Mratibu wa Kongamano hilo, Dk. Kaushik Ramalya, alisema lengo la kongamano hilo lilikuwa kuwakutanisha wadau kutoka nchi za Afrika Mashariki na Kusini, kuchunguza na kujadili Kisayansi madhara ya ugonjwa huo na namna ya kukabiliana nayo.
Ulikuwa uwanja wa kubadilishana uzoefu wa kutatua matatizo yatokanayo na ugonjwa huo ambao unakuwa kwa kasi barani Afrika.
Kongamano hilo liliendeshwa na asasi inayojihusisha na masuala ya ugonjwa wa kisukari Afika Mashariki, The Eafrica Diabetes Study Group (EADSG).
Waziri anasema kuwa, EADSG, kwa kushirikiana na wizara yake lilifanya mkutano maalumu wa wadau wa kisukari duniani jijini Dar es Salaam.
Anaongeza mkutano huo uliandaliwa na Mfuko wa Kusaidia Kisukari Duniani (NCD Symposium) wa Denmark, kwa kushirikiana na Wizara yake na na Shirika la Afya Duniani(WHO).
Mikutano hiyo miwili ililenga kutatua tatizo la Kisukari linalooendela kukua barani Afrika na sasa inaonekana kukua mara tatu zaidi, ndani ya miaka mitano iliyopita.
Dk. Ramalya anasema mbali na mjadala wa uchunguzi wa kisayansi, mengine yatakayojadiliwa ni kuongezeka kwa kisukari katika nchi zinazoendelea.
Mada nyingine zitakazojadiliwa ni kuhusu mzigo wa kijamii na kiuchumi unaotokana na watu wenye kisukari, familia zao na jamii kwa ujumla.
Hata hivyo, imeelezwa kuwa asilimia 9.1 ya Watanzania wanaugua ugonjwa wa kisukari, hali inayochangiwa na unywaji pombe, uvutaji wa sigara, na ulaji wa vyakula usiofaa.
Utafiti wa namna mbalimbnali unaonyesha kuwa kasi ya ongezko la ugonjwa wa Kisukari iko juu
Duniani na mwaka 2007, kulikuwapo wagonjwa milioni 246 duniani.
Takwimu zinaonyesdha kuwa, mwaka 2012 waliongezeka kufikia milioni 371 na mwaka 2013, walifikia wagonjwa milioni 382 duniani kote.
Kwa mwenendo huo, inakadiriwa ifikapo mwaka 2035, kutakuwapo wagonjwa 592 millioni.
Dk. Ramalya anasema kuna umuhimu wa kutafuta ufumbuzi wa ugonjwa huo, kuanzia ngazi za mkoa kwa kutolewa taarifa za uchunguzi kuhusu ugonjwa huo.
Aidha, utafiti uliotolewa hivi karibuni unaonyesha kuwa katika kila sekunde sita zinazopota, kuna mtu mmoja anakufa kutokana na ugonjwa wa kisukari (vifo zaidi ya milioni tano hutokea duniani)
Pia, mtu mmoja katika kundi la watu wazima 11 ana ugonjwa wa kisukari (watu milioni 415 duniani kote wanaishi na Kisukari)
Takwimu hizo zinatoa ufafanuzi kwamba kuna kundi kubwa la watu wazima wanaokufa kutokana na ugonjwa wa kisukari, kuliko kinachotokea kupita maambukizi ya Virusi vya Ukimwi, kifua kikuu na malaria.
KISUKARI NINI?
Ugonjwa wa Kisukari ni hali inayotokea, wakati sukari katika damu inapokuwa nyingi kupita kiwango cha kawaida kwa muda mrefu.
Sukari hutumiwa na mwili ili kupata nishati lishe na kuwezesha kutumia sukari inayotokana na vyakula.
Insulin husaidia sukari kuingia kwenye chembechembe hai ili kutengeneza nishati lishe.
Ugonjwa wa kisukari unasababishwa na kichocheo hicho kupungua au kutofanya kazi kama inavyotakiwa, hivyo kiwango cha kisukari kinabaki kuwa kikubwa kwenye damu, kwa sababu sukari haikuwezeshwa kuingia kwenye chembechembe hai za mwili wa binadamu.
Asilimia 80 ya wagonjwa wa kisukari duniani wanaishi katika nchi zinazoendelea, ikiwamo Tanzania.
Utafiti uliofanyika mwaka 2012 na kuhusisha wilaya 50 nchini Tanzania, ulionyesha asilimia 9.1 ya Watanzania wenye umri wa miaka 25 na kuendelea wana ugonjwa wa kisukari.
Katika nchi 10 zinazoongoza kwa kisukari Barani Afrika Tanzania inashika nafasi ya nane.
DALILI ZA KISUKARI
Kutokana na mfumo wa maisha kuna kundi kubwa la watu wasiojitambua kuwa wanaugua ugonjwa wa Kisukari.
Afrika inaongoza kwa wagonjwa wa kisukari ambao haujatambuliwa, kutokana na kutokaguliwa afya zao.
Mtu mwenye kisukari aina ya pili, inadaiwa anaweza kuishi kwa miaka kadhaa bila ya kuonyesha dalili yoyote, madhara yanayoweza kujitokeza ni pamoja na ugonjwa wa figo , moyo kushindwa kufanya kazi, ugonjwa wa jicho na kusababisha upofu na matatizo ya mguu na kusababisha ulemavu.
Hata hivyo, wapo wagonjwa wanaolezwa waanajitambua kuwa na Kisukari kwa kuona dalili, lakini hawachukui hatua za mapema, hivyo huelemewa hali inapofikia hatua mbaya.
Zaidi ya asilimia 66.7 ya watu wenye ugonjwa wa kisukari, wanadaiwa kutojitambua kuwa wana maradhi hayo.
DALILI ZAKE
Dalili za kisukari ni: kusikia kiu isiyoisha, kukojoa mara kwa mara, kupungua uzito, kusikia njaa kila wakati na mwili kukosa nguvu.
Mgonjwa anaweza kuona dalili ya kuchoka haraka, kupungua uzito, vipele mwilini.
Pia, kuna hali ya kuwa katika dalili ya kupata maambukizi katika kibofu cha mkojo, ngozi na kwa wanawake ni katika sehemu za siri.
Aidha kuna dalili mahsusi zinazotokea, iwapo mgonjwa wa atapatwa na mojawapo ya madhara ya ugonjwa huo.
Madhara hayo ambayo hujulikana kwa kifupi kama ‘DKA’ hutokea kwenye aina ya kwanza ya kisukari na huwa na dalili zifuatazo: Mgonjwa kutoa harufu inayofanana na pombe.
Pia mgonjwa hupumua kwa haraka akijihisi ana kichefuchefu, kutapika, maumivu ya tumbo na wakati mwingine anapoteza fahamu.
Kupoteza fahamu kwa mgonjwa kunakoitwa Hyperosmolar Non-ketotic, hutokea kwa mgonjwa wa kisukari aina ya pili na mara nyingi husababishwa na upungufu wa maji mwilini.
TIBA YA KISUKARI
Kisukari hakina tiba kamili, zaidi ya mazoezi na tiba mbadala ya ugonjwa wa kisukari inayotakiwa kufanyika kabla ya tatizo halijawa kubwa ni malazi mazuri na virutubisho.
Mpaka sasa hakuna dawa ya sahihi ya kukifuta kisukari, ingawa watu wanaweza kukirekebisha kupitia lishe, matumizi ya vidonge maalum aina ya insluni na sindano.
Dawa za kisukari za kumeza ni zile ambazo huchochea kongosho kutokeza insulini zaidi, nyingine hudhibiti ongezeko la sukari katika damu na nyingine hudhibiti ongezeko la sukari katika damu na nyingine huwezesha chembe za mwili kupokea insulini.
Kuna utafiti wa kupandikiza (transplant) unaofanywa, ili kuongeza insulini mwilini kwa kutumia sehemu ya kongosho (pancreases) ya mtu mwingine, lakini bado haujafanikiwa kutumika kama matibabu.
Watafiti nchini Japan wamegundua jinsi chembe hai za mfumo wa fahamu zinazoweza kutumika kupandikizwa kwenye kongosho, ili kukitibu kisukari.
Kwa hali ya kawaida, wataalamu wa afya hupendekeza lishe ambayo si tiba ya ugonjwa wa kisukari, lakini inaweza kurudisha virutubisho muhimu ambavyo vinaweza kukosekana, kutokana na ugonjwa wa kisukari.
Mataifa ya Barani Afrika yenye wagonjwa wengi wa Kisikari ni Afrika Kusini (Watu 2.3 milioni), Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo watu (milioni 1.8), Nigeria (milioni 1.6) na Ethiopia (1.3 milioni).
Mwisho.










