DK. Turuka: Kilimo kitakachotutoa ni hiki

02Jun 2016
Gaudensia Mngumi
Dar es Salaam
Nipashe
DK. Turuka: Kilimo kitakachotutoa ni hiki

TANZANIA inahitaji mikakati madhubuti na kuongeza mazao ya kilimo na uzalishaji kwa ajili ya kupata malighafi ya viwandani, ikiwa ni sehemu ya jitihada za kufanikisha utekelezaji wa Mpango wa Viwanda wa Miaka Mitano, unaotarajiwa kuanza kutekelezwa mwezi ujao.

pamba

Ni jambo ambal litakalofanikiwa kupitia sayansi na teknolojia. Katibu Mkuu wa Wizara ya KIlimo, Mifugo na Uvuvi, Dk. Florence Turuka, anasema serikali inaandaa mazingira yatakayoiwezesha nchi kutumia teknolojia ya uhandisi jeni (Genetic Engineering).

Hiyo ni sehemu ya kutatua changamoto za kilimo nchini na kupata ufumbuzi wa matatizo yanayoikabili sekta hiyo, inayoandamwa na mabadiliko ya tabia nchi.

Uhandisi jeni unaozalisha mazao au viumbe vilivyobadilishwa vinasaba (GMOs),unaweza kuwa sehemu ya ufumbuzi wa matatizo ya kilimo, kwa kuongeza chakula, upatikanaji malighafi ya viwanda, fedha za kigeni na ajira.

Akizungumza katika Chuo Kikuu cha Kilimo cha Sokoine (SUA) wiki hii mjini Morogoro, Dk. Turuka, wakati wa kuzindua ripoti ya hali ya biashara ya mazao ya GMO duniani. Anasema umefika wakati wa Tanzania kufaidika na teknolojia hiyo, huku akihoji: ”kama wenzetu wanafaidi, kwanini sisi tusifaidike?”

KILICHOJIFICHA KWENYE RIPOTI

Wakati Dk. Turuka anatoa maelezo hayo, Ripoti ya Biashara ya Mazao ya GMOs 2015, inataja mafanikio ya ugunduzi, akitoa mfano wa viazi mviringo visivyoshambuliwa na magonjwa vya Marekani, ambavyo sasa viko sokoni.

Pia, anataja kuingizwa sokoni samaki jamii ya jodari (salmon) wa GMO ambao Taasisi ya Udhibiti wa Chakula (FDA), imeruhusu kuwa kitoweo cha binadamu

“Jodari wanaopatikana baharini huchukua miaka mitatu kuvunwa. Ni tofauti na wa GMO wanaopandwa mabwawani na kuliwa baada ya miezi 18” inasema ripoti hiyo.

Ripoti inaeleza nguruwe wanaozalishwa kwa njia ya GMO, wasioshambuliwa na maradhi hatari ya virusi vya nguruwe, ambayo kila mwaka yanaigharimu sekta ya kilimo ya Marekani Dola milioni 600 kila mwaka(Wastani wa Sh. trilioni 1.3).

Katibu Mkuu anasisitiza kuwa, mataifa mbalimbali yanatumia Biooteknolojia kujibu changamoto za kilimo na uzalishaji, hivyo Tanzania nayo kama ilivyohama kutoka analoji na kuingia dijitali ndivyo pia inavyojipanga kutumia teknolojia hii.

Anahoji kama mataifa mengine yameneemeka kwenye kuzalisha pamba, mahindi,maharage, samaki, ni wakati wa Tanzania kufaidika nayo na hasa pamba na mahindi ambayo ni duni nchini.

Dk. Turuka anafafanua kuwa Mpango wa Maendeleo wa Miaka Mitano, unalenga kuongeza viwanda vya kuchakata mazao ya kilimo kama matunda, ngozi na pamba.

Anasema, lengo ni kuzalisha bidhaa za nguo, viatu, juisi na vyakula mbalimbali, taifa.

Kiongozi huyo anasema kuwa, uzalishaji unaotumia teknolojia ya GMOs unaweza kusaidia kukabiliana na tatizo la upatikanaji wa malighafi viwandani.

Anasema, kuwekeza katika viwanda vya kuchakata mazao ya kilimo bila ya kuwa na uhakika wa malighafi, kunaweza kukwamishwa na ukosefu wa malighafi hayo.

Katibu Mkuu anawataarifu watalaamu nawasomi wa SUA, watafiti na wadau wa kilimo nchini kote, kuwa serikali ina nia ya kuboresha kilimo kiwe cha kisasa na bio -teknolojia iwe njia mojawapo itakayotumiwa kusaidia taifa na wakulima kuongeza tija.

VITA YA GMO

Dk Turuka,anasema kuna vipingamizi vingi dhidi ya GMOs na anawataka wananchi kuacha vita dhidi ya teknolojia hiyo.

Anawataka wadau, wakiwamo wanaharakati,vyombo vya habari, wanasiasa, maofisa ugani na watafiti wa Tume ya Sayansi na Teknolojia(Costech), kuwahamasisha wananchi juu ya umuhimu wa teknolojia hiyo na si kuzungumza ubaya pekee.

Kiongozi huyo anakiri hakuna maendeleo ya uchumi pasipo teknolojia na mojawapo ni uhandisi jeni.

Anatoa mfano wa zamani kwamba, GMO na utafiti wa bidhaa hizo haikuruhusiwa, lakini sasa mlango uko wazi kwa serikali kuruhusu utafiti kwenye maabara na itaendelea kushirikiana na wataalam kufanikisha azma hiyo.

Dk. Turuka anasema kwamba, anachokiona katika mtazamo wake ni kwamba, kuna
kipingamizi cha bio- teknolojia, pasipo hata ufahamu wa kutosha.

Kwa ujumla GMOs au viumbe vilivyobadilishwa nasaba (DNA), mfano mazao yameboreshwa na kupewa tabia bora ambazo awali hazikuwepo,hayashambuliwi na magonjwa, huhimili ukame au kutumia kiasi kidogo cha maji , huzaa sana na hayahitaji kunyunyuziwa kemikali za kuua viatilifu,anaeleza Mtafiti wa Bayoteknolojia wa Jukwaa la Bayoteknolojia, Dk. Emerald Mneney.

Kubadilisha nasaba huko hufanywa maabara, baadaye kwenye eneo maalumu lililotengwa na kuandaliwa kwa ajili ya majaribio ili viumbe wasichangamane na ‘dunia’ nyingine ya viumbe wasiobadilishwa nasaba.

Mbegu za GMOs ni kama za ‘haibrid’ au chotara ambazo hupatikana kwa njia ya kupandisha wanyama wa asili na wa kisasa, ama kuchanganya chavua ya mazao ya asili na ya kisasa ili kuongeza ubora na wingi wa mazao.

Taarifa ya mtandao inaonyesha kuwa pamba ya GMO au ‘Bt Cotton’ inayolimwa kwa wingi China na kwa Afrika inapatika Bukinafasso.

Pamba hii inaelezwa kuwa imeongezewa tiba asilia ya kuua wadudu wavamizi kwa hiyo haihitaji viatilifu.Kama hayatanyunyiziwa sumu ni dhahiri haitaathiri mazingira ya asili na uoto utakuwa salama, pia inazaa sana hivyo ni tija kwa mkulima.

Kwa Tanzania utasikia maneno mengi dhidi ya teknolojia hii inaelezwa kuwa ni ya wakulima wakubwa wanaolenga kupata faida.
Wapo wanasiasa na wanaharakati wanaotangaza kuwa inatengeneza ‘utegemezi wa kiteknolojia’kwenye kilimo.

Hali hiyo inawalazimisha wakulima kutegemea viatilifu na mbegu kutoka nchi zinazobuni teknolojia hiyo.
Kuna hofu kuwa mbegu hizo zikipandwa huua uoto wa asili, huongeza aleji (mzio)kwa walaji.

Yapo madai kuwa wanaume wakila mazao ya GMO huota matiti makubwa wakati wanawake wanakuwa na ndevu.

Dk Mneney anasema madai hayo hayajathibitishwa na kwamba hofu hizo hazisaidii kwa vile ni za uongo. Anashauri kuwe na mawasiliano ya uwazi na ukweli ili umma ufahamu ukweli ili watu waamue kutumia teknolojia hii.

“Tanzania haijaanza kutumia teknolojia hiyo na kwamba hakuna mbegu za GMO wala bidhaa zake zinazopatikana nchini.” Anakumbusha.

Anasema uwekezaji kwenye teknolojia hiyo ni wa gharama kubwa kwa hiyo mkono wa serikali unahitajika na kukumbusha kuwa nchini Kenya Rais wa zamani Mwai Kibaki, alisema kwanini nchi hiyo ibaki nyuma kwenye teknolojia hiyo.

Wakati huko Uganda Rais Yoweri Museveni, aliwataka wanasayansi wake kubadilisha fikra na kuleta mabadiliko kupitia teknolojia hiyo.

Hayo yanaonyesha utashi wa kisiasa kwenye uwekezaji kwenye sekta ya bayoteknolojia ili kuongeza ufanisi, anasema Dk.Mneney.