Mlango unaowainua wasichana kwenye sayansi unapofunguka

21Feb 2023
Frank Monyo
DAR ES SALAAM
Nipashe
Mlango unaowainua wasichana kwenye sayansi unapofunguka
  • Ni mkakati wasome kozi za uhandisi mitambo, elektroniki na teknolojia

TANZANIA imekuwa mstari wa mbele kuhamasisha wanafunzi wakiwamo wasichana kusoma sayansi, juhudi zikiambatana na ujenzi wa sekondari ‘spesho’ za wasichana kwa kila mkoa.

Hamasa inaongezeka zaidi awamu ya sita, serikali inapoanza ujenzi wa shule hizo lakini kuanzisha rasmi ufadhili wa vyuo vikuu unaofanikishwa na Samia Scholarships kwa ‘vipanga’ wanafunzi wanaofanya maajabu kwenye masomo ya sayansi kidato cha sita.

Taifa linalenga na kutamani  kuwa na wasomi wa sayansi, teknolojia, uhandisi na hisabati (science, technology, engineering na mathematics-STEM).

Licha ya takwimu za Shirika la Umoja wa Mataifa la Elimu, Sayansi na Utamaduni (UNESCO), kuonyesha kati ya wanafunzi wote wanaokwenda vyuo vikuu kusoma masomo ya STEM, asilimia 30 pekee ni wanawake.

Ili kuunga mkono juhudi hizo wadau wa elimu, hawajabaki nyuma na katika jitihada za kukabiliana na pengo hilo, Kampuni ya Bia ya Serengeti (SBL) inaanzisha mpango wa uanagenzi wa STEM.

Uanagenzi ni mafunzo yanayohusisha kujifunza kutoka kwa wengine na kurithi kwa ufanisi kile wanachokifanya ili kuwa mahiri zaidi.

Ukiwa ni mkakati wa miaka 10 wa Diageo ujulikanao kama Society 2030: Spirit of Progress.Kupitia mpango wa uanagenzi kwa masomo ya STEM, SBL inafadhili wanafunzi waliohitimu elimu ya juu ili kujifunza na kupata uzoefu muhimu na mafunzo kazini.

Akizungumzia kuhusu programu hiyo kwenye mahojiano na Nipashe, Meneja Ubora wa Uzalishaji wa SBL, Natalia Kimacha, anasema kuna mafanikio ya kujivunia kwenye programu hiyo, hasa jinsi inavyowezesha vipaji katika eneo la sayansi, teknolojia, uhandisi na hisabati.

Anasema kupitia mpango wa uanagenzi kwa masomo ya STEM, SBL inafadhili wanafunzi wanaohitimu elimu ya juu ili kujifunza na kupata uzoefu muhimu na mafunzo kazini. 

"SBL kwa wakati wote imekuwa ikisisitiza ushirikishwaji katika shughuli zake za biashara, kwa hivyo, mpango wa uanagenzi wa STEM unaimarisha zaidi dhamira hiyo katika jitihada za kuziba pengo hilo kwa kuwapa wasichana fursa ya kupata ujuzi kwenye masomo ya STEM," anasema Natalia.Anaongeza kuwa SBL inachukua awamu nyingine ya makundi baada ya kukamilisha awamu ya kwanza ya programu ya uanagenzi."Mchakato wetu wa kuajiri huchagua 10 bora kati ya mamia ya waombaji. Tumeunda sera kwa wahitimu na kutoa programu ambayo inawapa uzoefu wa vitendo na nafasi za kazi. Kampuni ina ushirikiano na vyuo vikuu kadhaa na asasi za maonyesho ya kazi.” Anaongeza. 

Natalia anaeleza kuwa mpango wa kampuni ya ufadhili wa masomo ya kilimo ujulikanao kama ‘kilimo viwanda’ ni mikakati bayana ya jinsi wanavyosaidia vijana kupata uzoefu ndani ya soko la ajira.Anasisitiza kuwa SBL inaahidi kuendelea kusaidia wanawake katika nyanja za sayansi na teknolojia, kama sehemu ya juhudi zake za kuziba pengo hilo, huku ikipanua mipango yake ya kuwawezesha wanawake katika biashara zake zote pia. 

Anawataja wanafunzi ambao wamenufaika na mpango huo baada ya kuhitimu kuwa ni Lydia Masonda, Julieth Masawe na Christina Ndalichako ambao kwa sasa wanafanya kazi kwenye mitambo ya kiwanda cha SBL Moshi. 

Akitoa maoni yake kuhusu mpango huo, Lyidia anasema: “Naona fursa ya kukua, pamoja na kupata ajira ya kudumu katika kampuni ya SBL. Ninaweza kusema kwa kujiamini kuwa ninao mustakabali katika safari yangu ya kazi."Kwa upande wake, Julieth anasema anachukulia uzoefu wake katika programu kuwa safari ya ukuaji kitaaluma na kibinafsi akiongeza:"Sikuwahi kufikiria kwamba siku moja ningeweza kutumia kikamilifu mashine na kuiendesha kwenye uzalishaji tena kwenye kampuni kubwa kama SBL.”"Kuwapo kwangu hapa kunanifanya niwe na ari ya kujifunza na kuwa bora katika ufundi wangu. Nilipata mafunzo ya kiufundi, biashara na upande wa usambazaji wa biashara na vyote vina faida.”

Mmoja wa wanufaikaji wa mradi wa STEM kutoka kundi la pili, Miriam Masanja, mwanafunzi wa Chuo Kikuu cha Sayansi na Teknolojia Mbeya, mhitimu wa shahada ya uhandisi wa umeme na elektroniki anasema: “Tangu nijiunge na kundi hili, nimepata ujuzi wa kutatua matatizo na uwezo wa kiutendaji katika kiwanda cha bia.”

Halikadhalika anasema amepata ujuzi wa kufanya vitu vingi ambavyo ni zana za maendeleo ya kibinafsi na ukuaji katika sekta hiyo.

Glory Hungu, anayetoka Chuo Kikuu cha Sokoine cha Kilimo, akisoma shahada ya sayansi ya Chakula na teknolojia na aliyenufaika na mpango wa STEM anasema anaona mpango huo ni muhimu kwa wasichana na wanawake wa taifa hili.“Siku zote nimekuwa mdadisi wa kutatua changamoto katika masuala tofauti lakini nikiwa na shauku ya kupata ujuzi kupitia majaribio na sayansi daima imekuwa ikinipa majibu ninayohitaji.” Anaongeza Glory.