Ni hivi karibuni, Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI), imetia saini mkataba wa miaka mitatu ya makubaliano na Hospitali ya King Faisal ya nchini Rwanda na Hospitali ya Taifa ya Moyo, nchini Zambia, kutibu wagonjwa wa moyo.
Mbali na matibabu pia mkataba huo unahusisha ujenzi wa uwezo wataalamu wa afya wa hospitali kutoka nchi hizo, ikiwa ni mpango unaowezeshwa na Shirika la Okoa Moyo wa Mtoto Save a Child’s Heart (SACH) la nchini Israel, ambalo limejikita kwenye utoaji huduma na upatikanaji wa matibabu ya moyo nchini na kwa ujuzi kwa nchi mbalimbali za Afrika.
Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Afya Dk. Grace Magembe, mgeni rasmii kwenye hafla hiyo ya utiaji saini, anasema ni azma ya serikali ya Rais Dk. Samia, kuhakikisha kwamba huduma za afya nchini inakuwa sehemu ya utalii, huku nchi za Afrika zikivutiwa na huduma hizo na kuja kutibiwa.
Anasema, serikali iliyoko madarakani chini ya Rais Dk. Samia, imepiga hatua katika sura ya kuwekeza vifaa tiba na miundombinu, pia dawa za kuwezesha ufanisi wa hudunma hizo za kiafya ziimarike nchini.
“Huduma ya afya kiutalii ndio mkakati wa nchi na Rais Samia, baada ya kuwekeza kwenye rasilimali watu. Taasisi hii imekuwa ni kati ya zinazoaminiwa barani Afrika na huduma za JKCI zitaifikia mikoa yote kutoa uzoefu kwa madaktari wa hospitali zingine,” anasema Dk. Maghembe.
Anafafanua kisekta kuwa, nia ya rais sasa ni kupunguza idadi ya rufani ambazo hupatiwa wagonjwa kwa ajili ya tiba nje ya nchi, ambazo zina gharama kubwa, sasa zipatikaneJKCI.
WENYE JUKUMU
Mwenyekiti wa Bodi ya Wadhamini wa JKCI, Prof. William Mahalu, anasema hatua iliyofika taasisi hiyo ni kubwa, akisema anachokishuhudia katika utendaji wa matibabu bobezi na kibingwa ni ndoto yake kutimia.
“Wakati nafikiria kuanzisha taasisi ya moyo, kila mmoja aliniona napoteza muda. Nashukuru Mungu kunipa uhai na kushuhudia hiki leo, kwa sababu wapo walionikatisha tamaa kwamba taasisi ya moyo sio kipaumbele. Tujitahidi kufanya vitu wenyewe haijalishi kwa udogo gani. Upasuaji tufanye wenyewe,” anasema Prof. Mahalu.
Mkurugenzi Mtendaji wa JKCI, Dk. Peter Kisenge, anasema SACH ya Israel imekuwa ikiwasaidia watoto wenye magonjwa ya moyo kupata matibabu pamoja na kuwapa ujuzi madaktari wa JKCI, kwa ushirikiano tangu mwaka 2015.
Anasema shirika hilo lilianza kwa kuwachukua watoto wenye magonjwa ya moyo ambayo hayakuweza kutibiwa hapa nchini na kuwapeleka nchi ya Israel, kwa ajili ya matibabu na sasa JKCI imekuwa na uwezo wa kutibu magonjwa hayo, ndio maana nchi za Rwanda na Zambia zimefika nchini, ili nazo ziweze kupata ujuzi huo.
“Shirika la Okoa Moyo wa Mtoto la nchini Israel, limekuwa likiwahudumia watoto wenye magonjwa ya moyo wanaotoka katika familia duni kuokoa maisha yao na pale walipohitaji kuwapeleka nchini Israel walifanya hivyo kwa upendo,” anasema Dk. Kisenge.
Mkurugenzi Mtendaji wa Shirika la Okoa Moyo wa Mtoto (Save a Child’s Heart – SACH) la nchini Israel Simon Fisher, anasema hatua iliyofikia hadi Rwanda na Zambia kukubali kutia saini mikataba hiyo, imetokana na ushirikiano wa muda mrefu uliopo kati ya SACH na JKCI.
“Leo hii Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete inafanya upasuaji mkubwa wa moyo, pamoja na upasuaji wa tundu dogo kwa watoto kwa kujitegemea naamini baada ya miaka kadhaa wenzetu wa Rwanda na Zambia nao watakuwa na uwezo huo”, anasema Fisher
WADAU WASHIRIKA
Mkurugenzi wa Hospitali ya Taifa ya Moyo ya nchini Zambia, Dk. Shumba Chabwela, anasema kutia saini mkataba wa makubaliano ya kutibu wagonjwa wa moyo pamoja na kuwajengea uwezo wataalamu wa afya wa nchini Zambia, kunaonyesha utimilifu wa ushirikiano uliojengwa na waasisi wa nchi za Tanzania Mwalimu Julius Nyerere na wa Zambia Kenneth Kaunda.
“Kwa niaba ya nchi ya Zambia tunatoa shukrani zetu za dhati kwa kutupa nafasi ya kushirikiana nasi kuwahudumia wagonjwa wetu, kabla hata ya kusaini mkataba huu tayari tulishaanza kuleta wataalamu wetu kujifunza katika Taasisi hii”, anasema Dk. Shumba.
Naibu Mtendaji Mkuu Hospitali ya King Faisal ya nchini Rwanda, Frederic Ngirabacu, anasema ushirikiano katika sekta ya afya na sekta nyingine vinapaswa kufanyika baina ya nchi za Afrika ili kwa pamoja ziweze kukuwa na kuacha kutafuta huduma katika mataifa ya mbali.
“Tumeanza ushirikiano na JKCI wiki hii lakini pia tumefurahi kukuta waafrika wenzetu kutoka Zambia wanashirikiana nao, hii inaonyesha ukomavu katika nchi zetu za Afrika”, anasema Ngirabacu.
Kwa mujibu wa Naibu Mkurugenzio huyo, Shirika la Okoa Moyo wa Mtoto la nchini Israel, limekuwa likisaidia kutoa huduma za matibabu ya moyo kwa watoto wenye magonjwa ya moyo waliopo nchini Rwanda na sasa linawaunganisha na JKCI, ili kuendeleza ushirikiano, jambo ambalo hawakulitarajia hapo awali.