Japan; kinara wa madeni duniani

20Jan 2023
Na Mwandishi Wetu
DAR ES SALAAM
Nipashe
Japan; kinara wa madeni duniani
  • • Pata habari za nchi 10 tajiri duniani

MNAMO Septemba mwaka jana, Japan ilikuwa na deni la umma lililofikia Dola za Marekani trilioni 9.2, ambayo ni asilimia 266 zaidi ya Pato la Taifa.

 

Kwa kulinganisha ile ya Marekani, ilifikia dola za Marekani trilioni 31 katika kipindi hicho, lakini kiuchumi ni sawa na asilimia 98 ya Pato la Taifa.

Sababu inatajwa, Japan imetumia miongo kadhaa kuongeza matumizi ya ndani, kuhudumia uchumi wake. Inatajwa matumizi ya raia wake yako katika mahitaji yasiyoendana na ya kiserikali na ukuaji uchumi kwa ujumla.

"Akiba binafsi ni kubwa na uwekezaji ni dhaifu, ikimaanisha mahitaji dhaifu," anasema Takeshi Tashiro, Mchumi Mwandamizi katika Taasisi ya Peterson ya Uchumi wa Kimataifa, akifafanua kunashuhudiwa zaidi fedha katika akiba binafsi.

Sababu ya hali hiyo inatajwa ni kuwapo tatizo la idadi ya watu wake wengi ni wenye umri mkubwa, ambao huongeza gharama za usalama wa kijamii na huduma za afya serikalini na si wazalishaji zaidi.

"Uzee wa idadi ya watu unaochangia hali hii, unatarajiwa kuendelea kwa muda mrefu," anaongeza mtaalamu huyo.

Hata hivyo inaelezwa kuwa, pamoja na uwapo wa deni hilo kubwa la umma, wawekezaji kimataifa wanaendelea kuiamini Japan, kwa kuikopesha fedha kupitia kununua madeni yake.

CHANZO NINI?

Deni la umma la Japan linatajwa lilianza kuongezeka mwanzoni mwa miaka ya 1990 na kuathiri fedha na mali isiyohamishika. Hadi kufika mwaka 1991, uwiano huo wa deni ulikuwa asilimia 39.

Kuanzia wakati huo, kasi ya ukuaji uchumi ulianza kushuka sana, hata ikapunguza mapato ya serikali, huku  ikilazimisha kuongezeka matumizi yake.

Miaka 10 baadaye, zama za miaka ya 2000 deni la serikali lilivuka asilimia 100 na hadi kufikia mwaka 2010, lilikuwa limeongezeka mara mbili zaidi.

Inatajwa kukuzwa na matukio kama vile kushuka kwa uchumi wa dunia miaka ya 2008; Tetemeko la Ardhi la Fukushima na Tsunami iliyofuata 2011 na hivi karibuni zaidi janga la Covid 19, mahususi miaka ya 2020 na 2021.

INAKABILI VIPI?

Ili kupunguza athari za matukio haya na kudumisha bajeti ya kila mwaka katika maeneo kama vile elimu, afya au ulinzi, Japan kama karibu nchi zote duniani, huuza dhamana za serikali kwa watu na kampuni mbalimbali binafsi.

Kwa maneno mengine, inaweka deni lake katika masoko ya kimataifa kwa ahadi ya kumrudishia mwekezaji kwa ukamilifu wake pamoja na faida ndogo.

Wawekezaji hukopesha pesa zao kwa nchi hiyo, hasa wale wanaona hatimiliki hizo ni mahali salama pa kuweka pesa zao.

 

 

"Pamoja na mavuno yaliyopatikana, hati fungani kutoka nchi zilizoendelea zinaweza kutumika kwa urahisi kama dhamana ya mikopo," anaongeza Mtaalamu Tashiro.

Deni la Japan limekuwa endelevu kwa muda na nchi haijaanguka kiuchumi, wataalamu wanaeleza sababu ni kuweka mavuno kwenye bondi za serikali, wawekezaji wanaolipa kidogo wakiwa na imani.

"Kuna wawekezaji ambao wanapendelea utulivu badala ya faida na ndiyo maana wanachagua Japan kuweka akiba yao ya ziada," mwana - uchumi Shigeto Nagai anaelezea.

Bendera.

"Japan imeweka viwango vya riba vya chini sana. Ingawa kiwango cha deni ni kikubwa sana, serikali inalipa riba kidogo kwa wadai wake. Inaweza kuendeleza deni kubwa kwa muda usiojulikana," anasema Ken Kuttner, Profesa wa uchumi katika Chuo cha Williams, kutoka Massachusetts, Marekani.

"Hakuna madeni mengi ya Kijapani yanayoshikiliwa na wageni. Ilikuwa karibu asilimia nane mara ya mwisho nilipoangalia. Mengi yanashikiliwa na taasisi za fedha za Japan na Benki ya Japan," Profesa Kuttner, anasema.

WAJUE MATAJIRI 10

Kipimo kinachotumiwa kutafsiri ama utajiri au umaskini wa nchi ni Pato la Taifa, linalojumlisha uzalishaji bidhaa na huduma za nchi katika kipindi fulani na kuchukuliwa kama kiashirio cha utajiri wa eneo hilo.

Kipimo hicho huisaidia serikali kujua  kiasi chake cha mapato, pia matumizi kwa huduma muhimu kama vile afya na elimu.

Kwa mujibu wa takwimu za Oktoba 2022 kutoka Shirika la Fedha la Kimataifa na Visual Capitalist, nchi hizo 10 tajiri duniani ni zifuatavyo, kiashiria ikiwa ni thamani ya Pato la Taifa katika thamani ya pesa, Dola za Marekani.:

1. Marekani; ina bilioni Dola 25.03.

2. China; Dola bilioni 18.321

3. Japan; Dola  bilioni 4.301 .

4. Ujerumani; Dola bilioni 4.031.

5. India - dola za Marekani bilioni 3.469

6. Uingereza; Dola bilioni 3.199.

7. Ufaransa; Dola bilioni 2.778.

8. Canada; Dola bilioni 2.2

9. Russia; Dola bilioni 2.113

10. Italia; Dola bilioni 1.997