Mkwasa: Wanyama, Owino wangekuwa Stars tungefuzu

01Jun 2016
Lasteck Alfred
Lete Raha
Mkwasa: Wanyama, Owino wangekuwa Stars tungefuzu

KOCHA wa timu ya taifa ya Tanzania, Boniface Mkwasa, amedai kama Stars ingekuwa nyota wawili wa kimataifa wa Kenya, ingefuzu AFCON 2017.

Victor Wanyama

Mkwasa aliwataja nyota hao kuwa ni kiungo wa Southampton ya Uingereza, Victor Wanyama, na beki wa Zesco ya Zambia, David Owino ‘Calabar’, ambaye alikuwa atue Simba msimu uliopita.

Katika mechi ya Taifa Stars dhidi ya Harambee Stars ya Kenya iliyoisha kwa sare ya 1-1, Owino alionekana kucheza kwa utulivu na ustadi wa hali ya juu uliomvutia Mkwasa kwenye mchezo huo uliopigwa Jumapili iliyopita kwenye uwanja wa Moi Kasarani, jijini Nairobi.

Mkwasa alimsifia beki huyo akisema, "Kwenye timu ya taifa ya Kenya nilivutiwa zaidi Owino na Wanyama.

“Owino ni mtulivu, mbunifu na mwenye uwezo wa kukaba vizuri, wakati Wanyama alikuwa ni mfano wa kuigwa kwenye eneo kiungo kutokana na jinsi alivyomudu eneo la kati. Kama ningekuwa nao kwenye kikosi changu hakika Stars ingekuwa tayari imefuzu.

“Wanyama ndiye mchezaji bora niliyepata kumwona Kenya. Natamani Tanzania ingekuwa na mchezaji wa aina yake kwani ni moja kati ya viungo bora kuwahi kutokea kwenye ukanda huu wa Afrika Mashariki na Kati,” alisema kocha huyo.

Stars ilitumia mechi hiyo ya kirafiki kama sehemu ya maandalizi ya kuikabili Misri Juni 4, mwaka huu katika kuwania kufuzu kushiriki AFCON 2017.