MAISHA MPYA YA MLOGANZILA

19May 2016
Elizaberth Zaya
Dar
Nipashe
MAISHA MPYA YA MLOGANZILA
  • Mazito ya leo, siku ya bomoabomoa nafuu

KAZI mojawapo ya miti ni kustahimili mazingira na mabadiliko ya tabianchi.

Pamoja na hilo, ndege na wanyama wamekuwa wakiitumia kuwa mahali pa kuishi.

Ndege huitumia kutengeneza viota na nyuki wanatengeneza asali.

Lakini katika eneo la Kwembe - Mlogalzila, wakazi waliobomolewa nyumba zao kwa sasa nao wameamua kuchukua matumizi hayo kwa kufanya miti kuwa makazi yao.

Ni hatua iliyofikiwa na baadhi ya wakazi wa nyumba zipatazo 400 zilizobomelewa katika eneo hilo,baada ya mahakama kuamua kwamba walikojenga si halali na mwenye eneo kuchukua operesheni hiyo.

Mshindi wa kesi hiyo anadaiwa kumiliki tangu miaka ya 1990 na maisha ya chini ya mti yamekuwa mfumo wa maisha yao tangu wabomolewe majengo yao.

Wanaishi chini ya mti wakiwa ‘halali’ ya mvua, jua na mbu na wamekuwa jamii inayofananishwa na wanyama.

Mapema wiki hii, Nipashe ilipiga kambi mahali hapo kutathmini maisha yao, baada ya kuwa shuhuda wa bomoabomoa iliyosamabratisha makazi yao, wiki kadhaa zilizopita.

Badala ya majumba, sasa ni vibanda vilivyojengwa kwa mifuko na vyandarua vilivyotengenezwa katika vilima na mabonde.

Pia kulikulikuwapo vibanda vilivyoegeshwa na tofali zilizokatika, ili mradi kila mtu anakuwa na ubunifu unaomtengenezea mfano wa makazi.

Nje ya vibanda hivyo, kulikuwapo kinamama walioketi, wakiendelea na pilika pilika za shughuli mbalimbali za nyumbani, kama vile kufua nguo.

Ikiwa majira ya asubuhi, niliazimika kusogelea vibanda hivyo, lakini wenyeji baada ya kuiona sura yangu, walionyesha kuhamaki na nikasikia kauli:"Haya (mmiliki wa eneo) kawatuma tena watu wake kuja kutuondoa, hao wanakuja!"

Baada ya kufika ilibidi kujitambusha tena kwa kauli ya upole, ili kujihami na dalili hisia mbaya za aina yoyote ile ambazo dalili zake zilianza kujitokeza.

Ni hasira zitonakazo na kuvunjiwa nyumba, watu hawajiamini na muda mwingi wanahofia kufukuzwa kabisa eneo hilo walilojistiri, baada ya kuvunjiwa nyumba.

Hata hivyo, wapo walioendelea kuamini ugeni huo unawezekana ulitumwa na mtu aliyewavunjia majengo.

Kwa kuwa ni sehemu iliyokuwa na matofali mengi, nilichagua kimoja, ambako alikuwapo mama anayefua nguo.

UCHUNGU WAFUKULIWA

Baada ya kujitambulisha, mwenyeji wangu naye alijitambulisha kwa jina Atuganile Ipungi, akiwa na mtoto wake mdogo aliyesimama kando.

Pia alikuwapo mama mwingine aliyeketi. Nilimsogelea, huku naye akinikaribisha. Niliketi kwenye kipande cha tofali.

Kauli ya kwanza ilikuwa ombi la kuvumuliwa nizungumze naye kwa dakika chache.

Hapo ndipo simulizi ilipoanza. Alianza kueleza namna alivyoishi akiwa na nyumba yake na baada ya kuvunjwa.

Kwanza anaanza simulizi kwamba alikuwa anaishi katika nyumba hiyo na mumewe, kabla ya mume huyo kumkimbia huku nyuma akimuacha Atuganile na watoto wawili. Huko aliokoenda alioa.

Anasema pamoja na kwamba mwanzoni alipata shida, alijipa moyo na kuanzisha biashara ndogo iliyomsaidia kuendesha maisha na watoto katika mambo kama vile kula na kuwasomesha, jambo lililomsahaulisha machungu ya kukimbiwa na mume.

Ghafla wakati mazungumzo yanaendelea, Atuganile alibadilika na kuangua kiliom alipoanza kueleza maisha yake ya sasa na watoto wawili alio nao chini ya mti.

Ni maisha baada ya nyumba kuvunjwa wiki chache zilizopita na kusababisha watu waliokuwa jirani kusogea kumtuliza.

"Sijui nimekosea nini kwa Mungu wangu? Mume wangu alinikimbia, akaniacha nahangaika na watoto, lakini nilipata moyo wa kuendelea na maisha kwa sababu nilikuwa ninanyumba.

“Sikufikiria kodi, lakini eti kufumba na kufumbua makazi yangu yamekuwa kama ya mnyama. Naishi chini ya mti" analalama.

Atuganile, ambaye maana ya jina hilo katika lugha ya Kinyakyusa ni ‘Ananipenda’ anaendelea kulalamika huku akibubujikwa na machozi:”Iko wapi thamani ya maisha yangu, mtu mmoja anatutesa hivi?

“Siamini kama mimi ndio haya yamenikuta. Wazazi wangu nao wametangulia mbele ya haki, nitakimbilia wapi mimi?"

Ni mazungumzo yaliyozaa mandhari ya simanzi kwani hata waliokuwa wakimtuliza walianza kutokwa na machozi, huku mtoto aliyekuwa amesimama kando yake aliendelea kumsihi mama yake anyamaze.

Ilibidi nivumilie kidogo hadi anyamaze na aliponyamza nilimpa pole na kusitisha mazungumzo kwa ahadi ya kurudi tena.

Ziara ya ki-uanahabari ilihamia kibanda kingine alichokuwa mama mzee na mwingine mjamzito.

MAZITO MENGINE

Kwa kuzingatia mchakato ule ule, nilijitambulisha na kuomba kuzungumza nao. Bila ya hiyana walikubali.

Mama huyo mzee aliyejitambulisha kwa jina la Hadija Liloka, anasema amevunjiwa nyumba akiwa na wiki tatu tu baada ya kuhamia.

Hadija anasema nyumba hiyo alijengewa na mtoto wake wa kike kwa namna aliyoitaja ‘pesa za kudunduliza.’

Anasema mtoto huyo hivi sasa amelazwa katika Hospitali ya Rufani ya Amana, Dar es Salaam, baada ya kupata mshituko na kuzimia, alipoambiwa nyumba hiyo imevunjwa.

Mbali na bintiye, Hadija anasema ana mjukuu anayeishi naye aliyeathiriwa na moshi wa mabomu ya machozi yaliyopigwa na Polisi siku ya bomoabomoa.

Bila ya kumtaja jina, umri wala anakotibiwa, anasema mjukuu huyo hivi sasa anaendelea na matibabu ya macho.

Anasema ni tukio lililoacha historia katika maisha yake na kwamba hana matumaini ya kupata nyumba nyingine tena kulingana na uhalisia wa umri wake.

Bibi Hadija anatoa rai iwapo kuna msamaria mwema yeyote, ajitokeze kumsaidia apate mahali pa kulala, hata kama ni kipindi kifupi, tofauti na chini ya mti anakoishi sasa.

"Ukiniangalia mimi umri umekwenda. Sina uwezo wa kupata nyumba nyingine, hata binti yangu aliyenijengea hiyo nyumba ambaye angeweza kunisaidia naye anaumwa.

“Mimi mwenyewe nimekuwa naugua presha kwa kipindi kirefu, sasa kuendelea kukaa hapa chini ya mti na kunyeshewa mvua ninaweza kuugua zaidi.

“Kama nitapata hata msamaria mwema akanisaidia pa kulala hata kama ni nyumba ambayo haijamalizika, nikakaa kwa muda nitapata faraja," anasema Hadija.

Vumilia Kombole, ambaye ni mjamzito aliyekuwa amepumzika nje ya kibanda na Hadija, anasema yuko ukingoni kukamilisha miezi tisa ya ujauzito, lakini mahali pa kuishi ndiyo mtihani kwake, iwapo atajaliwa kupata mtoto.

Vumilia anayesema hana mtoto, anafafanua kuwa tangu makazi yake yavunjwe, afya yake imekuwa ikitetereka kwa kuumwa kila mara, akihisi chanzo kikuu ni baridi kali na kunyeshewa mvua.

Anasema pamoja na mume wake kujitahidi kutafuta nyumba ya kupanga, bado hawajapata kwani hawana fedha za kutosha.

Said Rashid, ni mwathirika wa bomoabomoa, anayelalama kuwa baadhi ya wakazi waliobomolewa nyumba zao wenye uwezo wamehama na kwenda kupanga na waliobaki ni wenye hali duni.

Anasema tangu wapatwe na mkasa huo, hakuna kiongozi aliyewatembelea kusikia shida zao, isipokuwa Diwani wa Kata ya Kwembe.

Ombi lake kwa serikali ni iangalie namna ya kuwasaidia watoto na wazee,kuwanusuru na hali hiyo ngumu.