Dk. Mpango anaongoza shughuli hiyo ya upandaji miti katika jiji la Dodoma katika maeneo ya Ihumwa na Msalato, ikiwa ni katika kusherehekea maadhimisho ya Mapinduzi ya Zanzibar yaliyofanyika wiki jana.
Anasema, miaka 59 ya Mapinduzi Matukufu ya Zanzibar, yanapaswa kutumika kama chachu ya kuifanya Tanzania kuwa ya kijani na kurekebisha yale yote yaliofanyika katika kuharibu mazingira.
“Tumesisitiza upandaji miti mitatu kwa kila nyumba, walau miwili ya matunda na mmoja wa kivuli hii ni lazima tufanye tuliambiwa Dodoma ni kama jangwa hivi siyo kweli,” anasema Dk. Mpango.
“Sasa nawataka wakuu wa mikoa, wilaya na wakurugenzi wa halmashauri na waziri ukasimamie kupanda miti sasa siyo hiari tena ni lazima,” Dk. Mpango anaongeza.
Aidha, Makamu wa Rais Dk. Mpango, anasisitiza ushirikishwaji wa sekta binafsi na wafanyabiashara katika upandaji na utunzaji miti na anazisihi familia kuongeza juhudi katika upandaji miti na usafi wa mazingira.
Anazitaka taasisi za serikali kupanda miti katika maeneo yao na kuhakikisha miti hiyo inaishi, pia akiwataka viongozi kuwa mfano katika shughuli hiyo ya upandaji na utunzaji miti kwa kuonyesha kwa vitendo.
Hapi anatoa maagizo kwa viongozi wa jiji la Dodoma, waratibu na kusimamia miti iliyopandwa, iishi na kupendezesha makao makuu ya nchi yanayopokea wageni wa ndani na nje ya Tanzania.
Anawataka kudhibiti masuala yote ya uchomaji moto maeneo yaliyopandwa miti, pamoja kukabiliana na changamoto ya uingizaji, pia upitishaji mifugo katika maeneo hayo.
Dk. Mpango anasema, kila mwananchi anawajibika kuimwagilia miti iliyopandwa, hususani wale wanaomiliki vituo vya mafuta na wanaozalisha tofali, akitoa wito kwa waandishi wa habari kutoa kipaumbele katika uelimishaji na kuhamasisha jamii juu ya upandaji miti na uhifadhi wa mazingira kwa ujumla.
Hapo inaendana na agizo lake kwa Wakala wa Misitu Nchini (TFS), kupitia upya utaratibu wa leseni za ukataji miti kwa ajili ya mkaa, ili kuokoa maeneo ambayo yana uoto na vyanzo vya maji.
WADAU MAZINGIRA
Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Rais Muungano na Mazingira, Dk. Selemani Jafo, anasema mipango ya uhifadhi wa mazingira imeshaanza kutekelezwa, ikiwamo kugawa maeneo yaliyopandwa miti kwa taasisi za serikali na binafsi kuzisimamia na kuhakikisha miti hiyo inaishi.
Dk. Jafo anamhakikishia Makamu wa Rais, kuwa shughuli za upandaji miti na kuitunza, itakuwa endelevu.
Mdau wa Mazingira na Waziri Mkuu Mstaafu, Mizengo Pinda, anatoa wito kwa wananchi kuzingatia utaratibu wakati wa upandaji wa miti ikiwamo kuandaa mazingira ya upandaji na kufuata maelekezo ya wataalamu ili kufahamu aina ya mti na mahali unapopaswa kupandwa.
Pinda anasema, Jiji la Dodoma linakabiliwa na upungufu wa mvua, hivyo ni vyema uchimbaji mashimo, pamoja na nafasi baina ya mti na mti ukawa wa kitaalamu zaidi, ili kuepusha miti hiyo kutofikia lengo.
Waziri Mkuu huyo mstaafu, anasema jamii ina wajibu mkubwa wa kusimamia na kutekeleza kwa makini yale yote yanayosababisha maisha ya binadamu kuwa salama ikiwamo upandaji wa miti.
Rosemary Senyamule, Mkuu wa Mkoa wa Dodoma, anasisitiza upandaji miti katika vyanzo vya maji upewe kipaumbele kimkoa, kwa kuanza na Bonde la Mzakwe ambalo limekuwa na changamoto ya ukuaji wa miti.
Senyamule anasema, wataalamu wamewezesha aina ya miti inayopaswa kupanda pamoja na kuweka mazingira yatakayookoa miti hiyo dhidi ya hatari ya moto.
“Sisi hapa kupitia ofisi ya Makamu wa Rais tunaendelea kusisitiza upandaji wa miti watendaji tutasimamia sheria kwa wale watakaoleta mifugo kula miti hii,” anasema Senyamule.
Mkuu huyo wa Mkoa, anawataka walimu wa shule za msingi kuhakikisha kila mwanafunzi anapoingia darasa la kwanza apewe mti mmoja wa kuutunza hadi hapo atakapohitimu darasa la saba lengo likiwa ni kuleta mabadiliko ya tabianchi.
Mkuu wa Wilaya ya Dodoma, Jabir Shekimweri, anawahakikisha kushirikiana na wadau mbalimbali katika usimamizi wa upandaji wa miti pamoja na kusimamia vyema programu ya soma na mti inafanikiwa.