Katika msimu wa kilimo (2015-16), Mkoa wa Shinyanga umeonekana kupata neema ya chakula ambacho kitawaondoa kwenye dhana ya kuombeleza chakula cha msaada, huku serikali mkoani humo ikianza kuhamasisha wananchi juu ya utunzaji wa chakula cha akiba na kuachana na tabia ya kukichezea kwa kunywea Pombe, kuoa wanawake wapya pamoja na kukiuza ovyo.
Mkoa huo ambao una halmashauri sita ambazo ni Ushetu, Msalala, Kahama mji, Shinyanga vijijni, Kishapu na Shinyanga manispaa, umekuwa ukikumbwa na baa la njaa kwa miaka mingi kutokana na ardhi yake kuwa kame na hivyo kusababisha serikali mkoani humo kuwa ombaomba wa msaada wa chakula kila mwaka.
Hata hivyo katika Halmshauri hizo sita mbili kati yao, Kishapu na Shinyanga vijijini ndio zimekuwa zikiadhirika sana na tatizo la njaa, hali ambayo serikali mkoani hapa imekuwa ikielekeza nguvu zake huko kuhamasisha wananchi kulima mazao ya ukame, Viazi vitamu, Choroko, Alzeti na Mtama.
Msimu wa kilimo uliopita (2014-15) wananchi wa halmashauri hizo walikuwa wanahalimbaya ya chakula ambapo licha ya kulima mazao hayo ya Muda mfupi yalikaushwa na jua kutokana na ardhi hiyo kuwa kame na kupelekea wananchi kushindia uji au mlo mmoja ili kunusuru maisha yao.
Aidha msimu huu wa kilimo (2015-16) umeonekana kuwa na neema sana ya mvua, ikiwa licha ya wananchi wa maeneo hayo ya ukame baadhi yao kukaidi agizo la serikali kulima mazao ya muda mfupi kama vile Mtama, na kuamua kulima Mahindi imeonekana kubahatika kupata chakula kwa wingi ambacho kitawakomboa.
Josephine Matiro ni mkuu wa wilaya ya Shinyanga ambaye ameamua kufanya ziara katika halmashauri ya wilaya ya Shinyanga vijijini akiambatana na mkurungezi wa halmashauri hiyo Kiomoni Kibamba kuhamasisha wananchi juu ya utunzaji wa chakula na kuacha kukichezea ovyo kwa matumizi yasiyo rasmi.
Matiro anasema kutokana na msimuu huu wa kilimo kuonyesha kuwa kutakuwa na dalili ya wananchi kupata mavuno mengi ya chakula, hivyo hategemei kusikia mkoa huo wa Shinyanga unakabiliwa na Janga la chakula tena.
“Itakuwa ni maajabu sana wananchi kupata mavuno mengi ya chakula harafu msimu wa kilimo ukikalibia tena, ninasikia wananchi wanataka msaada wa chakula haya yatakuwa ni maajabu ya Musa, hivyo natoa agizo kila kaya itunze chakula msimu wa Mavuno utakapo wadia tutakagua,” amesema Matiro
Anaongeza” Ninataka kila kichwa ndani ya familia itunze magunia ya chakula matatu kama mkiwa wanne nikute magunia 12, kwa mji ambao nitakuta hakuna chakula kilichotunzwa serikali itakula Sahani moja na nyie hatuwezi kila mwaka tunadhalilika kwa kuwa ombaomba wa msaada wa chakula.”
Naye Mkurugenzi wa halmashauri hiyo Kiomoni Kibamba anasema licha ya wananchi kulima mazao hayo ya muda mrefu, wanapaswa pia kulima mazao ya muda mfupi ambayo yanauhakika wa kutoa Mavuno katika ardhi ya Shinyanga na kuacha kulima kilimo cha kubahatisha.
Kibamba anasema anawataka wananchi kulima mazao ya muda mfupi angalau hata hekali Moja moja kuliko kuacha kabisa, huku akiwataka wataalamu wa kilimo kuacha tabia ya kukaa ofisini bali wanatakiwa kuweka Ratiba ya kutembelea wananchi na kuwahamasisha kulima Mazao hayo ya Muda mfupi pamoja na kukitunza.
Hawa Ng’humbi ni mkuu wa wilaya ya Kishapu yeye anatoa Ovyo kwenye mkutano wa hadhara na wananchi wa wilaya hiyo, kuwa kama mtu hajalima Mtama au kijiji, serikali haitaleta msaada wa chakula kwenye kaya hiyo au eneo hilo ili liwefundisho katika kutii maagizo ya serikali.
“Serikali tumeshapiga kelele vya kutosha wananchi kulima mazao ya muda mfupi lakini mmekuwa mkikaidi maagizo ya serikali na na janga la njaa linapowakumba mnaanza kuomba msaada wa chakula, kwa msimu wa kilimo (2015-16) msipokuwa makini hakuna msaada wa chakula mtajijua wenyewe,” anasema Ng’humbi
Aidha wakuu hao wawili wa wilaya ya Kishapu na Shinyanga maeneo ambayo yamekuwa na janga la njaa kila mwaka mkoani Shinyanga, wamewataka wananchi hao kutunza chakula kwa kutumia Vihenge, au Magunia ya kitaalamu na kuweka dawa iliyasiingiliwe na wadudu kwa lengo la kukomesha njaa mkoani humo.
Hazina Thomasi ni Ofisa kilimo wa Kijiji cha Ilola tarafa ya itwangi halmshauri ya wilaya ya Shinyanga vijijini, anasema licha ya kushauri wananchi kutunza chakula lakini wanaume ndio limekuwa tatizo hivyo anaiomba serikali itunge sheria ndogo ambayo itawapa nguvu ya kuwabana watu wanaochezea chakula kwa Pombe na kukiuza ovyo.
Naye Mariam Ngusa mkazi wa Itwangi halmshauri ya wilaya hiyo anasema Serikali inapaswa kutoa elimu zaidi kwa wanaume juu ya kulima mazao ya muda mfupi pamoja na utunzaji wa chakula ikiwa wao ndio kichwa cha familia na mwanamke akijaribu kupinga anapokea kipigo.










