Nidhamu ya wachezaji Simba 'ziro'

11Apr 2016
Somoe Ng'itu
Dar
Nipashe
Nidhamu ya wachezaji Simba 'ziro'

KIMAHESABU, Simba iko kwenye mbio za ubingwa wa bara msimu huu. Lakini nyuma yake, timu hiyo ya Msimbazi ina shida. Nidhamu ya wachezaji ni tatizo.

msemaji wa simba, haji manara.

Kama nidhamu itaendelea kukosekana, hatuwezi tena kusema; 'Simba iko kwenye mbio za ubingwa'.
Alianza beki Hassan Isihaka aliyeshindwa kulinda kinywa chake na kutoa kauli isiyopendeza kwa kocha wake, Jackson Mayanja.

Isihaka: "Alimuuliza kocha wake, kwanini hakupanga kwenye mechi dhidi ya Simba na leo anampanda kucheza dhidi ya Stand United?" Aliingilia mamlaka ya kocha, hakuwa sahihi.

Simba hawakufurahishwa, wakamsimamisha kwa muda usiojulikana na hiyo ilikuja baada ya kuomba msamaha.

Huku kesi ya Isihaka ikiwa haijasahaulika, beki mwingine wa timu hiyo, Abdi Banda naye aliandika ujumbe katika akaunti yake ya facebook akimlaumu Mayanja kwamba anapanga wachezaji kwa upendeleo na si kwa kuangalia viwango.

Banda katika ujumbe wake alieleza kwamba anamkumbuka aliyekuwa kocha wa timu hiyo Muingereza Dylan Kerr ambaye alidai kwamba alikuwa akipanga wachezaji bila upendeleo.

Huku sakata la mchezaji huyo bado halijaamuliwa, wachezaji wawili wa kimataifa, mshambuliaji Hamisi Kiiza na beki Juuko Murshid raia wa Uganda nao wamepitiliza siku za ruhusa walizopewa kwenda kuitumikia timu yao ya taifa.

Siku waliyotakiwa kurudi Dar es Salaam hawajarejea na kocha kulazimika kuwaondoa kwenye programu yake ya mazoezi.
Msemaji wa Simba, Haji Manara alisema wachezaji hao raia wa Uganda watakabili na adhabu kwa vile walichofanya ni utovu wa nidhamu.

"Ndani ya Simba tumeshawaeleza wachezaji hakuna ambaye ni bora zaidi ya mwenzake, kila mchezaji ana haki sawa na mwenzake, nidhamu inatakiwa ifuatwe ndani na nje ya uwanja," alisema Manara.

Manara alisema nyota hao walipewa ruhusa ya siku tano, kinyume chake waliendelea kubaki Kampala wakati wanafahamu kuwa timu inakabiliwa na mechi ngumu za Kombe la Shirikisho na mbio za kuusaka ubingwa wa Bara ambao unashikiliwa na Yanga.

"Hatujui kwa nini wamechelewa, wachezaji wa Afrika Mashariki wanapenda kutengeneza migogoro na klabu zao, wenzao wa Ulaya huwa hawafanyi makosa kama haya, ukipewa siku tano, hawazidishi, hii ni sawa na njama za kutaka kuhujumu kikosi," alisema Manara.

MAYANJA AFUNGUKA
Kocha huyo wa zamani wa Kagera Sugar na Coastal Union alisema uamuzi wa mchezaji kuanza kwenye kikosi cha kwanza uko mikononi mwake na hiyo inatokana na uzito wa kila mchezo.

Mayanja alisema pia anapanga timu kwa kuangalia mazingira ya timu pinzani na kiwango cha mchezaji alichokionyesha kwenye mchezo uliopita au mazoezini.

Mganda huyo alisema hawezi kumpa nafasi mchezaji ambaye hakufanya mazoezi.
"Nidhamu ndiyo msingi wa kila jambo, huwezi kupata mafanikio kama huna nidhamu, hata mimi (Mayanja) napaswa kufanya kazi kwa nidhamu," alisema Mayanja.

Aliongeza ataendelea kushikilia msimamo wake wa kuwapanga wachezaji waliofanya mazoezi.

AVEVA ANENA
Rais wa Simba, Evans Aveva, alisema wanajipanga kuhakikisha wanashinda mechi zao ili waweze kutimiza ndoto za kuwavua Yanga ubingwa msimu huu.

"Tulishawahi kutwaa ubingwa katika hali isiyotarajiwa, tunaomba Mungu pia tufanikiwe msimu huu," Aveva alisema.
Simba inaongoza msimamo wa ligi kuu ikiwa na pointi 57, wakifuatiwa na Yanga na Azam FC