Hivi Watanzania tunajisikiaje kubagaza Kiswahili

20Jan 2023
Joseph Kulangwa
DAR ES SALAAM
Nipashe
Hivi Watanzania tunajisikiaje kubagaza Kiswahili

KUNA nyakati, waandishi wa habari huonekana watu wa ajabu sana. Kwanini? Kwa sababu wanaweza kuwa wanaishi mahali fulani kuna habari, lakini wasiione.

 

Hubainika kuwa, hicho kilichoko ni habari baada ya mtu mwingine mgeni kufika mahali hapo na kubaini kuwa ipo habari na ndipo utaona waandishi hao nao kuichangamkia.

Hii ni kawaida kwa watu wote, kwamba unaweza kuwa na kitu kisicho cha kawaida nyumbani mwako, tena cha thamani kubwa, lakini usikione, mpaka aje mgeni akushtue.

Tanzania imekuwa hivyo siku zote, kwamba ina mambo mengi ya kifahari na ya kujivunia, lakini mara zote imekuwa ikijikuta ikijibeza yenyewe mpaka ishtuliwe.

Tumeshuhudia kwenye madini ya tanzanite, kwenye rasilimali zingine za wanyama na maliasili kedekede, zinazovutia mataifa mengine hata kuja kujionea kwa malipo.

Watanzania miaka nenda rudi tuliishi na vitu visivyo vya kawaida kama milima na hata maziwa, bila kujua kama vina thamani, mpaka walipokuja walioitwa wavumbuzi, kana kwamba hatukuwa tunaishi maeneo hayo.

Wakaja wengine, wakakuta tunatumia almasi kama kete kuchezea bao, wakatudanganya wakatubadilishia na shanga nasi tukakenua meno kwa furaha, huku wao wakinufaika nazo.

Tunajulikana duniani kama kitovu cha lugha ya Kiswahili, lakini bado hatuamini na tunaendelea kuamini Kiingereza! Dunia ina lugha zaidi ya 6,000, Kiswahili kikipewa nafasi ya saba, lakini bado hatuoni.

Dunia imetangaza Julai 7 ya kila mwaka kuwa Siku ya Kiswahili Duniani, lakini bado wazito, hatuelewi, tunashadidia Kiingereza na sasa tumeamsha mjadala wa Kiingereza kiendelee kutumika kufundishia na ikiwezekana hata chekechea!

Mtu na akili zake anasimama kadamnasi na kuhanikiza akilalamika kuwa inashangaza wanafunzi wa Kitanzania hawajui Kiingereza! Astaghafirulah, Kiingereza ni lugha mama ya Watanzania, kwamba asiyekijua hafai kuhesabiwa kuwa Mtanzania?

Yaani miaka yote hii ya uhuru, bado tunapanda basi la Kiingereza kweli? Inashangaza na kusikitisha, kuwa badala ya kusonga mbele tunarudi nyuma, hata hao wanaokiheshimisha Kiswahili, wanazidi kutushangaa.

Yaani mpaka leo hatujui kuwa kuna mataifa huko nje yanatamani kujua Kiswahili? Nchi jirani ya Kenya inajivunia Kiswahili kuliko hata sisi. Wamezagaa mataifani huko ughaibuni wakifundisha Kiswahili na kuaminisha kuwa chimbuko lake ni Kenya.

Leo, sisi badala ya kukitetea na kufanya haraka kutafsiri vitabu vya kiada na ziada vinavyotumika shuleni kufundishia, ndio kwanza tunakibagaza na kukiona kuwa ni cha kishenzi, kuwa aliyesoma ni anayejua Kiingereza.

Ugonjwa huu unatokana na ulevi tu, ambao unajibainisha pale baba mlevi anaporudi nyumbani kwake usiku na kugonga mlango huku akitukana: “You idiots open the door for me!” anafanya hivyo wakati mchana akiaga kwenda klabu cha pombe alifanya hivyo kwa Kiswahili!

Inashangaza kuwa si siku nyingi nyuma, tulishaamua (ingawa kinadharia) kuwa Kiswahili kitumike kufundishia shuleni, lakini sijui limetokea wimbi gani sasa tunajadili tena kitu kile kile, badala ya kusonga mbele, huku mahakamani baada ya tamko ilishaanza kutafsiri sheria!

Tatizo la Watanzania, ni wenye dhamana ambao wengi walisoma au kusomeshwa ughaibuni, ambako wanajua walilazimika kujifunza lugha za huko kabla ya kuanza mafunzo, ndio hao wanashadadia Kiingereza nchini.

Hawa ndio wenye watoto kwenye shule za Kiingereza wanazoziita za kimataifa na wengine wakisoma ughaibuni, lakini pamoja na kupewa nafasi serikalini, wanakuwa mstari wa mbele kukandamiza lugha mama yao!

Tulishakosea nyuma, kwa kuwa na utaratibu wa kufundisha masomo kwa Kiswahili kuanzia chekechea mpaka msingi na ghafla Kiingereza, sekondari mpaka vyuo. Hapo, lazima kigugumizi kiibuke katika Kiingereza.

Hivi tu ukiamua sasa, kwamba tunafundisha kwa Kiingereza tangu msingi, tunao hao walimu wakutufundishia watoto? Tufanye utafiti basi huko shuleni tuone kama tuna walimu wa Kiingereza hasa, kama siubabaishaji wa Yes! No!

Tukitaka kujijua tuko wapi, basi angalau siku moja ya Mkutano wa Bunge tuitenge mijadala iendeshwe kwa Kiingereza mchana kutwa, ndipo tutaona tunaning’inia wapi! Kiswahili ni lugha ya mama, hatujachelewa, tukae tutafsiri tufundishe kwa Kiswahili chekechea - chuo kikuu. Tujivunie kilicho chetu! Alamsiki!