KANTANGAZE

25Feb 2016
Nebart Msokwa
Mbeya
Nipashe
KANTANGAZE
  • ***Mdudu sugu wa nyanya ‘anayewalisha’ watumiaji sumu na mkojo wa ng’ombe

KWA wakazi na hasa wakulima wa mikoa ya Iringa na Njombe jina la mdudu ‘kanitangaze’ si geni kwao, kwani ndiko wanakopambana naye na hata wakampatia jina hilo.

mdudu ‘kanitangaze’ akishambulia nyanya.

Upekee wa jina hilo pamoja na madhara yake ndiyo yanayojenga umaarufu huo.

Kanitangaze katika lugha ya kitaalam anaitwa ‘Tuta Absoluta.’ Ni miongoni mwa wadudu waharibifu na wanaoshambulia kwa kasi zao la nyanya. Tabia hiyo ndiyo iliyosababisha wakazi wa mikoa hiyo kumpatia jina hilo.

Mtaalam wa Kilimo katika wilaya ya kilolo mkoani Iringa, Lawrence Mgova, ambaye ana uelewa mkubwa wa mdudu huyo, anasema kuwa amebatizwa jina hilo kutokana na tabia ya kushambulia zao la nyanya kwa kasi kubwa na kwamba hakuna sumu iliyothibitika kumdhibiti.

Mgova anasema, mdudu huyo anapoingia shambani ni lazima mkulima atahangaika kutangaza akiomba wataalam ama wamsaidie au kuomba ushauri kwa maofisa kilimo na wakulima wenzake ili kunusuru shamba lake.

“Mdudu huyu mara nyingi akiingia shambani, ni lazima mkulima atamtangaza kwa wenzake au kwa maafisa kilmo akiomba msaada, kwani hushambulia nyanya kwa kasi kubwa na mpaka sasa hakuna sumu inayomdhibiti, ndio maana tulimbatiza jina hilo la Kanitangaze,” anafafanua Mgova

Anasema mdudu huyo huharibu majani ya nyanya na matunda na huingia katika sehemu ya ndani katikati ya jani, analikunja ili isiwe rahisi kwa sumu kumdhuru.

Mgova anasaema kuwa, katika tunda ana tabia ya kuingia sehemu ya ndani kupitia kwenye kikonyo anakofanya makazi, jambo linalofanya sumu hiyo kuwa ngumu kumkuta, hali inayofanya tunda liendelee kuoza.

TIBA YA MKOJO WA NG’OMBE

Anasema katika wilaya yake ya Kilolo, wameshaanza kutumia mkojo wa ng’ombe kumthibiti, ingawaje anakiri humfanya azimie kwa muda na kisha anaendelea na uharibifu wake.

Mgova anasema hatua inayoendelea katika ‘utafiti pori’ wanaouendeleza sasa wilayani Kilolo ni kwamba wananuia kujaribu kuchanganya mkojo huo wa ng’ombe na baadhi ya dawa zingine, kuona ni matokeo yake kama yana manufaa.

Mkulima wa nyanya katika Kata ya Lyamkena, iliyoko kwenye Halmashauri ya Mji wa Makambako, Charles Mhapa, ambaye ni miongoni mwa wahanga wa ‘Kanitangaze’ anafafanua hasara itokanayo na mdudu huyo akitamka:

“Ni vigumu kujua hasara ambazo wakulima tunapata, kwa sababu mara nyingi hatutunzi kumbukumbu za kile tunachowekeza katika kilimo na kile wanachopata baada ya mavuno. Isipokuwa yanapotokea matatizo kila mtu hulalamika kuwa ameingia hasara.”

Ofisa Kilimo Mazao ya Bustani na Matunda wa Halmashauri ya Mji Makambako, Telesphory Danda, anasema bado wanaendelea kufanya utafiti wa kupata sumu ya kumdhibiti kabisa mdudu huyo.

Anasema ‘Kanitangaze’ nchini imeshamiri zaidi katika mikoa ya Iringa, Mbeya, Morogoro na Njombe.

Danda anasema kuwa baada ya watu kutumia sumu za madukani na imeshindikana, wameanza kutumia za dawa za kienyeji ikiwemo Muarobaini, huku kuna kundi la waliokata tamaa kabisa.

Naye Mkulima kutoka Kijiji cha Izumbwe katika Mamlaka ya Mji mdogo wa Mbalizi mkoani Mbeya, Raphael Msolo, anasema kwamba wameshauriwa kumdhibiti mdudu huyo kwa kulima nyanya kwenye mashamba yaliyolimwa mazao yenye mizizi tofauti.

Anataja baadhi ya mazao hayo ni mahindi, karoti na vitunguu. Msolo anasema hiyo itasaidia kuenea kwa mdudu huyo na wataalam wanashauri kuondolewa magugu mara kwa mara, kwani ndiko wanakoishi.

Msolo anasema mkoani Mbeya, hivi sasa ni mwaka wa pili tangu mdudu huyo aingie, wametumia dawa nyingi bila ya mafanikio ya kumdhibiti.

BALAA LA SUMU

Vita dhidi ya ‘Kantangaze’ imeleta balaa lingine la mikusanyiko ya sumu katika nyanya, kwanui kuna vita ya aina nyingi inayopiganwa na wakulima sasa wanaweka simu kwenye nyanaya inayoliwa na binadamu.

Ofisa Kilimo wa Mazao ya Bustani na Matunda wa Halmashauri ya Mji Makambako Telesphory Danda, anasema kuna sumu nyingi ambazo wakulima wanazitumia kupambana na mdudu huyo.

Mtaalam huyo anazitaja katika majina yao ya kitaalam kuwa ni; Prove, Belt, Thunder na Buffalo ambazo ni zote sumu kali.

Danda anafafanua kuwa Belt ni sumu hatari zaidi kwa walaji, kwa sababu huingia ndani ya matunda ya nyanya na hasa kupitia matundu yaliyotobolewa na ‘Kanitangaze’ na inabaki humo hadi hatua ya kuliwa.

Kutokana na tatizo la dawa, Danda anaasa ni vyema wakulima kutoitumia sumu hiyo wakati wa matunda na badala yake watumie nyanya zikiwa ndogo na baada ya hapo watumie sumu zingine.

WATAALAM WA KILIMO KENYA

Wataalam wa Kilimo wenye ofisi yao mjini haoa wakakiri kumfahamu mdudu huyo, na mmoja wa wataalam hao, Timothy Njuguna, anasema mdudu huyo yupo sehemu nyingi duniani.

Anataja mfano wa Brazil, ambako ‘Kanitangaze’ anasababisha hasara kubwa kwa wakulima na hadi sasa, kama walivyo kwa wakulima wa Mbarali, Kilolo na Makambako, nao huko ugaibnuni wanahanagaika pasipo ufumbuzi wa kumdhibiti.

“Nilikuwa nawasiliana na rafiki yangu mmoja anayeishi nchini Brazil ambaye aliniambia kuwa mdudu huyo ameshambulia na kuharibu shamba lenye ukubwa wa ekari 65 na hajaambulia kitu,” anasema Njuguna, kama sehemu ya mfano.

Anasema njia pekee iliyogunduliwa kusaidia vita dhidi ya ‘Kantangaze’ ni matumizi ya teknolojia ya Kitalu maarufu kama Green House. Hata hivyo, anatahadharisha kuwa inahitaji mtaji mkubwa.

Anaongeza kuwa, teknolojia licha ya kumdhibiti Kantangaze, pia inasaidia kuzuia wadudu wengine kama vile Vidukari, Vithiripi, Inzi weupe, Sota, Inzi Vidomozi, Utitiri Mwekundu na Minyoo fundo.

Njuguna anasema teknolojia hiyo ina tija na ndio imewatajirisha vijana wengi nchini Kenya na awanashauri wakulima wa Tanzania kuwekeza katika utaalamu huo.

Athari za ‘Kantangaze’ zimeanza kuonekana kitaifa hasa katika bei ya Nyanya katika mikoa ya Mbeya na Njombe, mathalan bei ya nyanya imepaanda.

Debe lililokuwa ilikiuzwa kati ya Sh. 10,000 na Sh. 15,000, sasa bei yake ni kati ya kwa debe lakini kwa sasa zinauzwa shilingi 20,000 na Sh. 25,000.

Mwandishi Nebart Msokwa anapatikana kwa mawasiliano Simu: +255 764 232 876 na barua pepe: msokwanebart @gmail.com