Uchunguzi uliofanywa na Nipashe kwa siku kadhaa, umebaini kuwapo kwa tatizo kubwa la udanganyifu ikiwamo kuuzwa kwa vyeti bandia vya kumaliza elimu ya sekondari; vinavyoonyesha kuwa vimetolewa na Baraza la Mitihani la Taifa (Necta) na kusainiwa na aliyekuwa Katibu Mtendaji wa baraza hilo, ambaye sasa ndiye Waziri wa Elimu na Mafunzo ya Ufundi, Profesa Joyce Ndalichako.
Uchunguzi huo umebaini kuwa vyeti bandia vya NECTA huuzwa kwa bei poa ya kuanzia Sh. 50,000.
Aidha, kuna vyeti bandia vya kuhitimu vyuo vya ngazi mbalimbali ya elimu ambavyo huwawezesha baadhi ya 'wasomi' hao kupata ajira licha ya kutokuwa na sifa.
Kupitia uchunguzi wake huo, Nipashe pia imebaini kushamiri kwa ‘biashara’ ya kuuza tafiti zenye mada mbalimbali kwa wanafunzi wa fani mbalimbali wa vyuo vya elimu ya juu.
Kuna vyuo vikuu na vyuo vikuu vishiriki zaidi ya hamsini nchini.
Tafiti hizo za kununua huwapa nafasi wahitimu kuwa na madaraja ya juu (GPA) wasiyostahili. Wastani wa gharama kwa kila utafiti hutegemeana na mtoaji wa huduma hiyo, ingawa Nipashe imebaini kupitia kwa wauzaji wawili wa tafiti hizo kuwa kila sura (chapter) hutozwa Sh.120,000, hivyo kwa sura sita huwa ni Sh.720,000.
Katika uchunguzi huo, Nipashe imebaini pia vitendo vya udanganyifu katika elimu vimeenea pia katika elimu ya msingi.
Baadhi ya wanafunzi hupewa majibu ya mitihani mapema kupitia njia mbalimbali na hivyo kupata alama za juu; lengo kubwa likiwa ni kuipa sifa shule husika ili ivutie wanafunzi wengi zaidi na kutoza ada kubwa kwa nia ya kunufaisha waendeshaji. Mtindo huo pia hutumika kulinda ‘vibarua’ vya walimu hasa wa shule za serikali, ambao ajira yao huwa shakani katika baadhi ya maeneo pindi shule zao zinapofanya vibaya.
“Kwakweli hali ni mbaya. Hakuna kulikosalimika, kuna watu wanafanya udanganyifu kuanzia shule ya msingi hadi vyuo vikuu. Serikali isipofanya jitihada maalumu za kuzuia hali hii kwa kushirikiana na wadau wa elimu, ni wazi kwamba taifa letu litaelekea shimoni,” mmoja wa wataalamu wa elimu aliiambia Nipashe katikati ya wiki.
“Madhara ya kuwa na hali hii ni makubwa kwa taifa. Kila mwaka tutakuwa tukizalisha wataalamu bandia katika sekta mbalimbali. Watu watakuwa na vyeti bandia vyenye ufaulu mzuri sana lakini kichwani hawana kitu. Hii ni hatari,” mchambuzi mmoja wa masuala ya elimu aliiambia Nipashe.
UDANGANYIFU UNAVYOFANYIKA
Katika uchunguzi wake, Nipashe imebaini kuwa zipo aina nyingi za udanganyifu kulingana na ngazi husika, kwa maana ya shule ya msingi, sekondari na vyuoni.
Nipashe imebaini kuwa njia za kuvujisha majibu ya mitihani kwa watoto wa shule ya msingi zipo nyingi, baadhi huhusisha walimu na hata wazazi.
Kupitia mahojiano maalum na baadhi ya walimu walioomba kuhifadhiwa kwa majina yao, Nipashe imebaini kuwa miongoni mwa njia tatu maarufu zinazotumika ni kuwakaririsha majibu ya mitihani watahiniwa wote ikiwa ni muda mfupi kabla ya kufanyika kwake, kuwatumia watoto wenye uwezo mkubwa darasani kuwasaidia wenzao kwenye chumba cha mtihani na walimu kufanya mitihani hiyo na kuwapa watoto majibu kwa utaratibu unaowahusisha pia wasimamizi watokao nje ya shule husika.
“Hii ya kuwakaririsha watoto majawabu ya mitihani hufanyika kiujanja sana kuelekea karibu na kipindi cha mithani. Baadhi ya shule huwaandalia watahiniwa programu maalum ya kujiandaa na kupitia mpango huo, watoto hukaririshwa majawabu kwa namna ambayo wakati mwingine siyo rahisi kwao (watoto) wala wazazi kujua ni kitu gani kinaendelea,” chanzo kimoja kiliiambia Nipashe.
“Kikubwa hapa huwa ni kuwakaririsha majibu kiujanja siku chache kabla ya mitihani ya taifa ambayo baadhi ya walimu hutumia mbinu zao kuipata mapema, lengo likiwa ni kuipa sifa shule kwa kuongeza ufaulu na mwishowe kuvutia wanafunzi wengi zaidi.
"Hata hivyo, ieleweke kwamba siyo shule zote zenye utaratibu wa kuwa na kambi hufanya vitendo hivyo. Ni baadhi tu,” chanzo kilisemaq zaidi.
Aidha, ilielezwa kuwa katika shule za msingi za serikali, wapo baadhi ya walimu na wakuu wao wa shule hushiriki mbinu chafu za kusaidia ufaulu mzuri kwa lengo la kulinda maslahi yao kikazi.
Wapo walimu wakuu katika baadhi ya shule hushushwa vyeo na walimu wengine kuhamishwa vituo vya kazi kutokana na shule zao kufanya vibaya kwenye mitihani ya taifa.
Kama ilivyo katika elimu ya msingi, Nipashe imebaini kuwa udanganyifu wa mitihani katika shule za sekondari huhusisha pia njia ya kuvujisha maswali ya mitihani muda mfupi kabla watahiniwa hawajaifanya na matumizi ya vyeti bandia.
“Katika badhi ya shule, hizi kambi maalum kwa ajili ya wanafunzi wanaojinadaa na mitihani ya taifa hubadilika kuelekea siku za mitihani kwa kujihusisha zaidi na uvujishaji wa maswali na kuyafanyia kazi kabla ya kuingia kwenye vyumba vya mitihani… pia kuna uvujishaji mwingine hauhitaji ushiriki wa uongozi wa shule bali wanafunzi wenyewe,” chanzo kilieleza.
Nipashe ilibaini pia kuwapo kwa njia ya ununuzi wa vyeti bandia, vikionyesha wahusika wamemaliza sekondari kabla ya mwaka 2008.
Mwandishi alishuhudia cheti kilichonunuliwa kwa Sh. 50,000 (pichani) na kuonyesha kuwa mhusika alimaliza kidato cha nne mwaka 2007 katika sekondari ya Mwanzi iliyopo Manyoni, Singida, huku aliyekisaini akiwa ni Katibu Mtendaji wa NECTA wakati huo, Prof. Ndalichako.
Cheti hicho ambacho jina lililotumika kwa ajili ya mmiliki wake tunalihifadhi, kinaonyesha kuwa mhusika alipata daraja la nne, akiwa na ufaulu wa alama ‘D’ kwa masomo ya Civics, History, Geography, Kiswahili na English, huku pia akipata alama ‘F’ kwa masomo ya Basic Mathematics na Biology. Pia kina alama karibu zote za usalama za Necta pamoja na muhuri wa moto.
“Kama unavyoona, cheti hiki hakitofautiani sana na cheti cha kidato cha nne kilichotolewa na Necta miaka hiyo. Umakini mkubwa unahitajika kubaini kuwa ni cha bandia kwa sababu kinafanana kwa kiasi kikubwa na vyeti halisi," kilisema chanzo chetu kiliiambia Nipashe.
“Kimepatikana maeneo ya Tabata (jijini Dar es Salaam) baada ya siku mbili tu tangu kukamilisha malipo na kimemsaidia sana mhusika.” Aidha, Nipashe imebaini kuwapo kwa udanganyifu mkubwa katika vyuo vya elimu ya juu.
Mbali ya baadhi ya watu kutumia vyeti bandia walivyonunua kwa bei poa vikionyesha kuwa wamemaliza katika vyuo vya elimu ya juu, lipo pia tatizo la kuwasilishwa kwa utafiti usiofanywa na wanafunzi husika bali kukamilishwa kwa kununua kutoka kwa ‘wajasiriamali’ wanaojihusisha na biashara hiyo.
Kwa kawaida, mfumo wa mitihani kwa wanafunzi wanaohitimu vyuoni huhusisha majumuisho ya mazoezi ya darasani (course works), mitihani ya mwisho maarufu kama University Examination (UE) na tafiti mbalimbali ambazo huwa ni lazima kukamilishwa na kila mhitimu.
Hata hivyo, imebainika kuwa wahadhiri wa baadhi ya masomo huwabeba wanafunzi kwa kuwapatia alama wasizostahili katika ‘course work’ zao kutokana na sababu mbalimbali zisizokuwa za kitaaluma.
Wahadhiri hao hutoa upendeleo huo kwa utashi binafsi, na pia wingi wa wanafunzi darasani ambao huwalazimu kuwawekea alama baadhi ya wanafunzi kwa kukadiria ili kuendana na shinikizo la kuwasilisha matokeo kwenye idara za taaluma.
Nipashe imebaini kuwa kuwapo kwa ‘biashara’ haramu ya kuwafanyia tafiti wanafunzi ndiyo kansa kubwa zaidi.
Biashara hiyo ndiyo kansa kubwa zaidi kwa sababu inahusisha wanafunzi wa stashahada (diploma), shahada ya kwanza (bachelor degree), stashahada za uzamili (postgraduate diploma) na shahada za uzamili (masters degree).
Katika kudhihirisha kuwa tatizo hilo limekuwa kubwa zaidi, Nipashe ilifanikiwa kuona matangazo kadhaa ya wauzaji wa tafiti kwa wanafunzi yakitolewa kwenye magazeti na namba za simu za wahusika zikiwekwa wazi.
Wanafunzi huhimizwa kwenda kwa wamiliki wa namba hizo ili warahisishiwe kazi ya kuandaa mapendekezo ya tafiti hizo, na pia kuandaa ripoti zake kwa ukamilifu ili wakapate alama za juu kati ya A na B+.
Nipashe iliwasiliana na baadhi ya wafanyabiashara ya kuuza ‘tafiti’ kupitia namba za simu wanazoziweka kwenye matangazo yao na kujitambulisha kama mwanafunzi ili wamhudhumie.
Tangazo mojawapo la watu hao, ambao zaidi hutumia matangazo madogo madogo (classified) lilisomeka:
“Je, unafanya Masters au Postgraduate lakini unahangaika na research proposal, report, concept paper na dissertation? Tupigie kwa simu (namba tunazihifadhi).”
Mwandishi wa Nipashe alipowasiliana na namba hiyo aligundua shughuli hiyo sasa ni kama rasmi kwani wahusika hujitambulisha kwa uwazi, pasi na hofu yoyote, bila shaka wakiamini kuwa wanachokifanya ni jambo jema katika jamii.
“Njoo ofisini kwetu Magomeni Mapipa ili tuzungumze nawe… tunafanya researches (tafiti) nzuri zinazowasadia wahitimu kupata alama za juu kama B+ na A," alisema mtu aliyejibu simu ya Nipashe kuhusiana na mpango huo wa kufanyiwa ‘research’.
“Karibu sana. Gharama zetu ni nafuu mno kulinganisha na hadhi ya cheti utakachokipata baada ya kumaliza shule yako.
"Tumeshawasaidia watu wengi sana na sasa wameajiriwa kwenye taasisi mbalimbali kubwa. Njoo tukusaidie, tena tutakamilishia kazi yako ndani ya muda mfupi sana.”
Kuhusu ufafanuzi kuhusiana na gharama, mwandishi wa Nipashe alielezwa na wauzaji hao wa tafiti kuwa kila sura moja (chapter) hutozwa Sh.120,000 na hivyo, gharama huongezeka kulingana na mahitaji ya mwanafunzi; kwa sura sita ikiwa ni Sh.720,000.
Katika mazungumzo yake ya ana kwa ana na mwandishi wa Nipashe, mmoja wa wafanyabiashara ya kufanyia wanafunzi utafiti alikiri kuwa jambo analolifanya siyo jema kwa taifa, na anaamini linachangia kwa kiasi kikubwa kuwapo kwa baadhi ya wahitimu wenye vyeti vizuri lakini wasiokuwa na sifa kiutendaji.
Aidha, alisema biashara hiyo anayoifanya kwa zaidi ya miaka 15 sasa inamuingizia kipato kizuri kwa sababu wanafunzi wavivu na wanaopenda kubebwa kwa kufanyiwa tafiti ni wengi.
Hata hivyo, alisema anadhani ipo haja kwa serikali kushirikisha wadau wa elimu katika kutafuta namna bora ya kuzuia udanganyifu huo.
Akizungumzia ukubwa wa tatizo, mfanyabiashara huyo wa tafiti alisema muhula wa 2014/2015 peke yake alikamilishia kazi za ‘research’ za wanafunzi 26 wa shahada ya kwanza na uzamili kutoka katika vyuo mbalimbali nchini na kuanzia mwaka jana hadi sasa, tayari ameshawahudumia wanafunzi 11.
“Kama mimi peke yake ninawasaidia wanafunzi wa idadi hiyo, jiulize ukichanganya na wengine wanaotoa huduma kama yangu kutakuwa na wanafunzi wangapi wanaohitimu kwa kutumia tafiti zisizokuwa zao?" Aliuliza.
"Hili jambo linapeleka nchi pabaya."
Mjasiriamali huyo alisema zinahitajika nguvu za pamoja kudhibiti na siyo mtu mmoja kuacha halafu wengine wakaendelea kuingiza fedha.
NECTA, TCU WAKIRI KUNA TATIZO
Alipoulizwa kuhusiana na tishio la kuwa na wataalamu bandia kutokana na udanganyifu katika elimu, ikiwamo wanafunzi kuandaliwa tafiti, Katibu Mtendaji wa Tume ya Vyuo Vikuu (TCU), Profesa Yunis Mgaya, alisema udanganyifu unaofanywa na baadhi ya wanafunzi kwenye vyuo vikuu nchini ni janga linalotishia ubora wa kiwango cha elimu.
Alisema jamii inapaswa kusimama pamoja katika kupiga vita vitendo hivyo kwa sababu ni vibaya na madhara yake ni makubwa kwa taifa.
Kwa kuanzia, Prof. Mgaya alisema wanafunzi wanaofanya vitendo hivyo wanapaswa kuitwa ‘mafisadi wa elimu’.
“Tumeshafahamishwa jambo hilo… na tunafuatilia. Wanafunzi hao (wanaoshiriki udanganyifu) wanapaswa kuitwa mafisadi kwa sababu wanapata elimu ambayo hawajaitolea jasho,” alisema Prof. Mgaya.Prof. Mgaya alisema changamoto ya kuwapo kwa udanganyifu katika elimu ipo duniani kote na siyo Tanzania peke yake hata hivyo.
Aidha, alisema udanganyifu mwingine wa wanafunzi huchangiwa pia na wahadhiri wanaosimamia tafiti (supervisors) kwa sababu haingii akilini ni kwa namna gani wanaletewa ‘draft’ ya kwanza ya utafiti hadi ya mwisho ikiwa haina kosa lolote kubwa na bado wanazipitisha bila kushtushwa na hali hiyo isiyokuwa ya kawaida, katika ukamilishaji wa tafiti.
Alisema jambo kubwa wanaloweza kulidhibiti hivi sasa ni wizi wa taarifa za kiutafiti (plagiarism) ambapo TCU, kwa kushirikiana na baadhi ya vyuo vikuu nchini kama Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM), Chuo Kikuu Mzumbe na Chuo Kikuu Huria Tanzania (OUT), wameanzisha programu maalum ya kuzuia vitendo hivyo iitwayo Turnipin.
“Hii (Turnipin) humsaidia msimamizi wa tafiti kujua kama (tafiti) imeshawahi kuandikwa na wengine au la,” alisema.
“Binafsi niliwahi kumkamata mwanafunzi mmoja wa masters (shahada ya uzamili) wakati nikiwa UDSM, ambaye alikuwa amenakili kazi… alilazimika kurudia mwaka wake wa masomo,” alisema Prof. Mgaya.
Aidha, Prof. Mgaya alisema ni vizuri jamii ikaanza kuwajenga watoto kujitegemea katika elimu kuanzia ngazi ya awali kwa sababu hivi sasa, wapo wanafunzi ambao makuzi yao yote wamekuwa wategemezi (katika elimu), wakifanyiwa kazi zao na watumishi wa ndani wakati wakiwa chekechea na sasa hata ukubwani hujikuta wakiendelea kuwa wazembe kwa kuwapa ujira wengine ili wawakamilishea tafiti zao.
“Hili jambo haliruhusiwi… ni kosa kubwa kwa mwanafunzi,” alisema Prof. Mgaya.Akizungumzia vitendo hivyo, Katibu Mtendaji wa NECTA, Dk. Charles Msonde, alikiri kuwapo kwa vyeti bandia vinavyohusisha vyeti vilivyotolewa miaka ya nyuma, kuanzia mwaka 2007 kurudi nyuma.
Akieleza zaidi, Dk. Msonde alisema hadi kufikia mwaka 2007, NECTA ilikuwa ikitoa vyeti vya wahitimu wa sekondari bila ya kuwa na picha ya mwanafunzi husika na hivyo kuwapo kwa mwanya kwa wadanganyifu kuchapisha vyeti bandia.
Dk. Msonde alisema kuanzia mwaka 2008, NECTA ilianza kutoa vyeti vyenye picha za watahiniwa na sasa tatizo hilo la kudurufu vyeti bandia limepungua kwa kiasi kikubwa.
“Ni kweli kuna udanganyifu katika vyeti vya elimu ya sekondari. Lakini ilipofika mwaka 2008, udanganyifu huo ukaanza kupungua… kwakweli tunajitahidi kupambana na udanganyifu.”
Kuhusiana na udanganyifu katika mitihani, Dk. Msonde alisema tatizo hilo lipo pia lakini wamejitahidi kulidhibiti kwa kiasi kikubwa na takwimu zinathibitisha hivyo.
Alisema mwaka 2011, waliwakamata wanafunzi zaidi ya 9,000 waliokuwa wamefanya udanganyifu katika mitihani yao ya mwisho, lakini mwaka uliofuata wa 2012, idadi ya wadanganyifu ilipungua hadi kufikia wanafunzi 263 na mwaka 2013 walibainika wanafunzi 13.“Mwaka 2014 hakukuwa na mwanafunzi aliyekutwa na kosa hilo na mwaka jana (2015), alipatikana mwanafunzi mmoja,” alisema.
WALIMU, WAHADHIRI WAELEZA YAO
Akielezea tatizo la udanganyifu katika elimu, Mwalimu Mkuu wa Shule ya Sekondari Rising Bird, Ephraim Solomoni, alisema ni kweli hivi sasa kuna baadhi ya shule hutumia mbinu chafu katika kufaulisha wanafunzi wao na hilo siyo jambo jema kwa taifa.
Akieleza zaidi, Solomoni alisema baadhi ya waendeshaji wa taasisi za elimu huchukulia elimu kuwa ni biashara na matokeo yake, kwa kiasi kikubwa wanafunzi hutafutiwa kila kitu na kufundishwa namna ya kufaulu mitihani ili shule ipate sifa na kukuza biashara, na siyo kwa lengo la kuhakikisha kuwa malengo ya kielimu yanatimizwa.
Mkufunzi kutoka Chuo cha Mtakatifu Augustine (SAUT), Prof. Mwesiga Baregu, alisema hivi sasa taifa lipo katika hali mbaya ya kutengeneza bomu kupitia vijana wasioiva kielimu bali kuwa na vyeti vye alama nzuri za ufaulu.
Alisema tatizo la udanganyifu vyuoni ni kubwa na kwamba kuna haja serikali ikaandaa timu ya wataalamu watakaotafuta chanzo na kutoa mapendekezo juu ya namna ya kuboresha mfumo wote wa elimu nchini.
Mhadhiri wa Shule Kuu ya Uandishi wa Habari na Mawasiliano ya Umma Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (SJMC), Dk. Ayoub Rioba, alisema mfumo wa elimu nchini umeingiliwa na watu ambao wanapenda mambo ya mkato na hiyo ndiyo sababu ya kuwapo kwa vitendo vya udanganyifu.
Dk. Rioba alitolea mfano tatizo la kuwapo kwa wahadhiri wasiokuwa makini katika kusimamia tafiti, hasa wale wanaotoa miongozo kwa mawasiliano ya mtandao tu (e-mail) na hivyo kutoa fursa ya kupitisha kazi zisizokuwa za wanafunzi husika.
“Kuna baadhi ya vyuo, Profesa ama Dokta anakuwa na research (tafiti) za wanafunzi 20 hadi 30… hili nalo ni tatizo kwa sababu hizi ni nyingi sana na hivyo hata usimamizi wake unakuwa wa ubabaishaji,” alisema.
Aidha, Rioba alisema kuna baadhi ya walimu wanaoshirikiana na wamiliki wa shule binafsi kushiriki uvujishaji wa mitihani kwa wanafunzi wao kwa madhumuni ya kuiletea sifa shule husika na hilo pia ni tatizo.
Mkuu wa Chuo Kikuu Kishiriki cha Elimu cha Dar es Salaam (DUCE), Profesa Willium Anangisye, alisema hivi sasa taifa linakwenda mwelekeo mbaya kutokana na vitendo vya udanganyifu kwa sababu zipo taarifa kuwa wanafunzi hupata alama za juu kama B+ na A kwa tafiti walizofanyiwa.
“Sina uhakika na wala sijawahi kuona au kumkamata mwanafunzi aliyeiba research (utafiti) ya mtu au ameandikiwa… ila nimewahi kusikia jambo hilo," alisema Prof Anangisye. "Kiukweli, kama hayo mambo yanafanyika, tutakuwa na wakati mgumu wa kutengeneza wasomi wenye manufaa kwa taifa.”
Alisema njia mojawapo ya kukabili tatizo hilo ni kuimarishwa kwa mfumo wa elimu kuanzia ngazi ya awali ili wanafunzi wajengewe uwezo wa kuelewa wanachofundishwa na kuchukia udanganyifu.










