Sakata la kunyimwa misaada MCC kuna vibaraka

10Apr 2016
J.M. Kibasso
Nipashe Jumapili
Sakata la kunyimwa misaada MCC kuna vibaraka

SIKU chache baada ya kuripotiwa kuwa Bodi ya Wakurugenzi wa Shirika la Changamoto za Milenia (MCC) la Marekani, limeinyima Tanzania misaada wa Dola milioni 472, karibu Shilingi trilion moja,

Rais wa Marekani, Baraka Obama

Umoja wa Ulaya (EU) pia uliibuka na kutangaza nia ya kufuta msaada wa Dola milioni 622, karibu Shilingi trilion 1.36 za msaada kwa Tanzania.

Ilielezwa kuwa EU inataka kufuata nyayo za Marekani kwa kile walichodai kusikitishwa nacho ambacho ni namna uchaguzi wa marudio Zanzibar ulivyofanyika hapo Machi 20, mwaka huu baada ya uchaguzi mkuu wa Octoba 25, mwaka jana kufutwa lakini pia na suala la sheria ya mtandao.

Taarifa hizi zimezidi kuiweka serikali ya Rais John Magufuli, njia panda. Ijapokuwa Waziri wa Mambo ya Nje, Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Kikanda na Kimataifa, Balozi Augustine Mahiga, alishaweka wazi msimamo wa serikali kusikitishwa na maamuzi hayo.

Balozi Mahiga alinukuliwa akisema; suala la Zanzibar liliendeshwa vizuri kwa kuwa lilitoa nafasi ya mazungumzo kwa pande zote na kwamba hakuna mwenye uwezo wa kuingilia masuala ya uchaguzi, serikali na mambo ya ndani visiwa humo, kwa kuwa wana katiba na hata Rais Magufuli alikuwa mwangalizi.

Pamoja na majibu haya, bado wadau wengi wanajiuliza maswali; je, kwanini mataifa haya ya nje yamekuja na kasi hii ya kushtukiza kuiandama Tanzania! Watu gani wako nyuma ya pazia?

Hakuna aliyetarajia kuiona Tanzania iliyokuwa ikisifika hasa kwenye utawala wa kidemokrasia tangu enzi za Baba wa Taifa Mwalimu Julius Nyerere, Marais wastaafu Ali Hassan Mwinyi, Benjamini Mkapa na Jakaya Kikwete, eti ifutiwe misaada mithili ya mbwa koko aliyeingia katika jumba la ibada.

Itakumbukwa kwamba Rais mstaafu Kikwete, ndiye alikuwa kiongozi wa kwanza kutoka barani Afrika kukaribishwa Ikulu ya Marekani na Rais Obama. Tangu hapo Kikwete alifanya ziara nyingi nchini Marekani kiasi kwamba hata nchi nyingine zikaanza kushtukia urafiki huo wa karibu wa viongozi wa mataifa haya.

Imekuwaje Tanzania iliyokuwa karibu sana na Marekani, ghafla mahusiano yanaharibika kwa kasi hiyo kulikoni? Wadau wengi wameshtushwa na hali hii ambayo haikutarajiwa kutokea. Wapo wanaojiuliza je, kundi gani linachochea mataifa haya na sababu ni nini mpaka wamefika uamuzi huo?

Hata hivyo, baadhi ya wanasiasa waliozungumza na safu hii wanaona kuwa Watanzania wasidanganyike kwani inajulikana siasa za ndani na nje ya nchi hii, hata siku moja haijatokea Tanzania ikakumbana na vikwazo vya kushtukiza vya mataifa wahisani kiasi hiki.

Ni wazi kuna watu mashuhuri ndani na nje ambao wanachangia kuichafua serikali ya Magufuli mbele ya mataifa haya. Hawa ni masalia ya vibaraka ni vyema wasiwafumbiwe macho, washughulikiwe.

Wachambuzi wengine wanaona nchi inapoteza umaarufu nje kwasababu ya kundi la watu ambao wamestushwa na kasi ya mafanikio ya serikali ya Rais Magufuli katika kutumbua majipu.

Wameanza kutumia mwanya wa Rais Magufuli kutotembelea nchi za nje kujenga hoja kwamba eti anayadharau mataifa hayo. Hivyo wanatumia uzoefu wao kuzishawishi nchi hizi wampe adhabu ya kumsaidia kwenye misaada ya maendeleo na huduma za jamii.

Inaelezwa kuwa baada ya Rais kuamua kutoondoka nchini kwa safari za nje, baadhi ya vigogo wametumia mwanya huo kudhoofisha serikali yake nje ya mipaka.

Lipo kundi la watu mashuhuri ndani na nje ya serikali ambao wameamua kupambana na serikali ya sasa baada ya kubaini maslahi yao yako hatarini endapo Rais Magufuli ataendelea kuungwa mkono katika falsafa yake ya “kutumbua majipu” kwa maana nyingine, hii ni vita ya ndani kwa ndani.

Mtu yeyote mwenye akili timamu hawezi kushangazwa na shinikizo hili. Haijawahi kutokea Tanzania ikasusiwa na wahisani kwa kishindo kama ilivyotokea nyakati hizi ni lazima tukiri kwamba upo mkono wa watu wazito nyuma ya pazia.

Hapana budi kwa serikali kujitokeza wazi na kuwaumbua watu hawa. Kwa bahati nzuri Watanzania walio wengi na ambao ndiyo wapiga kura, wanamuunga mkono Rais Magufuli kwa asilimia 85, kwa mantiki hiyo, Rais akiamua kuwaumbua vibaraka hawa hadharani, jamii kila kona ya nchi itashangilia.

Enzi za serikali ya kikoloni pia hali kama hii ilijitokeza na ilijitahidi kadri ilivyoweza kuwatumia baadhi ya machifu kuwa chombo cha kuzuia uenezaji wa TANU.

Mwaka 1957, serikali ya kikoloni iliunda Baraza la Machifu wa Tanganyika Territorial Convention of Chiefs. Kwa kuwatumia machifu, serikali ya kikoloni ilitegemea kuwagawa Watanganyika kwa misingi ya ukabila ili kuweza kutawala wananchi kwa urahisi zaidi.

Hawa vibaraka ni watu hatari wanacheka, kula na kuzungumza lakini si wema. Hapana budi kufuatilia nyendo za watu hawa. Atambue kwamba “kucheka na nyani mwishowe ni kuvuna mabua. Ndiyo maana nimesema masalia ya vibaraka wa wakoloni bado wapo nchini, wamulikwe mapema, wadhibitiwe.
Mawasiliano: 0713 399 004/0767 399 004, jmkibasso@gmail.com.