Serikali itaacha lini kununua 'mashangingi' kubana matumizi

25Apr 2016
Na Mwandishi Wetu
Sema Usikike
Serikali itaacha lini kununua 'mashangingi' kubana matumizi

MIAKA mitatu iliyopita, Waziri Mkuu mstaafu wa Tanzania, Mizengo Pinda, alipata fursa ya kuzungumza na makatibu wakuu wa wizara na kuwaambia wazi kuwa Serikali ilikua na kila sababu ya kupunguza kama si kuachana kabisa na ununuzi wa mashangingi.

Magari ya kifahari

Kauli hiyo ilionekana kama tumaini jipya kwa Watanzania ambao ndio wanabeba mzigo wa kuhudumia magari hayo tangu kununuliwa kwake hadi gharama za kila siku. Wengi tumeona jinsi ambavyo mambo yalivyokuwa magumu wakati wa serikali zilizopita na hii ya Awamu ya Tano kwa kuendelea kutumia magari hayo, hivyo kuibua swali kuwa, Je mpango huo wa kuachana na magari hayo utaanza lini kutekelezwa? MWANDISHI WETU anaeleza zaidi.

Ukipata fursa ya kuzungumza na watu wa kawaida, utawasikia wakilalamikia mpango wa muda mrefu wa Serikali kununua magari ya bei kubwa kwa ajili ya matumizi ya kila siku ya watumishi wake.

Kwa muda mrefu sasa, Serikali imekuwa ikinunua magari ya bei kubwa yakiwamo Mashangingi na kuwapa mawaziri, manaibu, makatibu wakuu wa wizara, wakuu wa mikoa, wilaya, idara mbalimbali na wakurugenzi wa taasisi zake.

Serikali pia imejikuta ikiwapa au kuwakopesha fedha au magari wabunge, mamea wa majiji na manispaa kupitia ofisi ya Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI), ambayo kwa sasa ipo chini ya Ofisi ya Rais.

Utaratibu huu umeonekana kama mzigo mzito kwa taifa, alisema Pinda na kuongeza kuwa mwaka mwaka juzi pekee Serikali ililazimika kununua magari mapya aina hiyo 80 katika kujaribu kufidia mapengo yaliyopo.

Aliwaambia makatibu wakuu hao kuwa, mzigo unakuwa mkubwa zaidi kutokana na utaratibu wa Serikali wa kutoagiza magari yaliyotumika na kwamba wakati sasa umefika kwa Serikali kubuni utaratibu mwingine wa kuwapatia magari wakubwa hao.

Aidha, Pinda alisema ni muhimu kama siyo lazima kwa Serikali kutata haraka iwezekanavyo mfumo mwingine wa kuendesha nchi, hasa katika ununuzi wa magari hayo ya wakubwa, vinginevyo nchi inaweza kujikuta katika lawama kubwa siku zijazo.

Kwa kawaida, shangingi moja jipya aina ya Toyota Landcruser VX New Model, GX na Landcruser Starndad uuzwa kati ya sh.Milioni 80 hadi 400 na kwamba, matumizi yake huwa ni makubwa zaidi kutokana na viongozi wengi kuwamo katika orodha ya wanaopata.

Pinda amekiri kuwa, hii ni changamoto nyingine kwa Serikali ya Awamu ya Tano hasa katika kipindi hiki cha miaka mitano ya mwanzo ambayo pamoja na mambo mengine, inapigania kujenga uchumi imara unaoendana na ubanaji wa matumizi.

Mheshimiwa Pinda awahi kusema kuwa Watanzania wanaangalia kwa makini mwenendo na utendaji wa shughuli za kila siku za serikali yao na kwamba wangependa kuona mabadiliko waliyoahidiwa katika kubana matumizi yakifanyika haraka.

Pia amesema kuwa ukubwa wa gharama za uendeshaji wa magari hayo haziishii katika manunuzi tu, bali hata huduma za mafuta na vipuri vyake ni vya bei ya juu pia.

Simon Ndalu, mhazini wa taasisi ya vijana na maendeleo inayojulikana kama Ruangwa Organization for Youth Network (Royonet) ni baadhi ya waliotoa maoni yao akisema kauli ya Pinda kwamba ununuzi wa magari hayo na uwendeshaji wake ni gharama kubwa, inapaswa kutafsiriwa kwa vitendo na kwa haraka sana.

Hata hivyo, Ndalu ameonyesha hofu yake juu ya utekelezaji wa mpango huo uliopangwa na serikali iliyopita hasa kutokana na watendaji wengi kutojali maadili ya uongozi na wengi wao kukosa uzalendo kwa nchi yao hivyo unaweza usitekelezeke.

"Katika uongozi wa serikali uliotangulia kulikuwa na utaratibu, kwamba kinachosemwa na kiongozi wa juu kama Pinda ni kama vile amri, lakini wakati huu ni zaidi, tunasubiri tuone utekelezaji wa ahadi hizo sasa," alisema.

Akichangia hoja, Mkurugenzi wa Asasi ya kiraia ya utoaji elimu kwa umma juu ya umuhimu wa kutambua haki za kila raia, Dr.Asha Bisemboy, alisema wazo na lengo la Pinda ni hatua ya awali inayoonyesha kuwapo kwa fikra za mabadiliko vichwani mwa wakuu wa nchi lakini akaonya utekelezaji wake uanze haraka kwa maslahi ya nchi.

Hata hivyo, Dk.Bisembo hakusita kuonyesha shaka yake juu ya utekelezaji wa dhamira hiyo, kutokana na utamaduni wa serikali uliojengeka kwa miaka mingi wa kila kiongozi wa idara ya serikali kutaka kutembelea gari la bei kubwa bila kuangalia mustakari wa nchi.