Picha hiyo ilikuwa na kichwa cha habari bunge ‘Live’.
Aidha, sambamba na tukio hilo la wabunge kujirusha moja kwa moja mitandaoni, Jumapili ya Mei Mosi, baadhi ya magazeti yalitoka na picha za baadhi ya wabunge wa kambi ya upinzani katika kurasa za mbele wakijirekodi na kurusha moja kwa moja wakati wakichangia hoja mbalimbali bungeni.
Tunaamini hizi ni sehemu tu ya picha nyingi kama hizo za wabunge kulazimika kujirusha ‘live’ kile wanachochangia baada ya serikali na uongozi wa bunge kuamua kuzuia vyombo vya habari kama luninga kurusha mijadala ya bunge moja kwa moja kama ilivyokuwa imezoeleka.
Aidha, tumesikia watu mbalimbali wakiwamo wanasiasa, wanahabari, viongozi wa dini na viongozi wakuu wa kitaifa waliostaafu kwa mfano Frederick Sumaye, wakilalamikia jambo hili.
Wengine wamekwenda mbali zaidi na kubainisha kwamba kuna uvunjifu wa katiba wakionyesha vifungu wanavyoona vinakiukwa na huku haki ya raia ya kupata habari ikipokwa wazi wazi na serikali ya awamu ya tano.
Matukio ya wabunge wa CCM na wale wa upinzani yaliyochapishwa na magazeti na yasiyochapishwa, ni kielelezo tosha kwamba bila kujali itikadi za vyama kitendo cha kuzuia kuonyesha bunge live kimewaudhi wabunge wengi kama kilivyowakwaza watu wengi.
Nasema hivi kwa sababu ni kitendo kinachominya uhuru wa raia kupata habari tena wazipate kwa wakati muafaka.
Nawaunga mkono wabunge walioonyesha kukerwa na wakachukua hatua kwa ubunifu wa kujirusha japo kunakuwa na ufinyu wa kuenea kwa habari yao kwa watu wengi.
Kwa bahati mbaya matukio wanayoyarusha hayawezi kusambaa vizuri kutokana na sababu zilizo wazi kama ukweli kwamba si wananchi wengi walio na uwezo wa kuwasiliana kwa kutumia mtandao wa intaneti.
Ili kuelewa kwanini watu wengi wanakerwa na zuio la vyombo vya habari kurusha matangazo ya bunge moja kwa moja ni vyema kwanza tukaangalia maana ya bunge na kwanini lipo na tufanye hivyo kwa kujikita katika muktadha wa maana pana ya utawala wa kidemokrasia.
Kwanza inabidi tutambue kwamba kuna aina au mifumo mbalimbali ya utawala duniani.
Kuna utawala wa kifalme, utawala wa kiimla au kidikteta, na kuna utawala wa kidemokrasia.
Ingawa aina hizi zinatofautiana katika misingi, staili na miundo yake, lakini zote zinanafana kwa jambo moja kwamba zote zimegawanyika katika sehemu kuu mbili yaani sehemu ya watawala na sehemu ya watawaliwa.
Wakati mwingine njia rahisi ya kuzipambanua aina hizi za utawala ni kwa kuangalia watawala na watawaliwa wanavyopatikana.
Katika mfumo wa utawala wa kifalme watawala utokana na familia moja ilyopewa hadhi ya kifalme, kwa hiyo anayezaliwa katika familia hiyo ujikuta yeye ni mtawala moja kwa moja bila kupigania wala kuomba kuwa mtawala.
Katika mfumo wa utawala wa kiimla au kidikteta, watawala hupatikana kwa mtu au kikundi kidogo cha watu kujiongezea madaraka na kufanya mambo nje ya mipaka waliyopewa na watawaliwa kwa makubaliano ya katiba.
Ili wafanikishe utawala wao, madikiteta hawa daima hutumia vyombo vya maguvu kama majeshi kuwatisha na kuwalazimisha watawaliwa wafuate wanachotaka wao.
Kwa upande wa mfumo wa utawala wa kidemokrasia, watawala hupatikana kwa kuchaguliwa na watawaliwa na utawala kulingana na madaraka waliyopewa na makubaliano waliyoafikiana na watawaliwa yaani katiba.
Katika hili, watawala hupendekeza taratibu nyingine za kuwasaidia katika utawala na huzipeleka kwa watawaliwa kupata baraka au idhini ya kuzitumia ambazo huitwa sheria na kanuni.
Kwa hiyo tunaona kwamba katika mfumo wa utawala wa kidemokrasia, watawala hawatakiwi kufanya lolote nje ya makubaliano kati yao na watawaliwa.
Kwa maana nyingine ni kwamba watawala hawaruhusiwi kufanya vitu nje ya katiba au sheria.
Ikitokea wakafanya kinyume na hayo basi wanakuwa wamejigeuza kutoka katika mfumo wa kidemokrasia na kujiigiza katika mfumo wa kidikteta kama tulivyo ainisha hapo juu.
Kwa tafakari nyingine tunasema rais kama mtawala mkuu (ana uwezo wa kuchagua watu wengine watakaomsaidia katika kutawala), hana madaraka zaidi ya aliyopewa kikatiba.
Na inatakiwa akitaka kufanya jambo nje ya taratibu arudi kwa watawaliwa kuomba idhini hiyo!
Kwa lugha rahisi zaidi ni kwamba rais wa Tanzania na serikali yake mathalani angehitaji kuomba ridhaa ya Watanzania ili kutunga sheria na kwa kuwa wote hatutokubaliana basi ingebidi tupige kura ili wengi waamue juu ya pendekezo lake.
Kusema kweli hayo ndiyo matakwa ya utawala wa kidemokrasia; na ili kurahisisha mambo na kuwawezesha watawala kufanya walichopanga basi ukawekwa muundo wa uwakilishi.
Kwamba kwa kuwa ni vigumu watawaliwa kupatikana kwa ujumla wao kuamua mambo, basi wachaguane katika makundi wapate wawakilishi wa kutoa maamuzi na idhini kwa watawala kwa niaba yao.
Ni katika muktadha huu tunapata chombo cha uwakilishi kinachoitwa Bunge. Kwa hiyo kazi kubwa nambari moja ya mbunge ni kuwasilisha maoni na matakwa ya watawaliwa wanaowawakilisha.
Pili, kazi kubwa namba mbili ya bunge ni kusimamia watawala kutekeleza ahadi zao kama walivyoahidi kutenda kupitia ilani yao ya uchaguzi.
Jambo la kusisitiza hapa ni kwamba bunge litafanya hiyo kazi ya kusimamia watawala kama wawakilishi wa watawaliwa.
Mbunge anapojifanya yuko upande wa watawala na kuwasemea watawala badala ya watawaliwa basi kuna mushkeli maana huyo mbunge atakuwa hatambui majukumu yake kama mwakilishi.
Kwa hiyo wabunge wanahaki ya kuwahakikishia wananchi wanaowawakilisha wanaona kile wanachokisema.
Kusema kwamba hayo matangazo ya mijadala yao yataonyeshwa baadaye na huku kukiwa na uwezekano mkubwa kwamba baadhi ya yaliyosemwa yatakatwa si jambo la kupendeza hata kidogo.
Ndiyo maana wabunge wanaojitambua wako upande gani kati ya watawala na watawaliwa wanafanya juhudi kuwaonyesha waliowatuma wanafanya nini bungeni.
Kwa mantiki hiyo basi wabunge wanaojirusha wanafanya kitu cha maana kwa vile wanajali maslahi ya waliowatuma.
Kwa upande mwingine wabunge wengi wanajichanganya na kujiona kwamba wao ni sehemu ya watawala kwa sababu serikali (watawala), imeundwa na chama ambacho wao ni wanachama wake.
Ni kwa sababu hiyo selikali inapata mwanya wa kufanya madudu na isiwajibishwe kwa sababu waliotumwa kuisimamia wamejifanya sehemu ya serikali.
Lakini wakati mwingine serikali inatumia nafasi kwamba wabunge wengi ni wanachama wa chama chake na hivyo inawarubuni au kuwatisha waiunge mkono.
Serikali inapofanya hivyo inakuwa inaua demokrasia na kidogo kidogo inaanza kujigeuza kutoka kuwa watawala wa mfumo wa kidemokrasia na kuingia mfumo wa kidikteta. Hili ni jambo hatari kwa mustakabali wa taifa.
Nasema ni hatari maana bunge linapotumiwa kwa njia yoyote kupitisha kila jambo linageuzwa kuwa muhuri wa watawala , jambo linaloweza kuzorotesha maendeleo ya wananchi.
Ndiyo sababu wananchi kupitia iliyokuwa Tume ya Mabadiliko ya Katiba, waliweka kipengele cha kuwapa haki ya kumwajibisha mbunge hata kabla ya muhula wake wa miaka mitano kumalizika.
Njia nyingine mbadala iliyopendekezwa ni mgombea binafsi ili wapate wawakilishi watakaowajibika kwao badala ya kuwajibika kwa vyama vyao na serikali.
Hili nalo linapingwa sana na watawala maana wanajua hawatakuwa na uthibiti na wabunge. Imekuwa jambo la kawaida sasa serikali kupitia chama kuwatishia wabunge kuwavua uanachama jambo linalomaanisha kulingana na katiba ya sasa kwamba mbunge atakayefanyiwa hivyo atapoteza ubunge wake.
Nahitimisha kwa kutoa wito kwa serikali kusikia malalamiko ya watu kwamba wanataka bunge lao walione live. Ni haki yao kuona wawakilishi wao wanafanya na kusema nini bungeni.










