Serikali na wadau wanaendelea kutoa elimu kuhusu athari za ukatili wa kijinsia mashirika ya kijamii yakiwa mstari wa mbele.
Miongoni mwa wadau hao, ni Kituo cha Sauti ya Jamii Kipunguni Dar es Salaam, ambacho hivi karibuni kinapokea wadau kutoka mataifa ya kigeni wanaovutiwa na mbinu wanazotumia kufikisha elimu kwa umma.Wageni hao wanatoka Ireland, Palestina, Uingereza na Sierra Leone wanaoongozwa na Ubalozi wa Ireland Tanzania, ili kujionea mafanikio ya kituo hicho, katika utoaji wa elimu ya kupinga ukatili huo.Akizungumza katika ziara hiyo, Ofisa Maendeleo ya Jamii Mwandamizi kutoka Wizara ya Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum, Dorah George anakisifu kwa kazi ya mfano."Kituo kimetembelewa kutokana na juhudi zake binafsi za kufanya kazi za maendeleo ya jamii, kwa njia shirikishi kwa maana ya kushirikisha makundi mbalimbali na kuwavutia wageni hawa kukitembelea," anasema Dorah.Anaeleza kuwa mashirika yasiyo ya kiserikali yanayotoa elimu ya kupinga ukeketaji ni mengi na kwamba Kituo cha Sauti ya Jamii ni mojawapo wa mfano wa kuigwa na kimewafanya wadau kutoka nje kuja kujifunza kitu.Kiongozi wa msafara wa wadau hao walifika katika kituo hicho, Mkuu wa Idara ya Jinsia kutoka Serikali ya Ireland, Tom Crowley anasema ujuzi waliopata kituoni hapo wataufikisha katika maeneo mengine duniani."Tumekuja hapa kutoka mataifa mbalimbali, tumejifunza jinsia wanavyotoa elimu ya kukabiliana na ukatili wa kijinsia, nasi tumepata ujuzi tutaufikisha kwa wengine nao waige mfano wenu," anasema Crowley.Mkuu wa Idara ya Programu ya Ruzuku kutoka Women Fund Tanzania (WFT), Redimna Ginwas, anasema Ireland huwawezesha kifedha ambazo wao hufadhili vikundi vinavyopambana na ukatili wa kijinsia."Wafadhili wameridhika na kazi yenu ya kupambana na ukatili wa kijinsia katika jamii, hivyo tunawatia moyo mwendelee zaidi ili kuhakikisha jamii inaishi salama bila ukatili wa aina yoyote," anasema Redimna. WALIVYOANZAKatibu wa Kituo cha Sauti ya Jamii, Sada Shifta, anasema mwaka 2014, walianza kazi kwa kuita watu katika kituo hicho na kuwapa elimu kuhusu haki zao na kuwahamasisha kukataa vitendo vya ukatili."Baadaye tukaanza kwenda kwa wanajamii na baada ya kuona mwitikio mkubwa watu wanaotamani kupata elimu hii, na tumefanikiwa kufikia wengi, ingawa vita zaidi inahitajika," anasema Sada.Anaeleza kuwa kwa njia hiyo, wamesaidia baadhi ya mabinti kupata mafunzo ya chereheni na ujasiriamali, hasa wale waliokimbia vitendo vya ukeketaji kutoka nyumbani kwao baada ya kuelimika na kutambua madhara ya ukatili huo."Kuanzia mwaka 2017 hadi 2022 tumefikia watu 1,111, wanawake ni 895 na wanaume 216. Aidha, mafunzo ya ujasiriamali kwa vitendo tulifikia watu 5,842 lakini tukiwaokoa mabinti 109 kutoka mikono ya wakeketaji," anasema.
Kipunguni ni eneo linaloishi jamii za wakeketaji wanaoendeleza mila na desturi hizo.
Kadhalika katika kipindi chote hadi sasa, wamefanikiwa kuongeza hamasa ya kudai haki na kwamba wananchi wamefunguka wanaripoti vitendo vya ukatili ikiwamo rushwa ya ngono anasema.
Anatoa mfano kuwa mwaka 2014 vitendo vya ukatili vilikuwa haviongelewi wala kuripotiwa,lakini kwa sasa wanapokea kesi nne hadi saba kwa siku, wanaume wanashiriki mijadala ya ukatili, wanawake na wasichana wanaripoti vitendo vya rushwa ya ngono.
Anafafanua kuwa kituo kimeongeza ushiriki wa wanawake katika ngazi za maamuzi na kwamba wamekuwa na jamii inayochukua hatua juu ya vitendo vya ukatili huku wakiwa na viongozi wa serikali bega kwa bega."Tumeanzisha klabu za kupinga ukatili ndani ya jamii, baadhi ya ngariba na wazee wa mila wameacha ukeketaji, lakini elimu tunayoitoa, imesaidia kuongeza uelewa wa haki kwa wafanyakazi wa majumbani," anasema.Mkurugenzi wa kituo hicho, Seleman Bishagazi anatoa ombi kwa WFT kuendelea na utaratibu wa kutoa ruzuku bila kuzingatia vikundi vya watu wenye elimu kubwa katika ufadhili bali hata wa kawaida wanaoishi karibu na jamii."WFT wanatoa fedha kwa vikundi vya kujamii kama chetu, lakini mashirika mengine yanaangalia elimu za watu badala ya kazi zinazofanywa na yanatoa fedha katika asasi si kwa vikundi," anasema Bishagazi.










