Yanga hawakuhitaji kusubiri hadi mechi yao ya jana ugenini dhidi ya Mbeya City ili kutwaa ubingwa, shukrani kwa kichapo hicho cha mahasimu wao wa jadi.
Lakini Yanga walifanya nini hadi kutwaa ubingwa wakiwa na tofauti ya pointi 10 dhidi ya wanaoshika nafasi ya pili huku mechi mbili zikiwa zimebaki msimu kumalizika?
Lete RAHA imeainisha mambo makuu 10 yaliyoiwezesha Yanga kutwaa ubingwa msimu huu ambayo baadhi hayakufanywa vyema na klabu za Simba na Azam ambazo zilikuwa kwenye mbio za kuwania ubingwa msimu huu.
Mambo hayo yalikuwa kama nguzo ya mafaniko kwa klabu ya Yanga. Ifuatayo ni orodha ya mambo ambayo yalikuwa wakifanywa:
Kikosi bora
Ubingwa hao haukuja hivi hivi, uimara wa kikosi kwa kiasi kikubwa umechangia timu hii kufanya vizuri na kuweza kutwaa ubingwa. Kwenye kikosi chake kila idara ilionekana kuwa ni imara na yenye kujitosheleza.
Si kwenye safu ya Ushambuliaji tu walifanya kazi kubwa kwa kufunga mabao mengi bali hata kwenye safu ya kiungo ilimiliki mpira vyema kwa kuanzisha mashambulizi lakini pia kuzuia mashambulizi ya timu pinzani. Safu ya ulinzi nayo ilikuwa imara huku kocha akiwa na uwezo wa kubadilisha wachezaji mara kwa mara.
Uimara wa kikosi cha Yanga kwa msimu huu huwezi kuufananisha na uimara wa kikosi cha Simba au Azam.
Nidhamu
Ni dhahiri kuwa mafanikio huchangiwa na nidhamu bora. Yanga wamekuwa na nidhamu ya aina yake nje na ndani ya uwanja kwa msimu huu. Licha ya baadhi ya wachezaji kuadhibiwa kwa kadi za njano na wengine nyekundu, kikosi hiko kimekuwa tulivu.
Hali hii iko tofauti na mahasimu wao ambao kwa siku za hivi karibuni wamekuwa wakiwasimamisha wachezaji kutokana na utovu wa nidhamu. Simba iliwasimamisha Abdi Banda, Hassan Issihaka na Hassan Kessy kwa kile walichodai kuwa ni utovu wa nidhamu. Nidhamu ya wachezaji hao imechangia kwa kiasi kikubwa timu hiyo kushindwa kufika mbali.
Uongozi tulivu
Ni tofauti na hali iivyo Simba, Yanga wamekuwa wakiendesha mambo yao ya kiutawala vizuri kutokana na jinsi uongozi ulivyotulia na kujipanga.
Uongozi wa Yanga umechangia kwa kiasi kikubwa mafanikio ya timu hiyo kwa mwaka huu kwa kuwa wamekuwa wakitimiza mahitaji ya timu kwa wakati na kwa kuzingatia uendeshaji bora.
Wachezaji wa kigeni
Kama unafuatilia utabaini kuwa wachezaji wote wa kigeni wa Yanga kwa msimu huu wamekuwa na mchango mkubwa kwenye kikosi cha timu hiyo kutokana na jinsi walivyojituma.
Wachezaji hao wa kigeni ni Vincent Bossou (Togo), Donald Ngoma (Zimbabwe), Haruna Niyonzima (Rwanda), Thabani Kamusoko (Zimbabwe), Amissi Tambwe (Burundi), Youssouf Boubakar (Niger), Mbuyu Twite (Rwanda). Kwa uwezo na mchango wa wachezaji hao ambao wote wamecheza na kuthibitisha thamani zao, Yanga imetwaa ubingwa. Ni Youssouf pekee ambaye hakuwa na nafasi Yanga.
Wachezaji kadhaa wa kigeni wa Simba na Azam hawakupewa nafasi pengine kwa kuwa viwango vyao viko chini kuliko wazawa au kutokana na kuwa majeruhi. Raphael Kiongera, Briann Majwega na Emiry Nimubona hawakuwa na nafasi Simba wakifunikwa na wazawa kama Hassan Kessy, Ibrahim Ajib na Danny Lyanga, wakati Alan Wanga, Kipre Bolou na Didier Kavumbagu wa Azam walionekana kufunikwa na wazawa kama Himid Mao, Salum Aboubakar, Mudathir Yahaya na John Bocco.
Michuano ya kimataifa
Michuano ya kimataifa Klabu BIngwa Afrika na Kombe la Shirikisho Afrika ilikuwa chachu ya Yanga kufanya vyema msimu huu. Licha ya kutolewa kwenye Klabu Bingwa Afrika, Yanga walicheza Ligi Kuu kwa kupambana ili kujijengea nafasi kuwa kwenye michuano ya mwaka ujao.
Uwezo na hamasa ambayo timu hiyo imekuwa ikipata hata sasa inavyoshiriki kwenye Kombe la Shirikisho imekuwa chachu ya timu kupambana kwenye ligi na kwa hilo limefanikiwa.
Bajeti nzuri
Yanga ni moja ya timu ambayo ilikuwa na bajeti nzuri msimu huu ikitumia zaidi ya Sh. bilioni 1 kufikia sasa. Fedha hizo zimetumika kwenye uendeshaji wa timu na mpaka sasa timu hiyo imekuwa haikumbani na changamoto yoyote inapokuwa kambini au hata nje inapokuwa inasafiri kwenda kutimiza majukumu mbalimbali kama ya ligi na michuano ya kimataifa. Bajeti yao bora kwa timu imechangia kwa kiasi kikubwa kwenye mafanikio ya timu.
Maslahi ya wachezaji
Kama ni kitu kilichoisaidia Yanga kutwaa ubingwa basi ni kulipa mshahara wachezaji wake kwa wakati. Yanga wamefanikiwa hilo na wamekuwa hawakumbani na hali ya wachezaji kugoma au kucheza chini ya kiwango kushinikizwa kulipwa.
Yanga wamekuwa wakiwalipa wachezaji wao kwa wakati huku wakiwapa pia bonasi mbalimbali na pia wamekuwa wakiboresha mikataba ya wachezaji wao.
Benchi bora la ufundi
Kocha Pluijm ni kocha mwenye uwezo mkubwa na ameshathibitisha mara kadhaa. Alifanya hivyo pia alipokuwa akiifundisha Berekum Chelsea ya Ghana iliyotesa Afrika.
Na kitendo cha kumuongeza Juma Mwambusi, kocha aliyeijenga Mbeya City kuwa timu bora inayopigania ubingwa wa bara katika msimu wao wa kwanza kabisa kucheza Ligi Kuu mwaka jana, ilikuwa ni hatua nyingine kubwa ya kujenga benchi imara kabisa la ufundi Yanga.
Kocha msaidizi Mwambusi na kocha wa makipa, Juma Pondamali 'Mensah', wamechangia kuifanya Yanga kuwa timu bora nchini msimu huu.
Usajili
Yanga ilifanikiwa kwa kusajili wachezaji bora wa kigeni, lakini pia kwa kunasa majembe ya hapa nyumbani. Wengi wao wamekuwa na mchango mkubwa katika kuisaidia timu kufanya vizuri.
Wachezaji kama Paul Nonga, Haji Mwinyi, Matheo Antony na Malimi Busungu wamekuwa kwenye kiwango kizuri na hii imedhibitika pale walipopata nafasi. Usajili wa wachezaji wengi umekuwa na manufaa kwenye kikosi.
Mipango
Yanga ni moja ya timu yenye mipango mikubwa ndani na nje ya uwanja. Kwanza mashabiki wa timu hiyo wanatambua umuhimu wao kwenye timu kuwa ni kuipa sapoti timu hiyo.
Pia Yanga ilijipanga kwenye maandalizi ya timu kwa kutoa ulinzi kwa wachezaji wake lakini pia kwa kuwa na mazingira mazuri ya maandalizi kokote walipokuwa wakienda. Yanga walikuwa wakituma watu wake kwenda kutazama na kuona kuwa wapo kwenye sehemu salama kabla ya kikosi chake kuwasili.










