mandera Ally Zuberi anasema,kufuatia sera hiyo uandikishwaji wa watoto wa darasa la kwanza uko juu na kwamba hadi sasa, idadi ya wanafunzi waliondikishwa ni 80 huku uandikishwaji unaendelea na kwamba wanatarajia ongezeko la idadi kubwa hadi kufikia 178 kwa mujibu wa sensa ya watoto wa umri wa kuanza shule.

“Sera ya elimu bure kwa wote imehamasisha wazazi hadi sasa nina zaidi ya watoto 80 walioandikishwa, na vyumba vya madarasa vinane tu, mahitaji ni vyumba 16 ili wanafunzi wakae kila darasa 45. Hata walimu hawatoshi. Changamoto kama hizo zingeshughulikiwa kwanza, ndipo sera hii ingeweza kutekelezeka kirahisi,” alisema na kuendelea.

“Kama mwalimu anaishi kilometa nne kutoka shule ama hakuna vyoo vya walimu shuleni, unafikiri anaweza kufundisha vizuri? Tusingalie tu elimu bure, tuangalie na walimu watakaotoa elimu hiyo kwa wanafunzi,” anasema mwalimu huyo.

Mwalimu Beda Ponela wa Shule ya Msingi Hondogo anasema ni lazima sera hiyo iendane na uboreshwaji wa miundombinu pamoja na kuboresha maslahi ya walimu ikiwamo mishahara ilipwe kwa wakati na kujengewa nyumba karibu na shule.

“Walimu wanaishi mazingira magumu sana vijijini. Mazingira yanayotulazimisha kwenda kulima vibarua ili tupate fedha za kujikimu. Hivyo, sera ya elimu bure kwa wote bila walimu kuwa na morali ya kazi ni bure. Tukizungumzia wanafunzi, tusiwaache walimu, kwani wakiandikishwa wengi nani atawafundisha kama si walimu,” anasema Beda.

Mwenyekiti wa kamati ya shule ya msingi Hondogo, Pilly Ally anakiri kuwa, ili utekelezaji wa sera hiyo ifanikiwe ni vema serikali ikashughulikia ama kupunguza changamoto shuleni.

“Shule zetu za msingi zina changamoto nyingi. Hapa Hondogo kuna upungufu wa walimu ambao baadhi wanaidai serikali stahili zao mbalimbali,” alisema Pilly.

Mwanafunzi wa shule ya msingi Hondogo, Zubeda Ally anakiri kuwapo kwa uchakavu wa majengo, upungufu mkubwa wa madawati, vyumba vya madarasa na kuiomba serikali kushughulikia suala hilo ili waweze kusoma vizuri.

Semani Saidi mkazi wa kijiji cha Rupungwi ambaye pia ni mjumbe wa serikali ya kijiji hicho anasema ni vema serikali ikashughulikia changamoto shuleni na kuboresha mazingira rafiki ili kuwavutia walimu waende vijijini kufundisha kikamilifu ndipo sera hiyo itatekelezwa vizuri