Uboreshaji wa Sheria ya Gesi na Mafuta

01Apr 2016
Denis Maringo
Nipashe
Uboreshaji wa Sheria ya Gesi na Mafuta

SEKTA ya gesi ni moja ya zile zinazokua kwa kasi zaidi na inayotabiriwa kuleta mapinduzi ya kipekee ya kiuchumi katika Tanzania, iwapo raslimali hii itatafutwa na kuvunwa kwa maslahi yenye kunufaisha si tu wawekezaji pia nchi yetu.

Ukweli wa kauli hii, unatokana na tathmini kutoka kwa wataalam na taasisi za kiuchumi zinazoheshimikakimataifa ambazo zinaiweka Tanzania miongoni mwa nchi nne zitakazokuwa na uchumi mkubwa zaidi dunia, sawia na nchi za Nigeria, Afrika ya Kusini na Misri.

Lakini yote haya yatatokea iwapo tu kutakuwa na maboresho zaidi ya kisera, kisheria na kitaasisi ili kwamba kila mdau anayehusika anufaike na raslimali hii pamoja na sekta nyinginezo kama zile za madini, utalii, biashara na nyinginezo.

Ndiyo maana basi, safu hii, mara kwa mara imerejea tena kuyazungumzia masuala muhimu yanayohitaji kufuatiliwa kwa karibu na kila raia wa Tanzania, ili kwamba raslimali kama Gesi asili ambayo ilivumbuliwa kwa wingi eneo la Songosongo, karibu na Kilwa, mkoani Lindi (1974), Ghuba ya Mnazi, mkoani Mtwara (1982), inalinufaisha taifa badala ya kugeuka kuwa laana izaayo umaskini ama vita kama ilivyotokea Congo na kwingineko.

Hivi karibuni uvumbuzi wa futi za ujazo wenye gesi nyingi zaidi umetokea katika maeneo hayo na mengineyo kama Mafia, Mkuranga, Tanga, Kigoma, Selous na kwingineko.

Katikati ya jambo hili, leo tuzungumzie ni namna gani nchi kama Tanzania inapaswa kufanya maboresho katika Sheria, utawala na Muundo wa Kitaasisi wa Usimamiaji wa Sekta hii inayokua kwa kasi kubwa.

Jambo hili ni muhimu sana, kwa sababu japo unufaikaji wa nchi hii haujakidhi maslahi ya nchi na pia matarajio ya wananchi wa kawaida hata sasa ambapo raslimali gesi-asilia inazidi kutafutwa na kuendelea kuchimbwa kwa ushirikiano wa mikataba ya Uzalishaji kwa Ubia (PSAs) baina ya Serikali, kupitia Shirika la Maendeleo ya Petroli (TPDC), kwa upande mmoja, pamoja na makampuni ya kimataifa yaliyowekeza katika sekta hiyo hapa nchini.

Tukumbuke kwamba, kwa utaratibu wa sasa, sekta ya gesi asili haina sera ya kitaifa, ingawa serikali kupitia Wizara ya Nishati na Madini, imeshakamilisha mchakato wa uandaaji wa Sera hiyo, ambayo rasimu yake imepangwa kuzinduliwa hivi karibuni iwapo ahadi ya Serikali itabaki ya kweli.

Pamoja na kutokuwepo sera ambayo tayari kuna mikataba mingi iliyoingia na makampuni yasiyopungua 12 ya kimataifa (kama Petrobras, BG, Pan Africa, Statoil, Maurel & Prom na mengineyo), pingufu jingine kubwa ni uzee wa sheria inayoitawala sekta hii ndogo.

Sheria hiyo ni Sheria ya Utafutaji na Uzalishaji wa Petroli, yaani Sheria namba 27 ya mwaka 1980, ambayo ilitungwa miaka mingi na imebaki pasipo kufanyiwa marekebisho muhimu ya kulinda maslahi ya nchi, japo maslahi ya wawekezaji yameboreshwa kupitia Sheria kama ile ya Uwekezaji ya mwaka 1997.

Muundo wa Kitaasisi ni jambo jingine lenye mapungufu. Wakati Sekta hii inasimamiwa na Wizara ya Nishati na Madini, kupitia Shirika la Petroli Tanzania (TPDC) katika uingiaji wa mikataba, Mamlaka ya Udhibiti wa Sekta za Nishati na Maji (EWURA) nayo ina mkono wake katika sekta hii, hasa katika masuala ya tozo.

Baraza la Mazingira la Taifa (NEMC) linahusika pia katika mazingira jambo ambalo ni muhimu kutokana na athari kubwa za mazingira katika utafutaji na uchimbaji huu.

Uhusika wa taasisi hizi si kitu kibaya, lakini ukweli ni kwamba zipo nyakati kuna mwingiliano fulani wa majukumu kama ilivyoainishwa na Kamati ndogo iliyofanya uchunguzi wa Sekta hii ndogo katika Ripoti muhimu iliyokuwa chini ya Waheshimiwa January Makamba na Diana Chilolo.

Zaidi ya hapo, taasisi hizi hazina meno makali ya kisheria linapokuja suala la kumchukulia hatua mwekezaji anayekiuka dhahiri sheria kama ambavyo Ripoti ya kamati hiyo ilivyofafanua na kutolea mifano baadhi ya makampuni haya ya gesi.

Pengine pungufu la kisera, kisheria na kitaasisi, lililokubwa zaidi ni kwamba nafasi ya ushirikishwaji wa mamlaka za uongozi wa za Serikali, Wilaya na Vijiji ambavyo raslimali ya gesi inapatikana.

Hili limedhihirika kote palipo na gesi hii, ambapo watendaji wa Halmashauri za Wilaya na Vijiji vitekelezavyo Majukumu yake kupitia Sheria namba 7 na 8 za mwaka 1982, zinazohusika na majukumu ya Mamlaka za Serikali za Mitaa Mijini na Wilayani, hawajui undani wa chochote kuhusiana na shughuli za utafutaji gesi na mfuta na pia uchimbaji gesi katika maeneo raslimali hizi zimo.

Ushirikishwaji wa serikali za mitaa kama Halmashauri na watendaji wa vijiji husika ungesaidia tu kuwafanya wanaozunguka raslimali hizo, kujiona nao ni wamiliki, lakini pia wangeisaidia Serikali Kuu, kubaini pungufu lolote kama ukiukwaji wa masuala ya kimazingira uwezao kufanywa na Wawekezaji katika shughuli zao.

Athari za kutoshirikishwa wananchi hawa, ni kwamba utokeapo ukiukwaji huo wananchi hawa wanakuwa tu si hawajaelimishwa wawasilishe malalamiko yao wapi, lakini pia pengine wanaweza wasidiriki hata kuyawasilisha kwa kuamini kwamba, pengine hicho kinachofanywa, japo kinakiuka sheria kama zile za mazingira, huenda kimeruhusiwa kufanyika, kwa vile mikataba husika kwa muda mrefu sasa imebaki kuwa siri baina ya Serikali Kuu, kupitia Wizara husika na TPDC, na wawekezaji.

Haitoshi tu kumshirikisha raia wa Tanzania, wakiwemo wakazi wa Kilwa, Songosongo, Mafia, Kilwa, ama vijiji lipitalo bomba la gesi, kutoa maoni katika ngazi ya Tathmini za Uharibifu wa Mazingira (EIAs).

Mchakato huu (EIAs), kwa mujibu wa Sheria ya Menejimenti ya Mazingira ya 2004, hupaswa kufanyika kwa mwekezaji kuandaa ripoti inayoonyesha athari chanya ama hasi za kimazingira ziwezazo kutokea katika shughuli zake na namna gani ataziepusha ama kuzipunguza.

Kwa kadri ninavyofahamu hatua hii ndipo pekee ambayo raia hawa hushirikishwa kwa dhati ingawa nayo ina mapungufu yake kama vile notisi kutowafikia wahusika wote na muda mfupi wa utangazwaji.

Mabadiliko yanayopendekezwa hapa yafanyiwe kazi kama ambavyo Serikali imeahidi mara kwa mara, kutaka kufanya mabadiliko ya kweli na yenye kulenga kuinufaisha nchi na kila raia kupitia sekta hii.

Wizara ya Nishati na Madini na Mwanasheria Mkuu wanatarajiwa sana walete muswada wenye tija wa Gesi sambamba na Sera katika masuala ya nishati za gesi pia mafuta.

Kwa hivyo basi, fursa za kuiimarisha sekta ndogo ya gesi zipo na ziendelee kutumiwa kwa kuwashirikisha wadau wote ili hatimaye mapinduzi yenye maslahi ya kiuchumi kwa nchi yetu yaonekane na kusaidia kuondokana na umaskini.

*Denis Maringo ni Mwanasheria aliyeko Dar es Salaam. Mawasiliano: 0719270067. Barua-pepe: dnmaringo@gmail.com